HEADER AD

HEADER AD

WATAMANI UBORA WA MAJENGO SHULE YA MSINGI KENYANGI UWE CHACHU KUINUA TAALUMA


>>Wananchi waupongeza Mgodi wa Barrick North Mara kutoa zabuni kwa Wakandarasi wazawa 

>>Watamani shule iwe na taaluma bora iendane na ubora wa majengo

Na Dinna Maningo, Tarime

MARA nyingi unapozitazama shule za msingi zilizopo vijijini na mjini utagundua baadhi ya shule majengo yamechakaa huku ukarabati au ujenzi wa shule kwa kiwango cha ubora na ya kisasa ukiwa ni wa kusuasua au kutofanyika kabisa kwa miaka mingi tangu kujengwa kwa shule.

Hali hiyo huifanya shule kutokuwa kivutio kwa wanafunzi na walimu, wakati mwingine kuwa chanzo cha kushuka kwa taaluma kwa wanafunzi kutokana na mazingira yasiyo rafiki ya wanafunzi kujifunzia na walimu kufundishia kwasababu ya uchakavu wa madarasa huku mengine yakiwa hayana sakafu na samani za kutosha.

Shule ya msingi Kenyangi iliyopo Kitongoji cha Kegonga A, Kijiji cha Matongo, Kata ya Matongo –Nyamongo, ilianzishwa mwaka 2003, ilijengwa kwa nguvu za wananchi wa Kitongoji cha Kegonga A na Kegonga B.

        Baadhi ya madarasa shule ya zamani ya msingi Kenyangi 

Shule hiyo imetimiza miaka 21 tangu wanafunzi walipoanza kusoma, kwa sasa ina wanafunzi wapatao 776, kati ya hao Wavulana ni 405 na Wasichanani 371 ikiwa na walimu 09 kati yao wanawake ni wawili .

Ina madarasa 8, pungufu madarasa 9, ina nyumba za walimu 07 pungufu nyumba 15,mahitaji ya walimu ni 22,waliopo 9, ina upungufu wa walimu 13, ina ofisi 1, pungufu ofisi 2, stoo hakuna mahitaji ni stoo 1, ina vyoo vya wanafunzi matundu 28 pungufu matundu 4,vyoo vya walimu matundu 2 pungufu matundu 2.

Baadhi ya madarasa shule ya zamani ya msingi Kenyangi

Shule ina jumla ya madawati 280 pungufu 12, Kabati 2 pungufu 17, ina viti 10 vya walimu , pungufu 12, benchi hakuna mahitaji ni mabenchi 3, meza 10 pungufu 12.

Hata hivyo mwaka 2019 Mgodi wa Dhahabu wa North Mara unaomilikiwa na Kampuni ya uchimbaji wa dhahabu ya Barrick ulifanya uthamini kwa baadhi ya maeneo ya wananchi wa Kitongoji cha Kegonga A na Kegonga B ikiwemo na shule ya msingi Kenyangi ili kupisha shughuli za mgodi.

Inaelezwa kuwa mwaka 2020 Wananchi walilipwa fidia na kuhama eneo lililochukuliwa na mgodi ambapo shule hiyo ilifanyiwa uthamini wa Tsh.  Milioni 500 ili linunuliwe eneo lingine kujenga majengo mapya ambapo mgodi ulinunua eneo na kuanza ujenzi mwaka 2022.

Uongozi wa mgodi wa North Mara ukatoa zabuni kwa wakandarasi wazawa kujenga shule ambapo Kampuni ya PKM ilijenga madarasa , vyoo na nyumba za walimu. Kampuni  ya RIN ilijenga jengo la utawala, kampuni ya RES nyumba za walimu, viwanja viwili vyamichezo,sinki na kuweka tenk la maji . Kiasi cha Tsh. Milioni 500 hakikuweza kutosheleza na hivyo ujenzi kugharimu Tsh. Bilion 1.28.

