WANACHAMA CCM TAWI LA MTURU WAJITOKEZA KUWANIA UANYEKITI WA MITAA
>>Mwenyekiti mtaa wa Rebu Senta hana mpinzani
>> 29 Wajitokeza nafasi ya ujumbe
Na Dinna Maningo, Tarime
WANACHAMA wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Tawi la Mturu, Kata ya Turwa, wilaya ya Tarime, mkoani Mara, wamejitokeza kuchukua fomu na kurejesha wakitiania kuwania nafasi ya uenyekiti wa mitaa kura za maoni kwa ajili ya kugombea uchaguzi Serikali za Mitaa.
Katika mtaa wa Rebu Senta aliyekuwa Mwenyekiti wa mtaa huo, Imani Samweli ndiye mtia nia pekee anayetetea nafasi hiyo ambapo wanachama wa Tawi hilo leo Oktoba, 23, 2024 wanapiga kura za maoni kwa watiania hao nafasi ya uenyeviti na ujumbe wa kamati ya mtaa utakaofanyika katika ofisi za Tawi hilo.
Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Tawi la Mturu, Mkapa Boniface akipokea fomu ya Mtiania nafasi ya uenyekiti wa mtaa wa Rebu Senta, Imani Samweli ambaye ni Mwenyekiti wa mtaa huo baada ya kurejesha ofisini.
Akizungumza na DIMA ONLINE Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Tawi la Mturu, Mkapa Boniface amewataja waliotiania nafasi ya uenyekiti wa mitaa ambao ni Imani Samweli mtia nia pekee mtaa wa Rebu Senta.
Wengine ni Samson Nyamurunga na Mackra Marwa wanatia nia uenyekiti mtaa wa Rebu Shuleni, Samweli Kibasa na John Gairigi mtaa wa Buguti huku wanachama 29 wanatiania nafasi ya ujumbe.
"Tawi la Mturu lina mitaa mitatu ambayo ni mtaa wa Rebu Senta, Rebu Shuleni na Buguti. Zoezi la kuchukua fomu na kurejesha lilianza tarehe 21, 10, 2024 na kuhitimishwa Oktoba, 22, mwaka huu.
"Jumla ya waliochukua fomu na kurejesha nafasi ya uenyekiti na ujumbe ni 34 ambapo idadi imeongezeka ikilinganishwa na 2019 walikuwa 20" amesema Mkapa.
Ameongeza kuwa zoezi la upigaji kura za maoni limeanza leo saa mbili asubuhi na litahitimishwa saa kumi jioni na kwamba watakaoruhusiwa kupiga kura ni wale wenye kadi za kielektoniki.
"Watakaopiga kura ni wale wenye kadi za kimfumo tu. Baada ya kupiga kura matokeo yatatangazwa na msimamizi kwenye mkutano mkuu wa Tawi, washindi watatangazwa.
" Upande wa wenyeviti majina yao yatapelekwa CCM wilaya ambao wao ndio watatuletea wagombea watakaokwenda kushindana na wapinzani katika uchaguzi utakaofanyika Novemba, 27, 2024" amesema Mkapa.
Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Turwa Marwa Timoro, amesema jumla ya watiania 108 katika Kata hiyo wamejitokeza kuwania nafasi ya uenyekiti wa mitaa na ujumbe.
Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Turwa, Marwa Timoro
" Zoezi limeenda vizuri kwa amani sasa kinachoendelea ni zoezi la upigaji kura za maoni. Nawaomba wanachama wapige kura kwa amani ili tuwapate wanachama watakaoipeperusha bendera ya CCM katika uchaguzi wa serikali za mitaa " amesema Marwa.
Chama cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Turwa kina Matawi matatu ya Chama hicho ambayo ni Tawi la Mturu, Rebu na Uwanja wa Ndege yenye jumla ya mitaa 8 ambayo ni mtaa wa Rebu Shuleni, Rebu Senta, Mkuyuni, Uwanja wa Ndege, Buguti , Gimenya, Kokehogoma na Kebikiri.
Kwa mujibu wa Tangazo la ratiba ya uchaguzi wa serikali za mitaa iliyotolewa Agosti, 15, 2024 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mohamed Mchengerwa, kampeni zitaanza Novemba, 20-26,2024 na uchaguzi utafanyka Novemba, 27,2024.
Post a Comment