PROFESSOR MWERA FOUNDATION KUWASOMESHA BURE WALIOACHA SHULE KWA UJAUZITO
>> Watajiunga na fani mbalimbali chuo cha Tarime Vocational Training College
>>Mkurugenzi Hezbon Mwera asema mpango huo ni wa miaka minne
>> Meneja NACTVET Kanda ya Ziwa aipongeza Taasisi kwa kuchapa kazi
Na Dinna Maningo, Tarime
MENEJA wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi Kanda ya Ziwa, Godfrey Muhangwa amezindua mpango wa kusaidia vijana wa Tarime pamoja na wasichana waliokatisha masomo baada ya kubeba ujauzito kuweza kusoma bure katika chuo cha mafunzo ya ufundi stadi Tarime maarufu Tarime Vocational Training College.
Mafunzo hayo yamefadhiliwa na Taasisi isiyo ya kiserikali hijulikanayo kwa jina la Professor Mwera Foundation yenye makao yake makuu mjini Tarime.
Akizindua mpango huo Meneja huyo aliyekuwa mgeni rasmi katika mahafali ya kwanza ya vijana waliohitimu masomo ngazi ya tatu ( Level 3 ) katika chuo cha Tarime VTC, ameipongeza taasisi hiyo ya PMF kwa kazi wanazozifanya.
Meneja wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi Kanda ya Ziwa, Godfrey Muhangwa akizindua mpango wa kusaidia vijana wa Tarime mjini na mpango wa kusaidia wasichana waliokatisha masomo baada ya kuwa wajawazito wakati wa mahafali ngazi ya tatu chuo cha Ufundi Stadi Tarime (TVTC)
" Kwa niaba ya Serikali naipongeza PMF kwa kazi nzuri, mnafanya mambo makubwa, serikali na wadau mbalimbali wanatambua mchango wenu.
" Mmeigusa Jamii ya Tanzania, mmetoa elimu bure kwa zaidi ya wanafunzi 5,000 hili sio jambo dogo. Kuna watu hawana uwezo, taasisi hii imeweza kusaidia kutoa elimu bure na huu ni mpango wa pili nimeuzindua mimi " amesema Godfrey.
Meneja huyo wa NACTVET amewaomba vijana waliohitimu kidato cha nne pamoja na wasichana walioacha shule baada ya kubeba ujauzito na kukatisha ndoto zao kuitumia fursa hiyo kujiunga na chuo katika fani mbalimbali kwani dunia ya sasa inazingatia umahiri katika utendaji wa kazi.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Profesa Mwera ambaye pia ni Mwenyekiti wa Wakuu wa Vyuo vya Ufundi Kanda ya Ziwa, Hezbon Mwera (kushoto aliyevaa koti) akiteta jambo na Meneja wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi Kanda ya Ziwa, Godfrey Muhangwa, kulia ni Mkuu wa chuo cha Tarime Vocational Training College, Mary Daniel
" Namshukuru mkurugenzi kwa kunialika najua Hezbon ni mchapa kazi na mpenda maendeleo. Niwapongeze wahitimu kwa kuhitimu, lakini niwaombe mkawe mabalozi wazuri kuhamasisha vijana waliohitimu kidato cha nne pamoja na wadada waliokatisha masomo kwa ujauzito waje hapa chuoni kujiunga na masomo yatakayotolewa bure " amesema Godyfey.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Profesa Mwera ambaye pia ni Mwenyekiti wa Wakuu wa Vyuo vya Ufundi Kanda ya Ziwa, Hezbon Mwera mesema taasisi imeandaa mpango wa kuwasomesha bure vijana wa Tarime mjini waliohitimu kidato cha nne pamoja na wasichana waliokatisha masomo yao baada ya kubeba ujauzito.
Amesema kuwa wasichana waliokatisha masomo kwa ujauzito ni kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara watasoma bure ambapo mpango huo ni wa miaka minne kwa mwaka 2024 hadi 2028.
"Mpango wa kusaidia vijana wa Tarime kusoma bure hapa chuoni tumeshasomesha bure vijana zaidi ya 5000 ambapo kama ingekuwa ni kulipia tungeingiza zaidi ya Tsh. Milioni 6 kutokana na ada ambazo wangelipa.
" Huo ulikuwa ni mchango wetu kwa jamii na mpango huu unaendelea kwa vijana wa Tarime wa kiume na w kike waliohitimu kidato cha nne na wadada waliokatisha masomo kwa ujauzito.
Mkurugenzi huyo ameliomba Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na mafunzo ya Ufundi Stadi kukipatia chuo usajili ili kiweze kutoa mafunzo kwa ngazi ya Stashahada.