       Majengo mapya ya madarasa shule ya msingi Kenyangi 

Mnamo Oktoba, 6,2024  Rais wa Barrick Dkt. Mark Bristow alifika shule mpya ya Kenyangi akiwa ameongozana na baadhi ya viongozi wa serikali akiwemo Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini Mwita Waitara, Diwani wa Kata ya Matongo, Godfrey Kegoye na viongozi wa mgodi wa North Mara Barrick ambapo aliikabidhi kwa uongozi wa Halmashauri ya wilaya ya Tarime.

       Rais wa Barrick Dkt. Mark Bristow akikata utepe wakati alipoitembelea shule ya msingi Kenyangi iliyojengwa na mgodi wa Barrick North Mara akiwa ameambatana na viongozi mbalimbali wa Serikali na Mgodi akiwemo Mbunge wa Jimbo la Tarime vijijini Mwita Waitara aliyevaa shati jeupe.

Meneja North Mara aeleza mafanikio

Tarehe 11, Oktoba, 2024, Meneja  Mkuu wa Mgodi wa Barrick North Mara, Apolinary Lyambiko akizungumza na Waandishi wa Habari waliofika kutembelea baadhi ya miradi iliyojengwa na mgodi huo ikiwemo shule ya msingi Kenyangi anaeleza mafanikio katika kuhakikisa inasaidia jamii katika maendeleo.

         Meneja  Mkuu wa Mgodi wa Barrick North Mara, Apolinary Lyambiko akizungumza na Waandishi wa habari

Anasema kupitia mpango wa uwajibikaji wa makampuni kwa jamii (CSR) wamekuwa wakitekeleza miradi mingi kwa jamii hususani katika vijiji 11 vinavyozunguka mgodi na wilaya kwa ujumla ambapo mwaka 2023 wameweza kutekeleza miradi takribani 115 iliyokamilika iliyogharimu Tsh. Bilioni 7.3.

‘’Shule ya msingi Kenyangi ujenzi wake umegharimu Tsh. Bilioni 1.28 ,tumejenga madarasa 12, ofisi 4, jengo la utawala, viwanja viwili vya michezo ,Samani za shule na ofisi , mfumo wa maji, vyoo matundu 24 ujenzi umegharimu fedha za kitanzania 1,287,000,000.

     Jengo la utawala shule ya msingi Kenyangi 

‘’ Bado tutajenga nyumba nne za walimu, banda la mifugo.chumba cha kompyuta na uzio wa shule. Pia tumetenga Tsh. Bilioni 9 kwa ajili ya miradi takribani 101 itakayofanyika katika halmashuri ya wilaya ya Tarime. Miradi yetu imejikita kwenye afya,elimu, maji na shughuli zingine za kijamii’’ anasema Apolinary.

Afisa Mahusiano mgodi wa Barrick North Mara, Francis Uhadi, anasema wametengeneza mpango wa miaka mitano wenye maono ya muda mrefu badala kuwa na miradi midogomidogo.

       Afisa Mahusiano mgodi wa Barrick North Mara, Francis Uhadi akizungumza na Waandishi wa habari

‘’Nawaomba Waandishi wa Habari mkihitaji taarifa zetu nipigie simu au fika ofisini tutakupa ushirikiano wa habari utakazozihitaji kupata ufafanuzi au kuzifahamu’’anasema Francis.

Walimu waomba ushirikiano na wazazi kuinua taaluma

Walimu katika shule hiyo wanawaomba wazazi kushirikiana kwa pamoja kuhakikisha wanafunzi wanahudhulia vipindi vyote darasani kwani baadhi ya watoto hukaa utoro na wazazi hawajali.

Mwalimu mkuu msaidizi wa Kenyangi , Paul Mapera anapongeza ujenzi wa shule na kwamba mahusiano mazuri kati ya mgodi na serikali ya kijiji yamefanikisha ujenzi wa shule bora huku akiomba mgodi uboreshe viwanja vya michezo kwa kuweka changarawe laini kwakuwa sehemu vilipojengwa kuna tope jingi.

