HEADER AD

HEADER AD

WANANCHI KIGOMA WAHIMIZWA KUBORESHA TAARIFA UCHAGUZI SERIKALI MITAA

Na Daniel Limbe, Kakonko

SERIKALI mkoani Kigoma imewataka wananchi kujitokeza kwa wingi ili kuboresha taarifa zao kwenye daftari la Makazi kwaajili ya uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2024.

Uboreshaji wa taarifa hizo hautahusiana na uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani wa mwaka 2025 badala yake utahusika kuwapata wenyeviti wa mitaa, vijiji, vitongoji na wajumbe wao.

Imeelezwa hatua hiyo itawasaidia wananchi kufanya uamuzi sahihi wa kuwachagua viongozi wanaowataka kuanzia ngazi ya chini kwa lengo la kuharakisha maendeleo wanayokusudia katika maeneo yao.

Kaimu Katibu tawala mkoa wa Kigoma, Aman Kanguye, amesema ni muhimu wananchi watofautishe taratibu za uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu wa Rais,Wabunge na Madiwani.

         Madiwani wakiendelea na mijadala mbalimbali

Ametoa wito huo wilayani Kakonko mkoani Kigoma huku akiwataka viongozi kuwa mstali wa mbele kuwaelimisha wananchi utofauti wa chaguzi hizo ili wasipoteza haki zao za msingi kuwachagua viongozi wao.

"Nitumie nafasi hii kuwataka wananchi wajitokeze kwa wingi kwenye vituo vya kujiandikishia kwaajili ya kuboresha taarifa zao kwenye daftari la makazi kuanzia Oktoba, 11, hadi Oktoba 22, 2024" amesema" Kanguya.

Mkuu wa wilaya ya Kakonko,Col. Evance Mallasa, amesema serikali ya wilaya hiyo itaweka utaratibu mzuri wa kutoa elimu kwa jamii ili watambue tofauti ya chaguzi hizo mbili.

         Mkuu wa wilaya ya Kakonko,Col. Evance Mallasa akizungumza na madiwani.

Hata hivyo amewatahadharisha wale wote wanaotambua kuwa siyo raia wa Tanzania kutojipenyeza kwenye uandikishwaji wa daftari la makazi na kwamba atakaye bainika sheria kali itachukua mkondo wake.

Tahadhali hiyo imetolewa kutokana na wilaya hiyo kuwa mpakani mwa nchi jirani ya Burundi, ambako baadhi ya raia kutoka nchi hiyo hujipenyeza kupitia njia za panya na kuingia nchini kinyume cha sheria za nchi.

Akizungumza kwenye kikao cha madiwani wa halmashauri hiyo, Mkurugenzi wa halmashauri hiyo,Ndaki Stephano, amesema wananchi wanapaswa kutumia fursa hiyo kutimiza haki yao kikatiba kuwachagua viongozi wanao wahitaji katika uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2024 na ule mkuu hapo mwakani.

     Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Kakonko, Ndaki Stephano,akitoa ufafanuzi mbele ya madiwani.

"Kama viongozi wa halmashauri pamoja na ninyi madiwani tunapaswa kuungana pamoja kuwahamasisha na kuwaelimisha wananchi wetu wajitokeze kwa wingi kwenda kuboresha taarifa zao ili wakidhi vigezo vya kupiga kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa"amesema Ndaki.

"Tunatambua ninyi mnaishi na wapiga kura huko na ninyi mnasikilizwa sana na wananchi,wahamasisheni wajitokeze kwa wingi ili wasipoteze fursa hii maana inapatikana mara moja kwa kila baada ya miaka mitano".

                      

No comments