WAZEE MKOANI KAGERA WATAJA CHANGAMOTO SABA AMBAZO SERIKALI INATAKIWA KUZITATUA
Na Alodia Dominick, Bukoba
BARAZA la wazee mkoa wa Kagera limetoa ombi kwa serikali kutatua changamoto saba zinazowakabili wazee ikiwemo kutungwa sheria ya wazee na kupitishwa na bunge kutokana na sera ya wazee ya mwaka 2003.
Maombi mengine ni pamoja na kuboresha huduma za afya kwa wazee, ombi la wazee kupewa malipo ya uzeeni yaani pensheni kama ilivyo kwa nchi ya Zanzibar, ushirikishwaji wa wazee katika vyombo vya maamuzi hususan katika mabaraza ya vijiji, kata na wilaya.
Pia wazee kuingizwa katika mikopo ya halmashauri ya asilimia 10 ya mapato ya ndani, kukemea na kutokomeza vitendo vya mauji ya kikatili dhidi ya wazee na mali zao, wazee wapewe vitambulisho vya matibabu vya taifa kuliko kwa sasa ambapo wana vitambulisho vya ngazi ya wilaya.
Maombi hayo yametolewa na mwenyekiti wa baraza la wazee Clement Nsherenguzi Oktoba 26, mwaka huu katika maadhimisho ya siku ya wazee duniani yaliyofanyika kimkoa katika kituo cha wazee Kilima kilichopo halmashauri ya Bukoba.
"Maadhimisho hayo yalipaswa kufanyika kimkoa Oktoba mosi, mwaka huu tukahairisha kutokana na shughuli nyeti ya ujio wa mbio za mwenge wa uhuru uliokuwa ukikimbizwa mkoani hapa ingawa kila wilaya iliweza kuadhimisha" amesema Nsherenguzi.
Nsherenguzi ameongeza, kuwepo kwa maadhimisho hayo ni matokeo ya serikali kutambua umuhimu wa kundi la wazee katika ujenzi wa taifa hili na kuwa ni muda muafaka kutambua umuhimu wa kupanga mipango yao mizuri kwa maisha ya mbeleni, kutambua hali ya wazee ilivyo sasa walikotoka, walipo na waendako.
Katikati ni kaimu katibu tawala mkoa wa Kagera Isaya Tendega kushoto kwake ni afisa ustawi wa jamii mkoa wa Kagera Issa Mlimi na kulia kwake ni mwenyekiti wa baraza la wazee Kagera mzee Clement Nsherenguzi
"Tunapenda kuchukua fulsa hii kushukuru serikali ya mapinduzi ya Zanzibar kwa kuanzisha mpango wa pensheni jamii kwa kila mzee kuanzia miaka 70, hii ni dalili tosha kuwa swala la jamii limekwishaanza kufanyiwa kazi huko Zanzibar ambayo ni sehemu ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania na sisi tunaomba swala hili lifanyike hata upande wa Tanzania Bara" amesema Nsherenguzi .
Pamoja na maombi ya baraza la wazee zipo changamoto zilizotolewa na kituo cha kulelea wazee Kilima ambazo ni ukosefu wa nyumba ya watumishi pamoja na huduma ya maji katika kituo hicho.
Afisa ustawi wa jamii katika kituo hicho Fatma Seleman amesema, kituo cha wazee kilima kinao wazee 19 wanawake wanne wanaume 15 na kuwa wazee hao wanatoka wilaya za mkoa wa Kagera na nje ya wilaya hizo.
Afisa ustawi wa jamii mkoa wa Kagera Issa Mlimi ameomba wadau mbalimbali kujitokeza kutoa misaada ya hali na mali ili kukarabati majengo ya kituo cha wazee Kilima ikiwa ni pamoja na kumalizia nyumba ya watumishi ambayo iko hatua ya madirisha.
"Tumelileta kwenu hapa ili kupitia kwenu baraza la wazee na mgeni rasmi pamoja na tasisi zinazoshughulikia wazee mkoani Kagera muone umuhimu wa kuwepo jengo la watumishi .
" Tunajua nyinyi huko mnakutana na wadau mbalimbali ambao wanaweza kusaidia ujenzi huu kwani inapofika usiku watumishi wanaondoka eneo la kituo na kwenda kulala nje ya kituo" amesema Mlimi.
Aidha, mgeni rasmi katika maadhimisho hayo Kaimu katibu tawala mkoa Isaya Tendega akimwakilisha katibu Tawala wa mkoa wa Kagera Mashauri Ndaki amesema kuwa, wataendelea kushirikiana na kushikamana na wazee na maombi ya baraza la wazee atayafikisha kwa viongozi husika ili yaweze kufanyiwa kazi.
Ameeleza juu ya changamoto ya kituo hicho kutokuwa na nyumba ya watumishi tayari imeanza kupatiwa ufumbuzi na ofisi ya mkuu wa mkoa wa Kagera imeishatoa mabati kwa ajili ya kuezeka jengo hilo.
Akizungumzia changamoto ya maji iliyopo katika kituo hicho ameahidi kuifikisha kwa mkurugenzi wa halmashauri ya Bukoba ili iweze kutatuliwa, amewaomba wazee kusaidia katika swala la maadili kwa jamii ambalo linaonekana kushuka na vitendo vya ukatili kushika kasi.
"Vitendo vya mauaji, ubakaji na urawiti na ushoga vimeshamili katika jamii yetu hivyo tuendelee kuliombea taifa letu, tuendelee kupiga vita matukio haya kwani hayafai kwa binadamu na katika uso wa dunia.
"Nawaomba wazee tuendelee kuwa chachu ya kuchochea maendeleo, malezi kwa vijana ili wanaokengeuka warudi kwenye mstari" ameeleza Tendega
Ametoa lai kwa vijana wanaozaliwa na wazee hao kuwatunza na swala la wazee kupelekwa kwenye kituo liwe ni la hatua ya mwisho, vijana watimize wajibu wao kila mmoja kwa nafasi yake kumlea na kumtunza mzee wake, waache kuwapeleka katika vituo vya kulelea wazee kwani kuendelea kufanya hivyo vijana wanakwepa majukumu yao.
Kaimu Katibu Tawala mkoa wa Kagera Isaya Tendega ( kushoto) akisalimia na Mwenyekiti wa baraza la wazee mkoa wa Kagera Clement Nsherenguzi
Vilevile katika maadhimisho hayo imetolewa misaada mbalimbali kwa kituo cha wazee ikiwemo fedha na vyakula ambapo mgeni rasmi Tendega alitoa shilingi 100,000, baraza la wazee mkoa kilo 75 za Michele, mafuta ya kupikia lita 10 pamoja na mbuzi.
Misaada mingine iliyotolewa ni pamoja na mkurugenzi wa shirika la saidia Wazee Karagwe na Kyerwa (Sawaka) Livingston Byekwaso aliendesha alambee na kupatikana sh 60,000 huku shirika la kwa wazee Nshamba wilaya ya Muleba likiongozwa na mwenyekiti wake Hussein Ahmada lilitoa mikungu mitano ya ndizi kwa kituo hicho cha wazee Kilima.
Post a Comment