      Uwanja wa michezo shule mpya ya Kenyangi 

Anasema walimu wanajitahidi kufundisha licha ya uchache wao na kwamba mwamko mdogo wa elimu unashusha taaluma huku akisisitiza wanafunzi kupenda masomo.

‘’ Darasa la awali lina wanafunzi 116, darasa la kwanza 123, inakuwa ni changamoto katika ufundishaji walimu ni wachache.  Mwamko mdogo wa elimu unashusha taaluma kwani baadhi ya watoto hutumikishwa shughuli za kilimo na kuchunga mifungo.

Mkuu wa shule ya msingi Kenyangi Khadija Sanga ameushukuru mgodi kujenga shule mpya yenye mazingira mazuri ya ufundishaji na kujifunzia tofauti na shule ya zamani ambayo ilikuwa sio rafiki kwa kujifunzia na kufundishia.

      Mkuu wa shule ya msingi Kenyangi Khadija Sanga akielezea ujenzi wa shule ya msingi Kenyangi.

‘’Shule ya zamani vyumba vya madarasa vilikuwa vichache saba, hakukuwa na ofisi ya usiri kwamba kila mwalimu ana ofisi yake au ofisi ya mwalimu mkuu. Walimu tulitumia ofisi moja, shule haikuwa na jengo la utawala.

‘’Kwa mazingira haya ya shule taaluma itapanda maana hata wanafunzi wanatamani kusoma kwenye shule mpya, itasababisha mahudhulio kuongezeka. Yamejengwa madarasa 12 yatawezesha kuwa na mikondo kwa madarasa yenye wanafunzi wengi tofauti na shule ya zamani walirundikana darasa moja ikatupa changamoto katika ufundshaji.

Ameongeza ‘’ Tumejengewa nyumba za walimu two in one zipo nne, vyoo vya walimu, kila darasa lina madawati 20, kuna viti, meza za walimu, viwanja vya michezo.

         Nyumba mpya za walimu shule ya msingi Kenyangi 

‘’Isipokuwa bado nyumba za walimu hazitoshelezi  ila mgodi ulisema utakamilisha nyumba zingine nne . Tuna upungufu wa walimu hasa walimu wa somo la Kingereza’’ anasema mkuu wa shule.

Wataka shule iwe na taaluma bora

Wazazi wa wanafunzi wanaosoma shule ya msingi Kenyangi wamewaomba walimu wa shule hiyo kujitahidi kufundisha wanafunzi ili wawe na ufahamu wa kutosha kwa kile walichoeleza kuwa baadhi ya wanafunzi wanafika darasa la tatu wakiwa hawajui kusoma wala kuandika.

’’Walimu wajitahidi kufundisha watoto ili wafanye vizuri, sio shule iwe na majengo mazuri huku wanafunzi wakishindwa kujua kusoma na kuandika. Itakuwa aibu sana kuwa na shule nzuri alafu tunakuwa na bora elimu’’anasema mzazi mmoja.

Wiliam Nyamhanga Makwahu anawasisitiza walimu kuwa na juhudi katika ufundishaji ili wanafunzi wafanye vizuri katika masomo yao kwani baadhi ya wazazi hawajui kusoma wala kuandika kwakuwa hawakusoma hivyo inakuwa vigumu kumwelekeza mtoto.

       Wiliam Nyamhanga Makwahu mkazi wa Kitongoji cha Kegonga B 

‘’Kuna siku mwanangu anayesoma darasa la tatu alikuja na mtihani nikamwambia nioneshe nikakuta amepata tano somo aliloniambia ni la maarifa. Mimi sijui kama mtoto anajua kusoma au kuandika maana mimi sikwenda shule sijui kusoma wala kuandika sasa mimi nitajuaje kufuatilia masomo yake wakati sijui kinachoendelea? Anauliza.

