HEADER AD

HEADER AD

TFS YAKERWA UCHOMAJI MOTO MISITU YA HIFADHI BIHARAMULO

Na Daniel Limbe, Biharamulo

WAKATI Tanzania ikiungana na nchi zingine kuadhimisha wiki ya mazingira duniani, Wakala wa huduma za misitu (TFS) Wilayani Biharamulo, mkoani Kagera imeeleza kukerwa na vitendo vya wananchi kuchoma ovyo misitu ya hifadhi kinyume cha sheria.

Licha ya kujivunia mafanikio makubwa ya kudhibiti uvamizi wa msitu ya hifadhi kwenye pori la Biharamulo na Nyantakara Kahama, bado suala la uchomaji moto limeonekana kuwa sugu unaofanywa na wananchi kwa kuchoma mkaa,kukata miti kwaajili ya shughuli za uchimbaji madini,kupasua mbao,kilimo na malisho ya mifugo.

Meneja wa Wakala wa huduma za misitu(TFS) wilayani Biharamulo, Goodluck Malisa, amesema licha ya kuendelea kuelimisha wananchi kuacha kuvamia msitu ya hifadhi bado hawaachi huku akitahadharisha watakao kamatwa wakitekeleza uharibifu huo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

     Meneja wa Wakala wa Huduma za Misitu(TFS) wilaya ya Biharamulo, Goodluck Malisa .

Amesema bado kuna haja kubwa kwa madiwani wa halmashauri hiyo kushirikiana na wakala wa huduma za misitu nchini kuwaelimisha wananchi faida za kuhifadhi misitu na madhara ya yanayoweza kutokea iwapo misitu itatoweka.

Diwani wa Kata ya Nyakanazi, Amos Madebwa, ameomba Wakala wa huduma za misitu wilayani humo, kufumbia macho baadhi ya makosa ya wananchi wanaokutwa na mkaa chini ya gunia moja ili kuwanusuru na chaguzi zijazo za serikali za mitaa na uchaguzi mkuu.

"Watu wanatoka na vifurushi vidogo vya mkaa unakuta askari wa TFS wamewasubiria kijijini,ikumbukwe tunakwenda kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa, juzi nilipigiwa simu nikaambiwa mnaharibu, kama mtu anatoka na kamkaa kake halafu anakamatwa hiyo ni shida" amesema Madebwa.

Diwani wa kata ya Kabindi, Philibert Rubula, ameiomba TFS kupunguza ukali wa adhabu kwa wananchi wanaojishughulisha na biashara ya mkaa na kwamba wajikite kutaitaifisha mkaa pekee badala ya kuwanyang'anya hadi vitendea kazi vyao kama vile baiskeli na pikipiki kwa madai zana hizo huwasaidia kuhudumia familia ikiwemo Kubeba wagonjwa wao kwenda kwenye huduma za afya.

Hata hivyo, mwenyekiti wa halmashauri hiyo,Leo Rushahu, amewataka TFS kuendelea kusimamia sheria kwa lengo la kunusuru uharibifu mkubwa wa misitu ambao usipodhibitiwa unaweza kuhatarisha wilaya hiyo kugeuka jangwa.

        Mwonekano wa moto ukiteketeza misitu ya hifadhi na kuharibu maisha ya viumbe hai wengine.

No comments