DMO TARIME KUFANYA UKAGUZI MADUKA BINAFSI YA DAWA, MAABARA , ZAHANATI
>>Lengo kuwawajibisha wanaokiuka sheria na miongozo katika utoaji huduma.
>>Wapo wanaouza dawa za serikali kwenye maduka binafsi ya dawa, kuchoma sindano, kutoa watu mimba,
>>Dkt. Vasomana asema kuna maabara zisizokidhi ubora , zahanati zinalaza wagonjwa
>> Katibu wa afya, Mfamasia,Msimamizi wa Maabara,Mwanasheria wawapa elimu wamiliki,watoa huduma maduka ya dawa, maabara, zahanati
Na Dinna Maningo, Tarime
MGANGA mkuu wa halmashauri ya wilaya ya Tarime, Amin Vasomana amewataka wamiliki na watoa huduma katika maduka binafsi ya dawa, maabara na zahanati kuzingatia sheria na miongozo ili kufanya kazi kwa weledi.
Dkt. Amin ameyasema hayo wakati akitoa elimu ya utoaji bora wa huduma ya afya inayozingatia sheria na miongozo kwa wamiliki na watoa huduma kwenye maduka ya dawa muhimu, maabara na zahanati iliyofanyika hivi karibuni Oktoba, 30, 2024 katika ukumbi wa hospitali ya halmashauri hiyo.
Mganga mkuu wa halmashauri ya wilaya ya Tarime, Amin Vasomana akizungumza na wamiliki na watoa huduma kwenye maduka ya dawa muhimu, maabara na zahanati halmashauri ya wilaya Tarime
Amesema mambo hayo ni pamoja na wauzaji au wamiliki wa maduka ya dawa kuchoma watu sindano, kutoa watu mimba vitendo ambavyo havitakiwi kwa mujibu wa sheria na miongozo ya afya.
"Tumeitana leo kuambizana huduma mnayotoa ni huduma ya binadamu lazima mjali afya za wenzenu. Huko kwenye maduka ya dawa kuna watu wanafanya ndivyo sivyo, watu hawana hofu ya Mungu, kitu hukijui unakifanya kwasababu tu unataka pesa, matokeo yake unakuwa chanzo cha kusababisha vifo.
" Hivi karibuni mama mmoja huko Nyamongo alitolewa mimba kwenye duka la dawa akachokonolewa na akafa na duka hilo tumelifunga, matendo kama haya yanaongeza vifo vya mama na mtoto. Pesa huwa haziishi lakini kuwa na utu na kufanya kazi kwa kufuata miongozo na sheria ni jambo la msingi sana.
Wamiliki na watoa huduma ya afya kwenye maabara, maduka ya dawa, zahanati binafsi wakipata elimu ya utoaji bora huduma ya afya
" Sifurahii nione kwenye duka lako la dawa unachoma sindano. Nyie wauguzi ukikaa kwenye duka la dawa huruhusiwi kuchoma sindano ,kumshona mgonjwa kidonda kwasababu hilo eneo sio sahihi la kupata hiyo huduma .
" Kama kuna duka pembeni linafanya hivyo mimi nawapa namba zangu za simu nipigie kama unadhani kuna jambo kwenye duka la mtu linahatarisha maisha mimi sitokutaja jina maana lengo letu sio kuua bali ni kuhudumia wananchi. Kinachoendelea matokeo yake kitapoteza maisha.
Amewanyoshea kidole wataalam wa afya wa Serikali wanaochukua dawa za serikali na kwenda kuziuza kwenye maduka yao binafsi ya dawa au kuwauzia wenye maduka ya dawa na kwamba watakaobainika watawajibishwa.
" Kuna baadhi sio waaminifu dawa zisizoruhusiwa kuuzwa duka la dawa wao wanauza, wengine wanachukua dawa za serikali na kwenda kuziuza kwenye maduka binafsi ya dawa na zahanati binafsi. Wanachukua dawa za ARV wanawauzia watu wanaenda kunenepeshea mifugo tukikuona tunajua kuna mtu pembeni yako anayekupa hizo dawa.
"Dawa za ukoma , TB zinauzwa kwenye maduka binafsi, watu wanauzia watu dawa hata kama hawaumwi ilimradi tu kaona duka lake lina dawa zimeisha muda au zinakaribia kuisha muda" amesema Dkt. Amin.
Amesema kuwa ofisi hiyo imeamua kuwapa elimu ili kukumbushana mambo yanayopaswa kufanywa na yasiyopaswa kufanywa kisha ofisi hiyo itafanya ukaguzi mkali kuwabaini wanaokiuka miongozo na sheria katika utoaji huduma ya afya ili wawajibishwe.
Mganga mkuu wa halmashauri ya wilaya ya Tarime, Amin Vasomana (kulia) akizungumza na wamiliki na watoa huduma kwenye maduka ya dawa muhimu, maabara na zahanati halmashauri ya wilaya Tarime, kushoto ni Katibu wa Afya Halmashauri hiyo Neema Alphonse.
" Tumeona kabla ya kufanya ukaguzi tuwape kwanza elimu tukumbushane ili tukianza kuchukua hatua tusilaumiane na mkiniona msinikimbie kama huelewi kitu uliza tutakupa maelekezo, mnayoyafanya hata Mungu hapendi.
