TRA YATOA ELIMU KWA WAANDISHI WA HABARI KAGERA UMUHIMU WA KUTOA , KUDAI RISITI

>> Yawasisitiza Waandishi wa habari kuwaelimisha wananchi umuhimu wa kutoa na kudai Risiti
Alodia Dominick, Bukoba
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) nchini imewasisitiza wananchi wanaponunua bidhaa yoyote kudai risiti na wanapouza kutoa risit kwa kufanya hivyo pande zote zitakuwa zimechangia ulipaji kodi inayosaidia katika ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo hapa nchini.
Afisa uhusiano mkuu kutoka mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) Hudson Kamoga ameyasema hayo Oktoba 19, 2024 wakati akizumgumza na waandishi wa habari katika mafunzo yaliyoandaliwa na mamlaka hiyo.
Afisa uhusiano mkuu kutoka mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) Hudson Kamoga aliyesimama akizungumza na Waandishi wa habari mkoani Kagera.
Kamoga amesema waandishi wa habari ni sehemu ya kuchochea maendeleo ya nchi yao na wanao wajibu wa kuelimisha jamii juu ya faida zinazopatikana kutokana na ulipaji kodi kwani asilimia 70 ya mapato ya serikali inatokana na kodi huku asilimia inayosalia ikitokana na wahisani mbalimbali.
"Unaponunua bidhaa ukadai risiti unatimiza wajibu wako, risiti ni ulinzi kwa bidhaa uliyoinunua unaweza kununua bidhaa ikiwa na changamoto usipokuwa na risiti huwezi kurudishiwa bidhaa hiyo.
Inapotokea ulinunua simu bila risiti ikatokea kuna mtu mwingine aliibiwa simu inayofanana na ya kwako mtu akasema hii ni simu yangu unajiteteaje kwamba hiyo simu ni ya kwako na siyo ya mtu yule anayedai" amesema Kamoga.
Kamoga ameongeza kuwa mtu anaponunua bidhaa akadai risiti uanaisaidia serikali kukusanya mapato yake na kuwa yule aliyemuuzia bidhaa kama hajampa risiti anakuwa amemsaidia kukwepa kulipa kodi hivyo wananchi waone umuhimu wa kudai risiti ili kuisaidia serikali kusonga mbele.
"Unaweza kununua kitu dukani bila kudai risiti alafu ukafika nje wakasema kuna kibaka ameiba kama huna risiti wewe ukikamatwa kama mwizi hautaweza kujitetea, wananchi waone kudai risiti ni wajibu wa kisheria lakini ni wajibu wao wa kizalendo kwa nchi yao na ni ulinzi wa bidhaa anayoinunua" ameeleza Kamoga
Meneja msaidizi huduma kwa mlipa kodi mkoa wa Kagera Estomih Mossi ameeleza kwamba elimu ya kodi imekuwa endelevu na walipa kodi inabidi waipate kutoka kwa waandishi wa habari kupitia vyombo vyao vya habari kwani wao ni kiunganishi kwa TRA na wananchi.
Meneja msaidizi huduma kwa mlipa kodi mkoa wa Kagera Estomih Mossi akifungua mafunzo kwa waandishi wa habari na mamlaka hiyo.
Amesema mamlaka hiyo kwa mwaka 2023/2024 walikusanya mapato zaidi ya Tsh. Trioni 28 na mwaka 2024/2025 wanapaswa kukusanya Tsh. Trioni 30.4
Akitoa mada ya elimu kwa waandishi wa habari afisa elimu na mahusiano TRA Kagera Rwekaza Rwegoshora amesisitiza utunzaji wa kumbukumbu kwa wafanyabiashara kwani itawaondolea kulipa kodi kubwa tofauti na mitaji yao ikiwemo kupata adhabu ya faini au kifungo.
Afisa elimu na mahusiano TRA Kagera Rwekaza Rwegoshora akitoa mada ya elimu kwa waandishi wa habari.
Pia amesisitiza kila mwananchi mwenye miaka 18 na kuendelea kuwa na namba ya utambulisho ya mlipa kodi (TIN namba) awe anafanya biashara au hafanyi na kuwa sheria hiyo ilifanyiwa maboresho mwaka 2023 ya mtanzania yeyote kuanzia umri huo anapaswa kuwa na namba ya TIN
kwani itamsaidia kupata huduma mbalimbali.
Alitolea mfano mtu anaponunua chombo cha moto kutumia namba hiyo ya utambulisho kupata leseni ya udreva au anaponunua chombo cha moto kutoka nje ya nchi ili ukifanyie usajili lazima awe na namba ya utambulisho ya mlipa kodi (TIN).
Ashura Jumapili mwandishi wa habari gazeti la majira ameshauri mamlaka hiyo kufuatilia hata wafanyabiashara waliopo nje ya mji ili nao waweze kulipa kodi kwani baadhi ya wafanyabiashara hao wanabiashara kubwa hadi bidhaa zingine wanatunza stoo lakini hawalipi kodi.
Baadhi ya waandishi wa habari mkoani Kagera waliohudhuria mafunzo yaliyotolewa na mamlaka ya mapato Tanzania TRA
Ikumbukwe kuwa, TRA Kagera imekuwa ikikaa mara kwa mara na waandishi wa habari kwa lengo la kuwapa elimu ili nao wakaelimishe jamii inayowazunguka juu ya umuhimu wa kulipa kodi kwa maendeleo ya nchi hii.
Post a Comment