Anaongeza ‘’Mimi sikusomeshwa na wazazi wangu ndiyo maana nikaamua kuwapeleka watoto wangu shuleni ili wapate elimu wasiwe kama mimi hivyo nategemea walimu wawasadie wanangu ili wafanye vizuri’’ anasema Wiliam.

Amos Timotheo aliyehitimu elimu ya msingi katika shule hiyo mwaka 2023 anasema kuna utofauti wa majengo wakati alipokuwa akisoma na sasa ‘’ Majengo ya sasa ni mazuri sana, wakati nasoma wanafunzi walikuwa wanabanana darasani, madarasa yalikuwa na sakafu lakini haya yamewekwa vigae,madirisha ya vioo kwakweli hii shule imejengwa kwa kiwango cha kimataifa’’ anasema Amos.

Mwanafunzi wa darasa la pili katika shule hiyo Anna Yusuf, anasema anatamani wanafunzi waanze rasmi kusoma katika shule mpya waache kusoma kwenye majengo ya zamani.

     Mwanafunzi wa darasa la pili katika shule hiyo Anna Yusuf mkazi wa Kitongoji cha Kegonga B 

‘’Tunashukuru Mgodi kutujengea shule, natamani nikasome kwenye shule mpya maana bado tunasoma kwenye shule ya zamani, natamani kuhamia shule mpya ‘’ anasema Anna.

Mgodi ukamilishe ujenzi

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kegonga B Gachori Gachori amepongeza shule hiyo kujengwa na Mgodi kupitia kampuni za wazawa huku akiusisitiza mgodi kukamilisha nyumba za walimu zilizosalia kisha ikabidhi wananchi na siyo halmashauri kwakuwa shule hiyo kabla ya kuhamishwa ilijengwa kwa nguvu za wananchi.

      Vyooo vya walimu shule  ya Kenyangi 

‘’ Mgodi ulifanya uthamini wa shule ya msingi Kenyangi na baadhi ya wakazi ili kupisha maeneo kwa shughuli za mgodi. Wananchi walilipwa fedha wakaenda kutafuta maeneo mengine wakajenga. Shule ya Kenyangi ilifanyiwa uthamini Tsh. Milioni 500, viongozi na wananchi tukaona fedha hizo ni ndogo hazitatosha kununua uwanja na kujenga shule .

‘’ Sisi viongozi wa halmashauri ya kijiji na wananchi tukasema hatutaki hizo fedha mgodi uchukue ununue uwanja na ujenge shule ikishakamilika ikabidhi wananchi ’’ anasema Gachori.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kegonga A Matinde Matiko, anasema shule ya zamani ilikuwa kwenye kitongoji chake na baada ya kuhamishwa na mgodi ipo Kitongoji cha Kegonga B huku akiupongeza mgodi kwa ujenzi wa majengo yanayovutia.

          Madarasa shule ya msingi Kenyangi 

‘’Kiukweli mgodi umeboresha majengo yamekuwa ya kisasa tofauti na yale yaliyojengwa zamani na wananchi, niuombe mgodi ujitahidi kukamilisha majengo yaliyobaki watoto wetu wasome pazuri na serikali ituletee umeme hatuwezi kuwa na shule nzuri alafu haina umeme ‘’ anasema Matinde.

Waupongeza mgodi kutoa zabuni kwa wakandarasi wazawa

Mwenyekiti wa Kamati ya shule ya msingi Kenyangi Wangwe Werema ameupongeza mgodi huo kutoa zabuni za ujenzi wa shule kwa wakandarasi wazawa huku akiuomba uendelee kuwaamini wazawa na kuwapa zabuni kwakuwa wana uwezo wa kufanya kazi zenye ubora.

