HEADER AD

HEADER AD

SHUGHULI ZA BINADAMU KWENYE SHOROBA CHANZO CHA MIGOGORO

Na Daniel Limbe, Biharamulo

IMEELEZWA kuwa shughuli za kibinadamu ikiwemo kilimo na ufugaji kwenye njia za wanyamapori ni chanzo kikuu cha ugomvi wa binadamu na wanyama .

Hayo yamesemwa wilayani Biharamulo mkoani Kagera na Mhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa(TANAPA) Burigi -Chato, Ayubu Nyakunga, wakati akitoa ufafanuzi wa malalamiko ya wananchi dhidi ya wanayamapori ambao ni waharibifu wa shughuli za kibinadamu.

      Mhifadhi wa Hifadhi ya taifa ya Burigi-Chato,Ayubu Nyakunga.

Wananchi amelalamika uwepo wa nyani wanaohatarisha maisha ya watu ikiwemo kushambulia mazao shambani hali inayotishia baadhi ya kaya kukumbwa na njaa.

Wamelalalamikia tukio la hivi karibuni kwenye kijiji cha Lusabya, ambapo nyani walitwaa mtoto mdogo na kuondoka naye kabla ya wananchi kuwakimbiza na kuwanyang'anya huku akiwa amejeruhiwa sehemu za uso na masikio.

Mhifadhi huyo amesema changamoto kubwa iliyopo ni kuendelezwa kwa shughuli za kibinadamu kwenye shoroba za wanyamapori na kwamba wanyama wanapokuta mazao kwenye maeneo hayo huyashambulia na wakati mwingine kuingia kwenye makazi ya watu.

       Mwonekano wa mnyama Kiboko

"Licha ya elimu ambayo imekuwa ikitolewa mara kwa mara kwa wananchi wanaoishi kwenye vijiji vinavyopakana na hifadhi ya taifa ya Burigi-Chato bado jamii imekuwa haitaki kuheshimu maeneo hayo hivyo kusababisha ugomvi wa watu na wanyamapori" amesema.

Amekanusha taarifa za kwamba TANAPA inathamini zaidi wanyama kuliko binadamu na kwamba uwepo wa wanyamapori husaidia pia kuimarika kwa uhifadhi wa misitu na usalama wa viumbe wengine hai katika jamii.

Amewataka wananchi kuendelea kushirikiana na serikali kwa kuwapatia haraka taarifa za matukio ya wanyamapori wanapoingia kwenye makazi ya watu ili iwe rahisi kwao kuwadhibiti kabla ya kusababisha madhara kwa jamii na kwamba suala la uhifadhi halitegemei taasisi moja bali ni suala la kila mtanzania.

Kwa mujibu wa matukio ya migongano baina ya wanyamapori na binadamu yalikuwa 997 mwaka 2018, lakini yameongezeka kwa kasi hadi kufikia matukio 3,496 mwaka jana huku mengi yakihusisha uvamizi wa tembo.

Takwimu za mwaka 2023/24 zinaonyesha kuwa wilaya ya Manyoni mkoani Singida ilikuwa na matukio 410,Nachingwea matukio 312,Lindi 260,Tunduru 218,Busega 214,Rufiji 202,Bunda 158,Liwale 112 na Chamwino matukio 111.

Imeelezwa kwamba tembo wamekuwa wakichangia kwa aslimia 80 kwenye migongano hiyo wakifuatiwa na Simba aslimia 6,Kiboko aslimia 5,Kifaru aslimia 4,Mamba aslimia 3 na Fisi aslimia 2.

Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Biharamulo, Leo Rushahu, amewataka TANAPA kuwadhibiti wanyama hao ikiwemo Nyani na viboko ambao wamekuwa wakiripotiwa kuharibu mashamba ya wananchi kwenye vijiji vya Kalenge,Msekwa na Kanyoni ili wasiendelee kuleta madhara kwa umma.

Pia ameshauri zifanyike oparesheni za kuwadunga sindano za usingizi ili waweze kuwahamisha kwenye maeneo ya makazi ya watu sambamba na kuitaka jamii kuacha kufanya kazi kwenye njia za wanyamapori ili kuepuka migogoro isiyokuwa ya lazima.

                         

No comments