HEADER AD

HEADER AD

HIVI NDIVYO ALIVYOTEKWA MFANYABIASHARA JOSEPH MWITA MTIBA


>> Watekaji walikuwa na silaha, walimbeba kwenye gari na kuondoka nae

Na Mwandishi Wetu, Tarime

MATUKIO ya watu kutekwa na kupelekwa kusikojulikana yamekuwa yakiwapa hofu watanzania walio wengi zikiwamo familia ,ndugu, jamaa na marafiki kitendo ambacho kinatakiwa kukemewa vikali.

Siku mbili zilizopita Oktoba, 29, 2024 majira ya saa tatu usiku watu wasiojulikana sura zao wala majina yao walimteka Mfanyabiashara Joseph Mwita Mtiba, mwenye umri wa miaka (47) mkazi wa mtaa wa Remberwi, Kata ya Mkende ,wilaya ya Tarime mkoani Mara na kuondoka nae kusikojulikana.

      Mfanyabiashara  Joseph Mwita Mtiba aliyetekwa na haijulikani aliko.

Habari zinasema kuwa Joseph akiwa ametoka duka la vinywaji la Matogoro lililopo nje ya stendi kuu ya mabasi  barabara ya lami, wasiojulikana wakiwa na bunduki na pisto walimvamia na kumteka kisha kumpandisha kwenye gari aina ya Toyota Land cruiser na kuondoka nae kusikojulikana.

DIMA ONLINE imefanikiwa kuzungumza na mashuhuda wa tukio hilo lililotokea katikati ya mji wa Tarime barabara ambayo haina taa za barabarani, nao walikuwa na haya ya kusema; 

Mtoto aeleza ilivyokuwa

Ibrahim mwenye umri wa miaka (25) ni mtoto wa Joseph Mwita ambaye walikuwa wote pamoja wakati tukio hilo likitokea na kushuhudia kilichoendelea huku akimwona baba yake akizingirwa na watu ambao hakuweza kuwatambua na kisha kumpakia kwenye gari na kuondoka nae.

     Gari linalodaiwa kutumiwa na watekaji kumbeba Joseph Mwita Mtiba na kuondoka nae mahali kusikojulikana

" Tulikuwa tumetoka kwenye msiba wa Awoo kule Msati. Badae tulitelemka kwa miguu hadi kituo cha maegesho ya pikipiki kilichopo hoteli ya Milani tukapanda pikipiki moja ikatupeleka hadi mjini, ikatushusha pembeni ya barabara karibu na maduka yaliyopo nje ya stend.

" Baba yeye akavuka barabara hadi dukani kwa Matogoro kuchukua dawa ya mdogo wangu anayeumwa ambayo alikuwa amemwagiza mtu Sirari amletee aiache dukani kisha ataipitia achukue.

" Mimi na dereva wa pikipiki tulisimama tukiwa tunamsubiri, ile anataka kuvuka barabara wanaume watano wakavuka barabara na kumfuata baba upande wa pili wa barabara alikokuwa akitokea dukani" anasema Ibrahim.

"Anaongeza kusema " Wakati tunamsubiri baba baada ya dakika tano hivi kuna gari aina ya Landcruiser lilitoka nyuma yetu uelekeo tulikotoka likapita mbele yetu kidogo na tulipokuwa tumesimama likasimama.Ghafla wakatoka wanaume watano waliovalia mavazi ya kiraia wawili wakiwa wameshikilia bunduki wakavuka barabara kwenda upande alikokuwa anatokea baba wakamzingira.

"Baba aliwauliza mnanipeleka wapi ? lakini hawakumwambia akawa anajitahidi kutoingia ndani ya gari tukapiga kelele watu nao waliokuwepo eneo hilo walikuwa hawajui kinachoendelea walikuwa wakishangaa. Baada ya mvutano huo wa baba kugoma kuingia ndani ya gari watu waliongezeka kama zaidi ya kumi wakapiga yowe.

" Wale watu walivyoona kelele inaongezeka watatu wakachomoa bastora na wale wawili wakanyoosha bunduki wote wakazikoki watu wakaogopa wakamzidi nguvu baba huku wakiwa wamemzingira wamemzibiti na kufanikiwa kumweka kwenye gari na kuondoka nae" anasema Ibrahim.

