ASKOFU MSONGAZILA, DC TARIME, NYAMBARI NYANGWINE WASISITIZA AMANI
>>DC Tarime awataka MA- OCD kushirikiana na Wazee wa mila
Na Dinna Maningo, Tarime
WANANCHI wametakiwa kudumisha amani kwani mahali kusipokuwa na amani hakuna maendeleo huku wakikumbushwa kuepuka mapigano na badala yake waishi kwa kupendana.
Askofu wa Jimbo Katoriki Musoma , Michael Msongazila amesema kuwa Taasisi za Dini na Taasisi za amani zimechangia kudumisha amani kwa kuzunguka wilaya kuhubiri amani.
Askofu wa Jimbo Katoriki Musoma Michael Msongazila akizungumza wakati wa harambee ya ujenzi wa Kanisa
" Kwa kipindi changu kama askofu cha miaka 16 ninaona amani, amani ipo katika mkoa wa Mara na ninasema bila kumumunya taasisi za kanisa ,taasisi za amani zimechangia kudumisha amani.
" Mungu katujalia mvua tunapata chakula tunashiba kwanini tupigane, ni kufuru kwa Mungu. Tutengeneze haki tutengeneze upendo kwa jirani" amesema Michael.
Ameongeza " wakati nilipokuwa askofu niliulizwa wewe sasa mpango mkakati wako ni upi katika kusimamia amani? miaka hiyo ya 2006 na 2007 vilitokea vita watu wakapigana wakakatana mapanga na kuuana, mazao yakagekwa watu wakishindwa kutembea kwa amani. Tulizunguka kuhimiza amani" amesema.
Askofu wa Jimbo Katoriki Musoma Michael Msongazila akisalimiana na mzee wa wazee wa Mila (Msubi) baada ya kumsimika Askofu huyo kuwa Msubi wa tatu.
Amewasisitiza waumini kudumisha amani " Na sisi kila tunapomaliza misa tunasema nendeni kwa amani tunaitikia tumshukuru Mungu. Haikueleweka kichwani mwangu unawaambia nendeni kwa amani alafu wanatoka nje wanaanza kupingana".
Ameongeza kuwa kwa sasa anamshukuru Mungu kutokana na amani iliyopo Mara ambapo amewashukuru viongozi wa dini, taasisi za amani, serikali na jamii kwa ujumla kudumisha amani na kuwataka waendelee kuidumisha amani.
Amewapongeza viongozi wa serikali , vyama , makundi mbalimbali kwa huduma ambazo zinafanyika inapokazaniwa amani na maendeleo na kwamba hakuna maendeleo bila amani na hakuna amani bila maendeleo.
Mkuu wa wilaya ya Tarime Edward Gowele amewaomba wazee wa mila kusisitiza amani kwani amani isipokuwepo hakuna maendeleo.
" Nawashukuru Wazee wa mila kwa kazi kubwa mliyoifanya mpaka sasa kwa kusimamia amani na utulivu kwenye koo zao na kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia kwenye jamii kuhakikisha vinatokomezwa kwani vitendo hivyo vinapoteza amani kwenye jamii.
Amewaagiza ma-OCD kushirikiana na Wazee wa mila " Tushawishi jamii zetu kuepuka vitendo vya ukatili, wizi, mauaji. Najua wana taratibu zao na nimeagiza ma OCD wote kushirikiana na Wazee wa mila kukemea vitendo vya wizi, mauaji .
"Niwahakikishie nitasimamia vijana wetu waweze kupata manufaa kwenye maeneo yetu, tayali tumeshaanza kufanya hiyo kazi na muda sio mrefu mtaona matokeo ili vijana waweze kushiriki uchumi kwenye maeneo yetu " amesema DC Edward.
Aliyewahi kuwa mbunge wa Jimbo la Tarime, Nyambari Nyangwine amesisitiza upendo na kusema kusipokuwepo upendo amani inakosekana huku akikumbuka wakati akiwa mbunge jinsi viongozi wa dini na wazee wa mila walivyoweza kudumisha amani na kudumisha upendo katika wilaya ya Tarime baada ya mapigano ya koo yaliyotokea 2006 na 2007 .
Nyambari Nyangwine pamoja na wadau wa maendeleo waliofika kanisani kwenye harambee ya kuchangia ujenzi wa Kanisa
Post a Comment