TARURA ILEMELA ILIVYOWAKOSHA WANANCHI BAADA YA KUKARABATI BARABARA YA IGOMBE- KAHAMA
>>Ni ile
iliyokuwa mbovu kuwalazimu wananchi kusafirisha majeneza yenye miili mabegani
>>Sasa Gari, Pikipiki,Bajaji,Toroli,
Mkokoteni yapita barabarani bila shida
>>Wananchi
waipongeza Serikali kusikiliza kilio chao
>> Hivi karibuni, DIMA ONLINE iliripoti ubovu wa barabara ya Igombe –Kahama unavyowatesa wananchi ikiwemo kulazimika kusafirisha majeneza yenye miili mabegani
Na Dinna Maningo, Mwanza
MAISHA ya Binadamu
yanahitaji furaha, pale inapotokea changamoto kadha wa kadha huondoa matumaini
ya furaha,amani na kubaki katika huzuni kutokana na kero zinazomsibu au
kumsumbua anapokwama kutimiza kile alichodhamilia, na wakati mwingine lawama
zote huitupia Serikali akiamini imeshindwa kutatua changamoto.
Wananchi
wanapotoa kero mbalimbali katika mazingira wanayoyaishi matamanio yao ni kuona
Serikali inawajibika kuzitatua. Serikali inapochukua hatua basi mwananchi huyo
hupata furaha na kuwa rafiki wa Serikali ama taasisi ya serikali pale
inapowajibika kutatua shida zinazowakabili zinazowapa mateso baada ya
kuziwasilisha katika mamlaka husika.
Wananchi wanaotumia Barabara ya Igombe – Kahama iliyopo ndani ya wilaya ya Ilemela mkoa wa Mwanza wamejawa na furaha baada ya changamoto iliyokuwa kero na mateso ya ubovu wa barabara yenye makorongo kukarabatiwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mjini (TARURA) wilaya ya Ilemela mkoa wa Mwanza.
Barabara iliyokarabatiwa hivi karibuni, baadhi ya pembezoni mwa barabara kuna mitaro iliyowekwa kipindi cha nyuma kabla ya ukarabati wa sasa wa barabara hiyo ya Igombe -KahamaMwenyekiti
wa Mtaa wa Bujingwa, Kata ya Bugogwa Shija Habari, anaipongeza TARURA kutatua
kero ya barabara hiyo na kusema kuwa TARURA ni wasikivu kwani baada ya kutoa
kilio chao kupitia chombo cha habari cha mtandoni cha DIMA Online imeweza kutatua kero ya barabara iliyokuwa ikiwatesa.
Anasema baada ya barabara kukarabatiwa wananchi wakiwemo wakulima na wavuvi wanapita bila karaha wakati wanaposafirisha bidhaa zao kwa kutumia usafiri wa Pikipiki, Gari, Bajaji, Baiskeri, Toroli na mkokoteni.
‘’Tunaishukuru
sana TARURA kusikiliza kilio chetu wametutengenezea barabara ambayo ilikuwa
inawapa kero wananchi wanaotembea kwa miguuu na watumiaji wa vyombo vya moto,
baiskeri, na mkokoteni.
‘’Sasa hivi
msiba ukitokea mwili wa marehemu unasafirishwa kwa gari au bajaji tofauti na
awali wakati haijakarabatiwa wananchi walilazimika kubeba jeneza lenye mwili
mabegani kutoka Kituo cha Afya Karume
mwendo wa km 3 kufika Bujingwa.
Mwenyekiti
huyo anaongeza kusema ‘’ Kwa sasa gari , pikipiki zinapita bila shida katika barabara
ya Igombe- Kahama Kwenda Busweru iliko makao makuu ya wilaya ya Ilemela pamoja
na Halmashauri ya manispaa ya Ilemea na maeneo mengineyo ‘’ anasema Shija.
Aiomba TARURA kuweka Mitaro na Karavati
Mwenyekiti huyo anasema pamoja na kuipongeza TARURA kwa kusikiliza kilio chao cha ubovu wa barabara na hivyo kuweza kuikarabati bado mitaro na karavati haijawekwa kwenye maeneo korofi ya barabara .
Mwenyekiti wa mtaa wa Bujingwa Shija Habari, akionesha eneo la barabara ya Igombe- Kahama kabla ya ukarabati, sehemu hiyo hadi sasa imekarabatiwa ila haijawekewa kalavati. Wakati wa mvua maji hujaa na kufunika barabara na kusababisha adha kwa wapitaji na wanafunzi kushindwa kuvuka kwenda shuleni.'' Changamoto katika barabara hiyo ilikuwa ni ubovu, ukosefu wa mitaro, karavati baadhi ya maeneo korofi. Tunaomba TARURA ijenge mitaro na karavati ili barabara iwe imara, wasipoweka msimu wa mvua barabara hiyo itaharibika na kurudi katika hali yake ya awali na kutusumbua.