Anasema baada ya baba yake kuchukuliwa aliwapigia simu ndugu zake kisha wakatoa taarifa kituo cha polisi eneo la Komaswa lakini hawakufanikiwa kuzuia gari.

" Tulipiga simu kituo cha polisi kule beria ya Komaswa tukawaambia kilichotokea na kuwaomba wafunge beria (kizuizi) wakague hilo gari . Tukaambiwa kuna gari moja lilipita pale la serikali wakasimamishwa lakini gari liliwashwa taa na likaruhusiwa kuondoka" anasema Ibrahim.

Anasema kulipokucha asubuhi yeye na ndugu zake walifunga safari kwenda kituo cha polisi Bomani wakauliza kama Polisi wana taarifa ya mzazi wake kushikiliwa na Polisi nao wakasema hawana taarifa ya baba yake kutekwa.

"Tulienda kwa OCCID kituo cha polisi Bomani tukamuuliza akasema hana taarifa ya hao watu . Tukatoa taarifa hadi ofisi ya RCO Tarime, Rorya nao wakasema hawana taarifa. Tukafungua Jarada ofisi ya mkuu wa upelelezi makosa ya jinai namba 28/2024 tunasubiri uchunguzi wao.

" Tunawaomba Polisi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama na watu mbalimbali, serikali watusaidie kumtafuta baba yangu ili haya matukio ya utekaji yasiwepo. Bado tunamtegemea baba yetu ana wake wawili na watoto sita " anasema Ibrahim.

 Ndugu wa Joseph aeleza 

Ndugu wa Joseph ambaye ni mfanyabiashara Lucus Soteri anasimulia jinsi ndugu yake alivyompigia simu kabla ya kutekwa.

"Hiyo siku ya tarehe 29 niliamka asubuhi nikaenda shambani kufanya kazi, mida ya saa mbili asubuhi Joseph alinipigia simu akaniuliza uko wapi ? Nikamwambia mimi nipo shambani baadae aliniuliza tena hutokuja Tarime mjini nikamwambia nikitoka shambani nitakuja.

" Mida ya saa nane mchana aliniuliza umeshatoka shambani ? akaniambia niko hapa msibani kwa mzee Awoo. Akaniuliza utakuja Tarime? nikamwambia hapana nimechoka. Akaniambia hata hawa wabaya wetu nao wako hapa.

" Nikamwambia hapo siupo karibu na watu hawatakufanya chochote . Mida ya saa kumi na moja nilikuja mjini kwenye shughuli zangu kisha nikaonda zangu nikaenda nyumbani . Saa moja na nusu usiku nikaenda Sirari kwenye kazi zangu.

Anaongeza kusema " mida ya saa tatu na dakika 26 Ibrahimu mtoto wa Joseph alinipigia simu akaniambia baba mdogo, baba ametekwa nikamwambia simpige yowe ,akasema wale watu wameshuka na mabunduki na wanatishia watu . Walifanya haraka haraka wakampandisha kwenye gari na kuondoka nae.

" Baada ya hizo taarifa nikafika Tarime mjini nikafuatilia nikaenda hadi Komaswa bahati nzuri nilimkuta askari mmoja akaniambia hiyo gari imepita hapa tumeisimamisha lakini haikusimama, ni gari aina ya Toyota Landcruiser.

" Tuliendelea kutoa taarifa tukawaambia watu wa beria pale Kirumi tukawapigia simu tukawaeleza ili wafunge beria wakague. Kuna gari moja lilienda pale kama la serikali wakasimama kwenye beria wakawawashia taa na gari likaruhusiwa kuondoka.

Anazidi kusema " Leo tumeeenda (Jana) polisi tulipowapa hiyo taarifa wakasema hawana taarifa ya yeye kutekwa kisha tukafungua Jarada la uchunguzi. 

"Tunawaomba watanzania watusaidie kumtafuta ndugu yangu ili apatikane,  kama waliona ana makosa wangempeleka polisi na ni haki yetu kupewa taarifa kufahamishwa " anasema Lucus.

