HEADER AD

HEADER AD

TFS, CBCC, CBFF WAFANYA MKUTANO KUKABILIANA NA CHANGAMOTO MABADILIKO TABIANCHI

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

KATIKA juhudi za kuboresha uhifadhi wa mazingira nchini, Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania TFS, imefanya mkutano na Kamisheni ya Tabianchi ya Bonde la Congo (CBCC) pamoja na Mfuko wa Bluu wa Bonde la Congo (CBFF) jijini Dodoma. 

Mkutano huo umejikita katika kuimarisha mikakati ya pamoja ya kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi na kuongeza ushirikiano kati ya pande hizo tatu katika juhudi za kulinda mazingira na kuendeleza uhifadhi.

Akiongea na waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa kikao cha ndani, Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dk. Pindi Chana (Mb)amesema mkutano huo unalenga kuimarisha juhudi za kulinda mazingira za kikanda na kukuza suluhu za pamoja kwa mabadiliko ya hali ya hewa na uhifadhi wa utofauti wa kibaiolojia katika Bonde la Congo na zaidi.


“Mkutano huu una maana kubwa kwa Tanzania, kama mwanachama wa CBCC, tunakwenda kunufaika na utaratibu wa pamoja wa usimamizi wa rasilimali za maliasili, rasilimali fedha, na kuimarisha mifumo ikolojia ya eneo letu kupitia Mfuko wa Bluu wa Bonde la Congo pamoja na Benki ya Maendeleo ya Nchi za Kati za Afrika (BDEAC) katika kutekeleza makubaliano ya utunzaji Mazingira ya kimataifa, ikiwa ni pamoja na Mkataba wa Paris na malengo ya maendeleo endelevu. 

Ameongeza kuwa kupitia mfuko wa bluu wa Bonde la Congo nchi wanachama 16 zinapata fursa mbalimbali ikiwemo kuandika miradi na kuomba mashirikiano katika kuhakikisha mazingira yanahifadhiwa hasa katika kipindi hiki ambapo kumekuwa na ongezeko kubwa la watu duniani.

Amesema kutokana na ongezeko hilo la watu duniani nchi wanachama zimeona kuna umuhimu wa kuungana na kuwa na sauti ya pamoja katika majadiliano ya kimataifa kuhusu usimamizi wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi, huku zikichangia uzoefu wao na kupokea maarifa mapya kutoka kwa nchi nyingine wanachama utakaosaidia uboreshwaji wa sera. 

Aidha, kupitia mkutano huo wamezungumza mambo kadhaa ikiwemo namna gani nchi wanachama zinaweza kuendeleza mfuko wa Bluu wa Bonde la Congo lakini pia kuongeza uwezo wa wataalamu katika  kulinda mazingira na maboresho ya sera ili mazingira yasiharibiwe.

Waziri wa Utalii na Mazingira wa Jamhuri ya Congo na Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Tabianchi ya Bonde la Congo (CBCC), Arlette Soudan – Nonault amesema pamoja na mambo mengine wamefanikiwa kukubaliana mambo mbalimbali.


Baadhi ya mambo hayo ni pamoja na kujua namna gani wanaweza kuzisaidia nchi wanachama kupata fedha ambazo tayari zimewekwa katika mfuko wa blue na benki mbalimbali wanazofanya nazo kazi kwa ajili ya kuendeleza shughuli za utalii na mabadiliko ya tabianchi.

Amesema kamisheni hiyo pia itashirikiana na mashirika mbalimbali yasiyo ya kiserikali ili kufanikisha dhamira ya kamisheni hiyo.

" Katika kuhakikisha hilo mwakani kutakuwa na mkutano mkubwa wa wakuu wa nchi kwa ajili ya kusaidia kamisheni hiyo kufanya kazi huku akisisitiza kuanzisha kwa redio na luninga itakayofanya kazi kwa lugha nne ambapo nchi wanachama zitashiriki kutoa maudhui".

Makamu wa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Nchi za Kati za Afrika (BDEAC) Megne Ekogana Msimamizi Mkuu wa shughuli za utawala wa kamisheni hiyo amesema jukumu lao kubwa ni kuratibu upatikanaji wa fedha zitakazozisaidia nchi wanachama na mashirika yasio ya kiserikali kuisaidia kamisheni hiyo kufikia malengo yake.

Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) na mwakilishi wa nchi katika mfuko wa Blue wa Bonde la Congo, Prof. Dos Santos Silayo amesema kamisheni hiyo ilianzishwa na inaundwa na nchi ambazo kijiografia, kiikolojia pamoja na kiuchumi zina uhusiano mkubwa katika kulinda na kuhifadhi bionuai na misitu ya bonde na mito ya Congo, ambayo ina umuhimu mkubwa katika ustamilivu wa bonde la Congo. 

“Tanzania ni nchi ya kimkakati katika kamisheni hii, ujio huu unalenga kuhamasisha vyombo vya serikali na sekta binafsi ili ziweze kujua ni nini kinafanywa na kamisheni na ugeni huu utakuwa nchini kwa siku tano na utakutana na wadau mbalimbali na sisi kama Taifa tumeingia kushirikiana nao kuimarisha ustamilivu wa rasilimali misitu na wanyamapori,” amesema.

Kamisheni ya Tabianchi ya Bonde la Kongo inajumuisha nchi ya Angola, Burundi, Cameroon, Jamhuri ya Kati ya Afrika, Chad, Jamhuri ya Congo, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Guinea Ikweta, Ufalme wa Morocco, Gabon, Kenya, Rwanda, Sao Tome na Principe, Sudan Kusini, Tanzania, Uganda, na Zambia.





No comments