       Jengo la utawala shule ya msingi Kenyangi ambapo shule ya zamani ya Kenyangi haikuwa na jengo la utawala

‘’Shule hii imejengwa na kampuni za wazawa ya PKM, RIN,RES ambao wote ni wa hapahapa Nyamongo, na bahati nzuri na wewe mwandishi umeshuhudia majengo mazuri yaliyojengwa na watu wa hapa hapa kwetu wanaotoka ndani ya Kata ya Matongo. Tunaomba mgodi utujengee na shule ya Sekondari maana uwanja upo’’ anasema Wangwe.

Mgodi wakumbushwa kukamilisha ujenzi

Katibu Itikadi na Uenezi Chama cha Mapinduzi (CCM) Tawi la Matongo, Sadock Maningo ameushukuru mgodi huo kwa kujenga majengo ya kisasa huku akiusisitiza kukamilisha majengo yaliyosalia kama waivyokubalina na kijiji.

        Katibu Itikadi na Uenezi Chama cha Mapinduzi (CCM) Tawi la Matongo, Sadock Maningo.

‘’Shule ilijengwa na wananchi kwa kushirikiana na serikali. Nashukuru mgodi kujenga majengo mazuri maana jukumu hilo lingefanywa na watu wengine huwenda tusingepata majengo mazuri kama ulivyoyaona pengine fedha zingeishia mifukoni mwa watu wasio wema.

‘’Kwa kawaida mradi unatakiwa kukabidhiwa ukiwa umekamilika lakini mgodi umekabidhi halmashauri huku majengo mengine yakiwa hayajajengwa hivyo basi tunaomba waweze kukamilisha mradi kama walivyokubaliana na kijiji’’ anasema Sadock.

Pia amesisitiza kuwepo na walimu wa kutosha, taaluma bora’’ Tunataraji sasa kwakuwa kuna mazingira mazuri ya wanafunzi kusoma tuone matokeo mazuri, maana kisingizio ilikuwa wanafeli kwasababu ya mazingira mabaya ya kusomea sasa majengo ni mazuri. Matamanio yetu ni kuona shule inakuwa na kiwango kizuri cha taaluma’’anasema.

Hali ya Taaluma Kenyangi

Kwa mujibu wa Baraza la Mitihani la Tanzania inaonesha wanafunzi waliofanya mtihani wa kuhitimu elimu ya shule ya msingi mwaka 2019 katika shule ya msingi Kenyangi walikuwa 33. Waliopata daraja A-0, daraja B walikuwa 2, C-7, D-14,na E-0.

Wanafunzi waliofanya mtihani mwaka 2020 walikuwa 60. Waliopata daraja A -1, B-9,C-29, D-19 na E-2. Matokeo ya mwaka 2021 waliofanya mtihani walikuwa wanafunzi 60. Daraja A-0, Daraja B-9, c-37,D-19,E-0.

Mwaka 2022 waliofanya mtihani walikuwa 97, waliopata daraja A-3, B-16, C-44,D-34 na E-0. Waliofanya mtihani mwaka 2023 walikuwa 76 matokeo yanaonyesha waliopata daraja A-1, B-9,C-37,D-29,E-0.

Mgodi wa Dhahabu wa North Mara unaendeshwa na kampuni ya uchimbaji wa dhahabu Barrick iliyowekeza nchini Tanzania katika shughuli za uchimbaji wa dhahabu ambapo mwaka 2019 iliingia ubia na serikali ya nchi hiyo kupitia Kampuni ya Twiga Minerals yenye hisa 16.




        Majengo mapya ya shule ya msingi Kenyangi



             Nyumba za walimu

               Vyoo vya walimu
                         Stoo


                     Vyoo vya wanafunzi 


          Uwanja  wa michezo wa shule mpya




         Madarasa shule ya zamani ya msingi Kenyangi 




        Nyumba za walimu shule ya zamani ya msingi Kenyangi 

          Choo cha walimu shule ya zamani Kenyangi 


       Vyoo vya wanafunzi shule ya zamani 


             Uwanja wa michezo shule ya zamani Kenyangi 


No comments