SERIKALI ILIVYOWASHIKA MKONO WAFUGAJI WA SAMAKI KWA NJIA YA VIZIMBA KAGERA
>>Waeleza mkopo wa Milioni 117 usio na riba utakavyokuza uchumi wao
Alodia Babara, Bukoba
KIZIMBA ni mfumo wa kufugia samaki waliowekwa kwenye nyavu iliyozungushwa kwenye fremu na kutumbukizwa kwenye maji yenye kina kirefu, mfano bwawa, ziwa au bahari.
Ufugaji huu unaruhusu kuweka samaki wengi katika eneo dogo hivyo unafaa mtu kufanya ufugaji wa kibiashara.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuwakomboa wananchi wake na umaskini, imeanzisha mpango wa ufugaji samaki kwa njia ya vizimba na kutoa mikopo ya miaka mitano isiyokuwa na riba kwa ajili ya vifaa vya uvuvi, vifaranga vya samaki na chakula ili kuwezesha wananchi kukuza uchumi wao kupitia ufugaji huo.
Serikali imefanya hivyo kwakuwa samaki ni chanzo bora cha protini na chenye usalama wa chakula na lishe kwa watanzania.
Mkoa wa Kagera ni miongoni mwa mikoa inayofuga samaki kwa njia ya vizimba na tayari vikundi na watu binafsi 12 wameanza kunufaika na ufugaji huo.
Jasson Mnubi ni mwenyekiti wa kikundi cha ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba kilichopo kata ya Kemondo (UFUKI) halmashauri ya Bukoba mkoani Kagera.
Kikundi chao kina wanachama 15 wanawake watatu na wanaume 12, wamenufaika na mkopo wa Tsh. Milioni 117.
Anasema wamejenga vizimba vinne na kufuga vifaranga vya samaki zaidi ya elfu 74,000. Wameanza ufugaji huo Julai, mwaka huu na wanatarajia kuvuna kati ya Desemba mwaka huu hadi Januari, mwaka kesho.
Mnubi anasema watakapovuna kwa awamu ya kwanza watalipa sehemu ya mkopo wao kwa asilimia 15 ambao ni mkopo wa miaka 5 na kwamba hadi kumaliza mkopo wao watakuwa waameishavuna samaki awamu 10 na wanatarajia kupata faida itakayoinua vipato vyao.
"Baada ya kuvuna samaki hao na kuwauza tutanunua vifaranga wengine na kuwapandikiza katika vizimba vyetu vinne na gharama za chakula tunatarajia tutakuwa tunatumia Tsh. Milioni 63 na gharama za kununua vifaranga ni Tsh. Milioni 12" anasema Mnubi.
Anawasihi wananchi wa mkoa wa Kagera kuona umuhimu wa mradi huo kujiunga na vikundi na mtu mmoja mmoja ili waweze kununufaika na kuongeza uchumi wao.
Anasema ufugaji huo una tija kubwa kwa viumbe wa majini hasa samaki wanaofugwa kwenye vizimba wanakula chakula majini wanacholishwa na wafugaji.
Anasema chakula hicho kinawasaidia waweze kukua haraka na ufugaji wa vizimba unasaidia kupunguza uvuvi haramu kwa kuwa samaki wanakuwa na muda wao wa kuvunwa wanapofikisha gramu 500.
Mwenyekiti wa umoja wa kikundi cha kufuga samaki Rubafu (UKISAKARU) Erenesti Galora kutoka halmashauri ya Bukoba anaeleza kwamba, kikundi chao kina wanachama 27, wanawake watano na wanaume 22 wamepata vizimba vitatu wanafuga samaki aina ya sato na mkopo wao ni wa Tsh Milioni 88.
Galora anataja lengo la kikundi chao ni kufuga samaki ili kujiondoa kwenye wimbi la umaskini na kwamba njia ya kufuga samaki katika vizimba ni njia nzuri na inasaidia kuwalinda samaki.
"Kutokana na thamani ya mkopo wetu tulitengenezewa vizimba vitatu, tukapewa vifaranga 53, 760 na tunapewa chakula cha samaki kwa awamu tatu hatua ya kwanza samaki wakiwa vifaranga, hatua ya pili samaki wakianza kukua na hatua ya tatu na ya mwisho samaki wanapokuwa wamefikia hatua ya kuvunwa" anasema Galura.
Anawasihi wananchi wenzake kuchangamkia fursa ya kuomba vizimba ili waweze kufuga samaki kwani maeneo tayari yameishapimwa na kugharamiwa na serikali.
Alinda Kiiza ni mama anayefanya ujasiriamali wa dagaa wabichi anasema ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba utawasaidia akina mama kupata ajira kwani zitakuwepo shughuli mbalimbali wakati wa uvunaji samaki katika vizimba.