'' Kuna
baadhi ya maeneo katika barabara hiyo panahitaji karavati, mvua ikinyesha
wananchi,wanafunzi, wanavuka barabara kwa shida kwasababu maji yanajaa na
kusababisha wakati mwingine wanafunzi kushindwa kupita kwenda shuleni wanakaa
utoro au wanasubiri kwa saa kadhaa maji yapungue ndio wavuke kwenda shuleni’’
anasema Shija.
Shabani Nkungu ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM ) Tawi la Bujingwa anaipongeza Serikali kupitia TARURA kukarabati barabara na kusema kuwa ubovu wa barabara uliwatesa kisiasa na kuipa hofu CCM.
'' Naishukuru
Serikali inayoongzwa na CCM kwa usikivu tulilalamika na imesikiliza kilio chetu
na kukarabati barabara ambayo ilitutesa kisiasa, tulipigwa madongo na wananchi
wakiwemo wapinzani wakisema kuwa CCM imeshindwa kusimamia serikali ikarabati
barabara.
'' Sasa tunachoomba
TARURA ikamilishe zile kasoro zilizosalia iweke mitaro na karavati kwenye
maeneo korofi ya barabara hiyo ili barabara iendelee kuwa imara. Inaleta faraja
pale wananchi wakitoa kero zao na Serikali ikawajibika na kuzitatua''anasema.
Neema Joseph
anasema kukarabatiwa kwa barabara kumerahisisha usafiri ''Baada ya barabara
kukarabatiwa sasa hivi tunatumia nauli Tsh. 1000 kutoka Igombe senta hadi
Bujingwa.
'' Wakati barabara haijatengenezwa ili ufike Bunjingwa ulilazimika kulipa Tsh. 3,000 na ukiwa na mgonjwa nyakati za usiku nauli ni zaidi ya Tsh.10,000 kwenda kituo cha afya Karume'' anasema Neema.
Mkazi wa
mtaa wa Kilabela Kata ya Bugogwa, Lucy Samsoni anaipongeza TARURA kwa
kukarabati barabara na kusema kuwa imewapunguzia mwendo na gharama kuzunguka
sabasaba wanapokwenda wilayani.

''Baada ya barabara kukarabatiwa hatusumbuki tena kuzunguka sabasaba kwenda wilayani, tunapita hii hii barabara ya Igombe- Kahama muda mfupi umeshafika wilayani kwa usafiri wa pikipi au bajaji kwa ghama ndogo ya Tsh. 1000 hadi 2000.
'' Wakati
barabara haijakarabatiwa wakazi wa kata ya Bugogwa ili uende wilayani ulilazimika
kupanda gari nauli Tsh. 1000 ushukie sabasaba ulipe tena nauli gari za kwenda
Busweru wilayani Tsh. 600 jumla kwenda na kurudi ni Tsh. 3200, unatumia muda
mwingi kwenda wilayani '' anasema Lucy Samson.
David Shija
Mwendesha pikipiki anasema baada ya barabara kukarabatiwa imewapunguzia kero
wanaposafirisha abiria kwani walipofika maeneo korofi abiria alilazimika
kushuka kutembea kwa miguu hadi watakapofika eneo lisilo korofi.
'' Kwakweli
naishukuru Serikali kwa kukarabati barabara imetusaidia sana maana tulikuwa
tukifika kwenye makorongo inabidi abiria ashuke atembee kwa miguu hadi sehemu
ambayo barabara ina unafuu ndiyo apande tuendelee na safari.
''Kitendo
hicho kiliwakera sana abiria maana katumia nauli yake alafu unamshusha atembee
kwa miguu kisa tu ubovu wa barabara. Hali hiyo ilisababisha madereva wa
pikipiki au bajaji kupandisha nauli kwa bei atakayojisikia’’ anasema David.
Mwendesha pikipiki huyo anasema kuwa bado kuna changamoto ya ukosefu wa karavati na mitaro na kwamba fedha zilizotengwa na TARURA kukarabati,kujenga mitaro na karavati ni ndogo kutokana na hali ya ubovu wa barabara hiyo hasa msimu wa mvua barabara uharibika sana na kuwa kero.
Muonekano wa barabara ya Igombe -Kahama kabla haijakarabatiwa'' TARURA ituwekee mitaro hii inasaidia mvua ikinyesha maji hayapiti juu ya barabara na haiharibiki mapema. Waweke na karavati maaana mvua ikinyesha nyingi maji yanajaa barabara inafunikwa na maji tunashindwa kusafirisha abiria pamoja na mizigo’’ anasema David.
