HEADER AD

HEADER AD

BASHUNGWA AWAHAKIKISHIA WANANCHI WA MLANDIZI UJENZI BARABARA YA LAMI

Na Gustaphu Haule, Pwani

WAZIRI wa Ujenzi Innocent Bashungwa amewahakikishia wakazi wa Mamlaka ya Mji mdogo wa Mlandizi iliyopo Kibaha Vijijini kuwa Serikali itafanya jitihada kuhakikisha inajenga kwa kiwango cha lami barabara ya kilomita 23 inayoanzia Mlandizi stendi kuelekea kituo cha reli ya mwendokasi ( SGR) kilichopo Ruvu Stesheni.

Bashungwa ametoa kauli hiyo Oktoba 8, 2024 wakati akizungumza na wakazi hao katika mkutano wake wa hadhara aliohufanya katika Kata ya Janga ikiwa ni sehemu ya ziara yake wilayani Kibaha.

     Waziri wa ujenzi Innocent Bashungwa akizungumza na Wananchi katika moja ya mikutano yake ya hadhara aliyoifanya Oktoba 8 ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo aliyoifanya Wilayani Kibaha mkoani Pwani.

Bashungwa amesema kuwa barabara ya Mlandizi inayoelekea katika kituo cha reli ya mwendokasi Ruvu ni muhimu kwakuwa ikikamilika itawasaidia Wananchi wanaotumia reli hiyo kusafiri kirahisi.

Amesema kuwa si tu kufika katika kituo cha reli hiyo lakini pia kujengwa kwa barabara hiyo kutasaidia kufungua fursa za uchumi kwa Wananchi sambamba na kuweka mazingira mazuri kwa wawekezaji wa viwanda katika maeneo hayo .

"Nimepita katika barabara hii nimegundua ina umuhimu mkubwa kwakuwa inaelekea katika reli yetu ya mwendokasi kituo cha Ruvu Stesheni ,hospitali ya Wilaya na hata katika eneo la uwekezaji wa viwanda hivyo nitakwenda kuifanyiakazi ili kusudi tuweze kuijenga kwa kiwango cha lami,"amesema Bashungwa 

Bashungwa amesema kuwa wakati zikisubiliwa fedha za ujenzi huo kwa kiwango cha lami kuna haja ya kuanza kuikarabati kwa kiwango cha changarawe ili iweze kupitika.

Amemuagiza Meneja wa Barabara ( TANROADS) Mkoa wa Pwani, Baraka Mwambage kufanya utaratibu wa kumpata mkandarasi ambaye atairekebisha na kuiweka sawa ili hiweze kupitika kwa urahisi na hivyo kupelekea shughuli za kiuchumi na masuala mengine yaweze kuendelea.

     Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa ( katikati)akikagua ujenzi wa Soko la kisasa jana linalojengwa katika Halmashauri ya Kibaha Vijijini Mkoani Pwani na Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge.

Amesema kuwa anafahamu barabara hiyo ni ndefu kwakuwa inaunganisha Bagamoyo- Makofi - Mlandizi - Mzenga  Maneromango mpaka vikumburu lakini ni vizuri ikaanza kujengwa kidogokidogo kuliko kusubiri mpaka fedha zote.

Amewaomba Wananchi kuwa wavumilivu wakati Serikali ikiendelea kuweka jitihada na mikakati mbalimbali ya kuhakikisha barabara hiyo inajengwa kwani anaamini Rais Samia ni Rais wa vitendo na kila jambo litatekelezwa kulingana na mipango iliyopo.

Wakati huohuo,  Waziri Bashungwa amewahamasisha Wananchi kujitokeza katika kushiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Vitongoji ikiwa pamoja na kujiandikisha katika daftari la wapiga kura ili kusudi muda ukifika wapate fursa ya kuchagua viongozi wazuri watakaowaletea maendeleo.
 
Akiwa Wilayani Kibaha Bashungwa ametembelea mradi wa Zahanati uliopo Kata ya Msangani, mradi wa ujenzi wa Sekondari Kata ya Viziwaziwa katika Halmashauri ya Kibaha Mjini huku Halmashauri ya Kibaha Vijijini ametembelea hospitali na ujenzi wa Soko la kisasa.

         Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa akikagua hospitali ya Halmashauri ya Wilaya Kibaha Mkoani Pwani katika ziara yake aliyoianza Oktoba 8 Mkoani Pwani


Naye Mkuu wa mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amesema kuwa barabara hiyo ikijengwa itafungua fursa nyingi kiuchumi ambapo pia amemuomba Waziri Bashungwa kutoa kipaumbele kwa barabara zote zinazopita kwenye miradi  ya kimkakati ili kusudi wawekezaji waweze kuja kwa wingi.

Pamoja na mambo mengine Kunenge ametumia fursa hiyo kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kazi anayyoifanya hususani kwa Wananchi wa mkoa wa Pwani.

        Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge akizungumza katika moja ya mikutano katika ziara ya Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa aliyoanza kuifanya Oktoba 8 katika Halmashauri ya Kibaha Mjini na Kibaha Vijijini Mkoani Pwani.

Kunenge, amesema kuwa katika kipindi cha miaka mitatu ya Rais Samia Mkoa wa Pwani umepokea jumla ya Tsh. Trilioni 1.3 fedha ambazo zimekwenda kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa Shule,vituo vya afya, maji barabara, umeme na hata masuala mengine.

Hata hivyo, Kunenge amesema kazi kubwa wanayoifanya ni kuhakikisha wanazisimamia fedha hizo ili kusudi zifanyekazi iliyokusudiwa na kwa upande wa mkoa wake fedha hizo zimefanya mambo makubwa na kufanya mkoa kupiga hatua kubwa ya kimaendeleo.


No comments