" Sitavumilia mtu yeyote atakayekwenda tofauti kama ni duka la dawa, hospitali, kituo cha afya, zahanati, maabara kuna miongozo na taratibu zake na unapoanzisha huduma hiyo huwa unaelekezwa mambo unayopaswa kufanya" amesema Dkt. Amin.
Amewataka waaalam wa vipimo vya binadamu kwenye maabara kuzingatia taratibu kwani baadhi ya maabara vipimo havina ubora na wengine hawana utaalam wa kutosha jambo ambalo linasababisha watu kubambikiziwa magonjwa wasio nayo.
Katibu wa Afya Halmashauri ya wilaya ya Tarime , Neema Alphonce amewataka watoa huduma kwenye zahanati kutolaza wagonjwa kwani kufanya hivyo ni makosa.
Katibu wa Afya Halmashauri ya wilaya ya Tarime , Neema Alphonce akiwapa elimu wamiliki na watoa huduma ya afya.
" Kila eneo lina miongozo yake kama ni zahanati hupaswi kulaza ni kupumzisha tu. Kama serikali hailazi wagonjwa kwenye zahanati wewe mtu binafsi kwanini ulaze?, kama unataka kulaza fuata utaratibu ili ubadilishiwe hadhi ya kituo chako.
" Na ndio maana hawa watoa huduma wakituona tunapita na gari wanafunga maduka kama vile tuna uhasama licha ya kwamba wakati wanapewa vibali walipewa na masharti ya huduma ambazo wanatakiwa kufanya ndio maana wakituona wanatukimbia maana wanajua wanayoyafanya sio sahihi" amesema Neema.
Msimamizi wa Maabara halmashauri ya wilaya ya Tarime, Albinus Kirina amewaelimisha watoa huduma ya afya kufuata miongozo ikiwemo usajili wa maabara, , uhifadhi wa vitendea kazi, mambo muhimu ya uendeshaji wa maabara.
Msimamizi wa Maabara halmashauri ya wilaya ya Tarime, Albinus Kirina akiwaelimisha wamiliki na watoa huduma ya afya.
Mfamasia wa Halmashauri ya wilaya ya Tarime, Esteria Martine ametoa elimu ya uuzaji wa dawa vikiwemo vigezo vya muuzaji wa duka la dawa, usajili wa maduka ya dawa na vibali, taaluma inayohitajika kwa mmiliki na muuzaji wa dawa pamoja na mtoa huduma anavyopaswa kutoa ushauri kwa mgonjwa.
Mfamasia wa Halmashauri ya wilaya ya Tarime, Esteria Martine akitoa elimu ya taratibu za uuzaji utumiaji na uuzaji wa dawa
Mwanasheria wa Halmashauri ya wilaya ya Tarime, Charles Tem amewakumbusha sheria na miongozo na kuwataka wafanye kazi kwa weledi kama taratibu zinavyotaka.
" Tumewakumbusha sheria mbalimbali ikiwemo sheria ya bodi ya usajili wa huduma za afya. Mfano maabara sheria inamtaka mtu kusajili maabara yake usipofanya hivyo utapelekwa mahakamani na endapo utakutwa na hatia utalipa faini isiyozidi laki mbili, au kifungo kisichopungua au kisichozidi miaka miwili au adhabu zote pamoja.
Afisa Muuguzi mstaafu na mmiliki wa duka la dawa muhimu, mkazi wa Sirari Neema Nyasary ameishukuru ofisi ya mganga mkuu kuwakutanisha watoa huduma ya afya na kuwapa elimu na kuwakumbusha wajibu wao.
Afisa Muuguzi mstaafu na mmiliki wa duka la dawa muhimu, mkazi wa Sirari Neema Nyasary akieleza umuhimu wa kupata elimu kwa wamiliki na watoa huduma ya afya.
" Niliposikia wito wa kuhudhulia kikao nilifurahi sana maana nilijua kuna vitu nitajifunza ambavyo nilikuwa sifahamu na kweli tumekumbushwa taratibu, sheria ,miongozo inasemaje. Tuendelee kukumbishana mara kwa mara tusikae muda mrefu bila kufanya vikao maana tunapokutana hivi inasaidia kujitathimini."amesema Neema.
Neema ameiomba serikali kuongezea dawa zingine ziweze kuuzwa katika maduka ya dawa muhimu kwani uchache wa dawa unapelekea baadhi kutoa huduma zingine zisizoruhusiwa kwenye maduka ya dawa.
"Idadi ndogo ya dawa tunayoruhusiwa kutoa tunajikuta mapato yetu ni madogo hali inayopelekea wengine kushindwa kulipa mapato na wengine kuuza dawa zisizo ruhusiwa. Maana mtu analipa pango, analipa mapato na leseni, mishahara , sasa unakuta zile dawa anazouza hazikidhi mahitaji hayo" amesema Neema.
Ameongeza kuwa, kukiuka sheria ni kosa na hakuna msamaha mtu anapoenda kinyume na sheria huku akiwashauri watoa huduma wenzake kufuata sheria na taratibu zilizowekwa na serikali ikiwa ni pamoja na kulipa mapato.
Post a Comment