Anaongeza
kusema '' Nilisoma habari ya ubovu wa barabara ya Igombe- Kahama kwenye chombo
hiki cha habari cha DIMA Online, Meneja
TARURA anasema kuwa wametenga fedha Tsh. Milioni 25 kukarabati barabara,
kuweka, karavati tano na mitaro mita 300 barabara yenye urefu wa km 9.2.
‘’Mimi si
mtaalamu wa mambo ya barabara lakini kwa kuona kwangu na mtumiaji wa barabara
hii kwa miaka mingi hicho kiasi ni kidogo sana kufanya mambo yote hayo. Kiasi
hicho naona ni cha ukarabati wa barabara tu.
'' Hakitoshi
kuweka mitaro na karavati ndio maana unaona hiii barabara imekarabatiwa
haijawekwa mitaro na karavati. Ni vema Serikali iongeze fedha ili ifanye kazi
kwa uhakika barabara iwe imara’’ anasema David.
Barabara ijengwe kwa
kiwango cha Lami
Mwenyekiti wa
CCM Tawi la Bugogwa Shabani Nkugu anasema ili kuepusha gharama za mara kwa mara
za ukarabati wa barabara ya Igombe – Kahama kuna haja ya Serikali kujenga barabara
hiyo kwa kiwango cha lami kwakuwa ni barabara muhimu inayokwenda hadi wilayani
na Halmashauri.
Anasema kuwa
barabara hiyo ikijengwa kwa kiwango cha lami itakuza uchumi wa mwananchi na
serikali na itawaepushia gharama na muda wananchi wanaolazimika kupita barabara
ya Igombe- mjini inayopita sabasaba wanapokwenda wilaya ya IIlemela na
Halmashauri.
'' Hii
barabara ikijengwa kwa kiwango cha lami itaharakisha maendeleo watu watajenga,
magari mengi yatapita mazao yatasafirishwa bila shida, wavuvi wataneemeka maana
wanapata shida kusafirisha samaki pindi barabara inapokuwa mbovu '' anasema
Mwenyekiti CCM.
Kauli ya Meneja TARURA
Awali
akizungumza na Mwandishi wa Habri wa DIMA
Online ofisi ya TARURA, Meneja Wakala wa Barabara za Vijijini na Mjini
(TARURA) wilaya ya Ilemela Mhandisi Sobe Makonyo kama ilivyoripotiwa katika
chombo hiki cha habari Agosti, 26,2024 alisema kuwa barabara hiyo itakarabatiwa
kwa kiwango cha changarawe, kujenga mitaro na karavati.

Akaongeza
kusema kuwa, Kazi kubwa zitakazofanyika ni kuikarabati ,kuweka karavati tano,
mitaro mita 300 hasa sehemu korofi ili ziendelee kupitika ‘’ anasema Sobe.
Kuhusu ombi
la wananchi la barabara kujengwa kwa kiwango cha lami, Sobe akasema kuwa ujenzi wa barabara
hiyo utagharimu zaidi ya Bilioni 5, hivyo pesa zikipatikana itajengwa kwa
kiwango cha lami.
Meneja
TARURA akaeleza manufaa ya barabara hiyo kwamba ikifanyiwa matengenezo itarahisisha
wanafunzi kwenda shuleni bila kupata adha , itavutia watu kuwekeza kandokando
ya Kahama na Igombe na itachochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
'' Kazi ipo katika hatua ya manunuzi itakapokamilika kazi ya matengenezo itaanza mara moja . Barabara hiyo ni muhimu itawarahisishia wavuvi wa Igombe kufikisha mazao yao sokoni maana makao makuu ya wilaya yapo Busweru hivyo itasaidia kupunguza gharama na muda kuzunguka Sabasaba.
Kata ya
Bugogwa ni miongoni mwa kata 19 ndani ya halamshauri ya Manispaa ya Ilemela,
mkoa wa Mwanza. Ina jumla ya mitaa 19, kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2022, kata hiyo ina jumla ya kaya 7,108
zenye jumla ya wakazi 38,698 kati yao wanawake ni 22,666 na wanaume ni 16,032.
Mwezi Agosti, 26, 2024 DIMA Online iliripoti Makala iliyokuwa
ikielezea namna barabara ya Igombe – Kahama inavyowapa mateso wananchi kutokana
na ubovu wa barabara. Kwa undani wa Makala hiyo tembelea chombo hiki cha habari
kupata undani wa Makala hiyo.
DIRA WIZARA YA UJENZI : Kuwa na miundombinu bora na endelevu
itakayochochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini.
Post a Comment