HEADER AD

HEADER AD

WATUHUMIWA 9 WA MAUAJI YA MTOTO MWENYE ULEMAVU WA NGOZI WAFIKISHWA MAHAKAMANI

Na Alodia Dominick, Bukoba

WATUHUMIWA tisa wanaotuhumiwa kuhusika na mauaji ya kikatili ya mtoto mwenye ualbino Noela Asimwe Novat wa umri wa miaka miwili na nusu wamefikishwa katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Bukoba.

Mtoto huyo alikuwa mkazi wa kijiji cha Bulamula, kata ya Kamachumu Wilaya ya Muleba mkoani Kagera ambapo watuhumiwa wamefikishwa Mahakama kuu kusomewa shtaka linalowakabili na maelezo ya awali ya kesi hiyo kabla haijaanza kusikilizwa.

Washtakiwa hao akiwemo Padri Elpidius Rwegoshora (51) wamefikishwa mahakamani hapo Oktoba, 25,2024 na kusomewa shitaka linalowakabili.

Watuhumiwa wa mauaji ya mtoto mwenye ualbino Noela Asimwe Novat aliyekuwa na umri wa miaka  miwili na nusu mkazi wa kijiji cha Bulamula kata ya Kamachumu wilaya ya Muleba mkoani Kagera

Washtakiwa wengine waliofikishwa mahakamani ni pamoja na Novat Venant (24) baba mzazi wa marehemu Asimwe Novat ambaye ni dereva bodaboda, Nurdin Masoud (25), Ramadhani Selestine (23)  Alphonce Rwenyagila (30) pamoja na  Faswiu Athuman (39), Gozibert Alkard (35), Desdery Evarist (33), na Dastan Burchard (47).

Washtakiwa hao kwa pamoja wamefikishwa mbele ya Jaji mkuu wa mahakama hiyo, Emanuel Ngingwana aliyekubaliana na maombi yaliyowasilishwa na upande wa jopo la mawakili wa utetezi wa mtuhumiwa namba moja padre Elipidius Rwegoshora kutomsomea mashtaka mshtakiwa yanayomkabili hadi atakapofanyiwa uchunguzi wa ugonjwa wa akili.

Jopo la mawakili wanne wa upande wa utetezi likiongozwa wakili msomi Projestus Mulokozi awali liliiomba mahakama isitishe zoezi hilo kwa kuwa mteja wao kwa sasa hana uwezo wa kuongea vizuri pamoja na kuelewa anachokifanya kwa maana hiyo hawezi kujitetea kwa usahihi  hivyo wakaomba kupokelewa kwa  maombi ya upande wa utetezi yaliyotolewa.

Aidha mawakili wa Jamhuri wakiongozwa na wakili wa Serikali mwandamizi, Waziri Magumbo anayeshirikiana na mawakili wengine wa serikali ambao ni pamoja na Erick Mabagala na Matilda Assey hawakuweka pingamizi la aina yoyote walikubaliana na uamuzi uliotolewa na mahakama wa kusitisha zoezi.


Jaji Ngigwana ameamua mtuhumiwa apelekwe Isanga akapimwe akili hivyo,ameeleza kuwa watuhumiwa wote watasomewa mashtaka ya kesi inayowakabili kwa pamoja baada ya kupatikana matokeo ya uchunguzi wa ugonjwa wa akili wa mtuhumiwa namba moja padre Elipidius Rwegoshora ambapo kesi hiyo itatajwa tena Desemba 11,mwaka huu.

Washitakiwa hao wanadaiwa kutenda kosa hilo Mei, 30 mwaka huu katika kijiji cha Bulamula kata ya Kamachumu Wilayani Muleba.




No comments