Anaeleza kuwa, yeye kama mwanamke anajua mpango wa serikali wa ufugaji samaki kwa njia ya vizimba utaleta mafanikio makubwa na kuongeza uchumi wa wafugaji samaki na wananchi wa kawaida na taifa kwa ujumla.
Afisa uvuvi mkoa wa Kagera Eflazi Mukama anasema serikali imetoa mkopo kwa wafugaji wa samaki kwa njia ya vizimba na mikopo hiyo inatolewa kwa wale wananchi waliojitokeza kutuma maombi Wizara ya mifugo na uvuvi kupitia katika halmashauri za wilaya zao.
" Mikakati hiyo ilianzishwa na Wizara kwa lengo la kuwawezesha wananchi wanaoishi maeneo ya ukanda wa ziwa pamoja na bahari kuwa na kipato mbadala na shughuli nyingine za kujiingizia kipato kupitia mazao ya samaki na kuongeza rasilimali ya uvuvi" anasemaEflazi
Anataja vigezo mbalimbali vya kuomba mkopo kuwa ni pamoja na barua za maombi, andiko la mpango biashara, na nyaraka zingine kama akaunti ya benki, kama ni kikundi cheti cha usajiri, muhtasari wa wanachama ambao wameridhia kupata mkopo, benk statiment na kitambulisho cha mwenyeki wa kijiji au mtaa kilipo kikundi.
"Afisa uvuvi wa eneo husika baada ya kupitia hizo nyaraka anajaza fomu ya kuwapitisha kwa kukagua nyaraka zote kuwa zimekamilika na maombi yanatumwa Wizarani.
" Wizara inashirikiana na benki ya maendeleo ya kilimo (TADB) ambayo ina wataalamu wanaopitia maandiko ya maombi pamoja na kutoa matokeo ya watu waliofikia vigezo" anasema Eflazi.
Eflazi anaeleza kuwa kwa kipindi cha nyuma kuna sheria na vikwazo vilivyokuwa vimewekwa vya athari ya mazingira ambavyo ili mwananchi afuge kwa njia ya vizimba ilimulazimu atumie gharama zaidi ya Tsh Milioni 10, kufanya tathimini ya athari ya mazingira.
"Pia kufanya utafiti wa eneo la ufugaji, kibali cha matumizi ya maji kutoka mamlaka ya bonde ziwa Victoria ikiwemo gharama za kuwaleta wataalamu lakini kwa sasa gharama hizo zinagharamiwa na serikali.
"Kugharamia kwa serikali ni kuwawezesha wataalamu kuweza kupima maeneo husika, katika maeneo 15 yaliyopimwa mkoa wa Kagera. Maeneo yaliyobainika yanafaa kwa ufugaji wa njia ya vizimba ni maeneo 12 yalipitishwa na wizara ya mifugo na uvuvi kupitia taasisi ya TAFIRI na ofisi ya makamu wa Rais mazingira (NEMC) kwa kutoa vibali" anasema Eflazi.
Anayataja maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba kuwa, kwa wilaya ya Muleba kuna maeneo tisa, halmashauri ya Bukoba maeneo mawili ya Rubafu na Kemondo na wilaya ya Misenyi eneo moja la Kashenyi.
Anasema katika manispaa ya Bukoba maeneo mawili yalifanyiwa vipimo upande wa Nyamkazi kuelekea kisiwa cha Msira lakini lilibainika halina sifa kutokana na eneo hilo kuwa njia za vyombo vya usafiri
Ukanda huo pia ulibainika kuwa na upepo mkali ambao mawimbi yake ni makubwa yana uwezo wa kuathiri vizimba.
Eneo jingine lililopimwa ni Makongo ambalo lilionekana lina mwamba pamoja na upepo na mawimbi yake ni makubwa.
"Mkoa wa Kagera yalipatikana maeneo 12 ambayo ni maeneo makubwa hayawezi kujaa vizimba ambavyo vingine vina ukubwa wa mita 256 au mita 142 vya mduara au vya pembe nne.
"Toka mwaka jana wananchi 36 walijitokeza kuomba kujengewa vizimba na hadi sasa vimejengwa vizimba 11 na vingine vinaendelea kujengwa na mkandarasi aliyepewa tenda hiyo.
Anasema waombaji wa vizimba kutoka manispaa ya Bukoba wamejengewa vizimba sita kikundi kimoja kimepata vizimba vitano, mtu binafsi kizimba kimoja, halmashauri ya Bukoba vizimba 18, wilaya ya Muleba kuna vikundi vitatu na mtu binafsi mmoja watapata vizimba 12.
" Kila kizimba chenye ukubwa wa mita 256 kina uwezo wa kubeba vifaranga 17,920 vyenye gramu tano hadi 10 ni vifaranga vidogo ambavyo vinahimili uwezo wa kusafirishwa kutoka sehemu moja hadi nyingine.