Mkurugenzi wa PMF Hezbon Mwera akiteta jambo na Meneja wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi Kanda ya Ziwa, Godfrey Muhangwa
"Tunaishukuru Serikali kwa ushirikiano katika sekta hii ya elimu na mafunzo. Pia tunakushukuru Meneja wa NACTVET kwa kukubali kuja kushirikiana na sisi kwenye mahafali haya. Umeleta mapinduzi mazuri ndani ya Kanda ya Ziwa, umekuwa mtu wa kuitikia pale unapoitwa kwenye matukio unakuwa ni mwepesi kufika.
"Chuo chetu kina usajili wa kutoa mafunzo ngazi ya Certificate ( Astashahada) Tunakuomba Meneja wa NACTET utusaidie tupate usajili mapema kwa ngazi ya Diploma ( Stashahada) tukipata mapema tutatoa ofa kwa hawa wahitimu 33 kusoma bure diploma katika fani mbalimbali hapa chuoni kama mfano " amesema Hezbon.
Akisoma Risala ya chuo, Mkuu wa chuo cha Tarime Vocational Training College, Maria Daniel amesema chuo hicho kilisajiliwa mwaka 2015 na kuanza kutoa mafunzo ya ufundi stadi.
" Chuo kinatoa kozi za muda mrefu kama vile ufundi umeme wa majumbani, Ushonaji, kudalizi, magari, masomo ya biashara, uchomeleaji wa vyuma, uhaziri na zinginezo.
" Mafunzo ya muda mfupi ya miezi mitatu na miezi sita kama vile kompyuta, udereva, video production, uchomeleaji vyuma, utengenezaji wa sabuni na zinginezo. amesema. mkuu wa chuo.
Ameongeza kuwa jumla ya wahitimu 33 ngazi ya tatu (Level 3 ) wanatarajia kufanya mtihani wa kuhitimu Juni, 17, 2024, ambapo wakati wanajiunga chuo walikuwa 250.
"Walijiunga chuo mwaka 2021 katika kozi tofauti tofauti wakiwa wanafunzi 250 na ilipofika 2022 walifanya mtihani wa kuingia mwaka watatu wanafunzi 200, mpaka leo hii wanaotarajia kufanya mtihani ni wanafunzi 33.
" Tuna changamoto ya idadi ya wanafunzi kupungua toka ngazi moja na nyingine kutokana na mtazamo hasi, wanapokuwa wamefanya mtihani ngazi mojawapo na kupewa vyeti wanalidhika kuwa wamehitimu masoma na kutoendelea na ngazi nyingine" amesema.
Mkuu huyo ametaja changamoto nyingine ni upungufu wa maktaba toshelezi, bohari muhimu na kwamba chuo kinafanya jitihada kuhakikisha mahitaji hayo yanapewa kipaumbele.
Meneja wa Taasisi ya Profesa Mwera, Mwita Samson Marwa amesema Taasisi inaendelea na utafiti wa kubaini mambo ambayo yatakuwa ya msaada mkubwa kwa vijana na jamii.
Akisoma Risala ya wanafunzi waliohitimu ngazi ya tatu katika chuo, Zainabu Hussein amewapongeza walimu na wafanyakazi wa chuo cha Tarime Vocational Training College kuhakikisha wanapata elimu pamoja na malezi bora wawapo shuleni.
" Mafanikio ya chuo ni pamoja na shule kuwa na usafiri, juhudi za kitaaluma zilizowezesha wao kupata maarifa, maabara kwa ajili ya kujisomea kwa vitendo, mafunzo ya ujasiliamali, kuwepo kwa kamera chuoni kwaajili ya kuimalisha ulinzi kwa wanafunzi pamoja na kuwepo vyombo vya muziki vya kujifunzia wanaosoma fani ya muziki.
" Pamoja na mafanikio kuna baadhi ya mapungufu yakiwemo ya kotokuwepo nishati mbadala ya sola pindi umeme wa TANESCO unapokatika huwa hatujisomei, maji ni shida yakikatika tunalazimika kwenda kutafuta kwenye vyanzo vingine vya maji" amesema Zainabu.
Katika Mahafali hayo burudani mbalimbali zilitumbuizwa wakiwemo wachezaji wa mchezo wa Karate kutoka kikundi cha Tarime Shotokan Karate club ambao walionesha umahiri wapo.
Pia Burudani za vichekesho ,burudani kutoka Mwera Jazz Band, na zinginezo. Pia wahitimu walionesha kwa vitendo jinsi walivyopata mafunzo yakiwemo ya utengenezaji batiki, mafuta ya kujipaka.
Vijana wakionesha umahiri wao katika mchezo wa Karate kutoka kikundi cha Tarime Shotokan Karate club
Meneja wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi Kanda ya Ziwa, Godfrey Muhangwa wapili kushoto akitizama vitendo kwa wanafunzi wa kozi ya utalii
Wanafunzi wakionesha mazoezi kwa vitendo kwa kutengeneza mafuta ya mgando
Wanafunzi wakionesha mazoezi kwa vitendo kwa kutengeneza Batiki
Post a Comment