Mke wa Joseph aiangukia Serikali

Monica ni mke wa Joseph anaiomba serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na mwanamke mwenzie Dkt. Samia Suluhu Hassan kumsaidia kumtafuta mmewe kwakuwa yeye ndiye kila kitu katika familia na akikosekana watoto watateseka kwani maisha bila baba ni mateso.

" Nilifuatilia hadi kituoni lakini walisema hawana taarifa. Naiomba serikali , rais Samia ukiwa kama mwanamke mwenzangu mama mwenye mme kama mimi naomba unisaidie mme wangu aweze kupatikana ndiye tegemeo letu. Nakuomba sana niko chini ya miguu yako nisaidie najua wewe ni Rais ukiamua jambo hakuna kitakachoshindikana na mme wangu atapatikana " anasema Monika.

Shuhuda wanena

Mfanyabiashara mmoja mwenye duka jilani na tukio lilikofanyika anasema kuwa watu hao walikuwa na silaha nzito za kivita jambo ambalo liliwafanya watu kuduwaa na hivyo kufanikiwa kumteka mtu huyo.

" Huyo mtu wakati anatoka dukani ghafla alivamiwa na watu wasiojulikana wakamteka, kuna mmoja alitokea uchocho mdogo huu wa kuingia stendi kuu ya mabasi akamtokea kwa nyuma akamkaba, ghafla wakaja watu wengine wanne wakamzunguka. Wale watu walikuwa na silaha nzito za kivita iliogopesha sana kiasi kwamba kila aliyekuwepo alizubaa akiwashangaa " anasema .

Shuhuda mwingine ambaye ni mwendesha pikipiki katika eneo la maegosho walikokuwa hao watekaji anasema " Wale watu walikuwa wengi , watano walishuka kwenye gari wakamfata yule jamaa na wengine walibaki kwenye gari.

" Wawili walikuwa na Bunduki zile zinazotumiwa na Polisi na watatu walikuwa na Pisto. Yule mtu alikuwa na nguvu sema walimzidi kwakuwa wao walikuwa wengi. Watu walipiga kelele lakini hazikufanikiwa maana walitekeleza tukio harakaharaka wakamdhibiti na kuondoka nae.

" Ilikuwa ngumu kutambua maana hili eneo halina taa za barabarani na wananchi hawakuwa na silaha za kupambana na watekaji. Kiukweli yule jamaa alipiga kelele kuomba usaidizi, bodaboda walipiga kelele. 

"Walipoona watu wameongezeka wote wakainua siraha zao wakazikoki watu wakaogopa wakamchukua na kumweka ndani ya gari na kuondoka nae . Eneo kulikofanyika tukio ni jirani na stendi kuu ambako kuna kituo cha Polisi inamana hicho kituo hakukuwa na askari ? maana yowe ilipigwa na pale ni jirani walisikia wangeonyesha ushirikiano, labda nao waliogopa" anasema mwendesha pikipiki mmoja.

Hata hivyo shuhuda mmoja alifanikiwa kupiga picha gari la watekaji lililombeba Joseph ambalo namba zake za usajili hazikuweza kuonekana kutokana na eneo hilo kutokuwa na taa za barabarani.

Kwa mujibu wa jeshi la Polisi Tarime, Rorya limepata taarifa za kutekwa kwa Joseph Mwita Mtiba zilizoripotiwa Polisi na familia na linaendelea na uchunguzi.

Isemavyo Katiba ya Jamhuri 

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 Ibara ya 13 (1) inasema watu wote ni sawa mbele ya sheria, na wanayo haki, bila ya ubaguzi wowote, kulindwa na kupata haki sawa mbele ya sheria.

Katika Ibara hiyo (e) inasema ni marufuku kwa mtu kuteswa, kuadhibiwa kinyama au kupewa adhabu zinazomtweza au kumdhalilisha.

Ibara ya 14 inasema kila mtu anayo haki ya kuishi na kupata kutoka katika jamii hifadhi ya maisha yake , kwa mujibu wa sheria.

No comments