"Vizimba 36 ambavyo tutavipokea tutapandikiza idadi ya vifaranga 645,720 na kwa kuwa vizimba hivyo ni mikopo iliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan mikopo hiyo ina thamani ya shilingi Bilioni 3.7 " anaeleza Eflazi.
Anaongea " Muda wa uvunaji samaki hao itakuwa ni miezi sita hadi saba na samaki atakuwa na nusu kilo au gramu 500, maji anayoishi yanapaswa kuwa masafi kwani yakiwa machafu yanaathiri ukuaji wake.
Eflazi anataja lengo la mpango huo kuwa ni kuongeza rasilimali ya samaki na kuongeza kipato kwa wananchi kwani maeneo yanayopakana na maji yanaendelea kutokana na samaki kwa hiyo lazima wabuni mbinu ya kuongeza samaki pamoja na uchumi kwa wananchi.
Anasema bei ya samaki kwa sasa imeongezeka kwani nchi mbalimbali za Jumuia ya ulaya na Uarabuni zimekuwa zikifanya biashara hii na kwa sasa kilo moja ya samaki inaanzia sh 6,000 na kuendelea hii inamsadia mvuvi anavuna kidogo anapata faida kubwa tofauti na kipindi cha nyuma alikuwa anavuna samaki wengi anapata faida ndogo.
Kuongezeka kwa bei ya samaki ni kutokana na ubora wake na nchi nyingi zimegundua kwamba samaki wa Tanzania ni bora, wazuri wana radha nzuri na kiafya wanasaidia na ndiyo maana wanatoka kote huko wanakuja kununua Tanzania.
Anasema ufugaji huo wa samaki kwa njia ya vizimba utasaidia kuongeza ajira kwa wanawake na vijana na hata magari ya kubeba kwani wataweza kusaidia katika shughuli za kubeba na kuosha samaki kabla hawajapelekwa sokoni.
Eflazi anasema vifaranga 645,720 iwapo vitafikisha ukubwa wa nusu kilo vitakuwa na tani zaidi ya laki 1.2 sawa na kilo milioni 1.2 kwa kilo moja sh.6,000 kikundi kitakuwa bilioni 7.7 ni fedha ambazo zitazalishwa ndani ya miezi saba.
Anaishukuru serikali kwa kukubali mkoa wa Kagera kunufaika na mpango huo kwa kutoa mkopo kama njia ya kuwaongezea uchumi wananchi.
Anawaomba wananchi kuchangamkia fursa hiyo kwa maeneo 12 yaliyotengwa kama mtu ana mtaji wake binafsi ajitokeze ili aombe mkopo aongeze kipato na uchumi katika mzunguko wa samaki.
Meneja wa Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Kanda ya Ziwa, Kayombo Jerome anasema hakuna kizimba kinaweza kujengwa bila kufuata taratibu za kisheria kama kufanya tathimini ya athari ya mazingira na kama kuna athari yoyote wakati wa tathimini inakuwa imeishabainishwa na kutengenezewa mikakati ya kuipunguza au kuiondoa.
Jerome anasema wapo watu wanaojenga vizimba bila kufuata sheria hakuna tathimini inayokuwa imefanyika hivyo uwezekano wa kuwepo changamoto unakuwa mkubwa inaweza ikawa kwa mfugaji mwenyewe au katika mazingira.
"Unaweza kujenga kizimba kikazolewa na mawimbi au ukatengeneza kizimba na kukiweka katika mazingira ya samaki hapo unakuwa umeathiri ikorojia ya eneo hilo lakini vizimba vilivyofuata utaratibu wa kisheria changamoto zinakuwa kidogo" anasema Jerome.
Kwa mujibu wa mwongozo wa ufugaji wa samaki kwenye vizimba kutoka Wizara ya mifugo na uvuvi unatoa maelekezo mahsusi yatakayomwezesha mfugaji wa samaki kwa kutumia vizimba kupata mazao bora na yenye tija.
Mwongozo huo unaelekeza mambo ya kuzingatia wakati wa kuchagua eneo la kufugia samaki kwa kutumia vizimba.
Pia ufugaji huo unapaswa kufanyika kwa uangalifu ili kuepuka uchafuzi wa mazingira na migogoro kati ya watumiaji wengine wa maji.
Aidha eneo lisiwe na mwingiliano na watumiaji wengine wa maji, eneo husika liwe na kina cha maji kuanzia mita tano na kuendelea.
Anasema vizimba viache kina cha mita mbili kati yake na sakafu, eneo lisiwe na mawimbi makali, eneo liwe linafikika kiurahisi ili kupeleka na kutoa mahitaji ya uzalishaji.
Hata hivyo, mpango wa serikali wa ufugaji samaki kwa njia ya vizimba utaleta mafanikio makubwa na kuongeza uchumi wa wafugaji samaki, mwananchi mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
Post a Comment