WANAWAKE SIMIYU WAPATIWA ELIMU MATUMIZI NISHATI SAFI YA KUPIKIA
Na Samwel Mwanga, Maswa
KATIKA jitihada za kuhakikisha wanawake wanaondokana na matumizi ya kuni na mkaa, Umoja wa Wanawake na Samia mkoa wa Simiyu umeendelea kutoa elimu ya matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa kundi hilo.
Hatua hiyo ni juhudi za kuunga mkono jitihada za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ameonyesha dhamira ya kulinda mazingira na kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala.
Pia imelenga kupunguza ukataji miti kwa ajili ya kuni na mkaa, jambo ambalo linasababisha uharibifu mkubwa wa misitu na kuharibu mfumo wa ikolojia.
Akizungumza katika mkutano uliofanyika Novemba 6 mwaka huu, uliofanyika kwenye ukumbi wa halmashauri ya wilaya hiyo, Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake na Samia mkoa wa Simiyu, Mwanahawa Said amesema kuwa kampeni hiyo inalenga kuunga mkono juhudi za serikali na wanatarajia kutembelea wilaya zote za mkoa huo.
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake na Samia mkoa wa Simiyu,Mwanahawa Said akizungumza na wakinamama wa wilaya ya Maswa katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya ya Maswa.
“Serikali imeweka malengo yake kuwa hadi kufikia mwaka 2025 asilimia 80 ya wanzania wote wawe tayari kuanza kutumia nishati safi wakati wa kupika chakula ili kulinda afya,kukuza uchumi na kulinda mazingira na sisi kwa kuanzia tumeanza kutoa elimu ya matumizi ya makaa ya makaa ya mawe katika kupikia,”amesema.
Amesema kuwa watu wengi wanapata madhara kutokana na matumizi ya nishati isiyo sahihi na kuna maeneo mengi hapa nchini huku akitolea mfano wa mkoa wa Simiyu yanabaki jangwa kutokana na ukataji wa miti.
“Tunahitaji kwa sasa kupunguza matumizi ya kuni na mkaa na hii itapunguza ukataji wa miti, ambao umekuwa ukichangia sana katika uharibifu wa misitu na kuharibu vyanzo vya maji na miti inapopotea na kuwa jangwa na mfano mzuri ni kwenye mkoa wetu wa Simiyu, kunakuwa na hatari ya kuongezeka kwa mmomonyoko wa udongo na kupungua kwa mvua, hali inayoweza kuathiri kilimo na uzalishaji wa chakula,”amesema.
Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka Halmashauri ya wilaya ya Maswa, Lucia Misinzo amesema kuwa shughuli zinazofanywa na Mamalishe, Wachoma Chipsi na wenye Magenge wengi wao wamekuwa wakitumia nishati ya mkaa na kuni katika kupikia hivyo kwa sasa wameona njia pekee ya kuwatoa huko ili waweze kutumia nishati safi ya kupikia.
Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka Halmashauri ya wilaya ya Maswa, Lucia Misinzo akisisitiza wanawake kujiunga kwenye vikundi ili waweze kupata mikopo ili waweze kuwa mawakala wa kuuza
makaa ya mawe ambayo ni nishati safi ya kupikia.
“Serikali kwa sasa inatoa mikopo kwa makundi maalum ambayo ni wanawake, vijana na wenye ulemavu na kwa wilaya ya Maswa tumetenga kiasi cha Tsh. Milioni 314 kwa ajili ya mikopo hiyo.
" Niwahamasishe wanawake muunde vikundi vyenu na mvisajili hapa ofisini kwetu ili muweze kupata mikopo na wengine mnaweza kuwa mawakala wa kuuza makaa haya ya mawe, hii ni fursa ili tuweze kuiondoa jamii yetu kutumia nishati ya kuni na mkaa wa miti,”amesema.
Deograsia Chidege mkazi wa Majebele mjini Maswa ambaye ni Mamalishe ameeleza kuwa kutumia nishati safi katika kupikia itasaidia kuhifadhi afya kwani matumizi ya mkaa na kuni hutoa moshi wenye madhara, unaosababisha magonjwa ya kupumua, hata kuongeza hatari ya saratani na macho kuwa mekundu ambapo katika mkoa huo utafsiriwa kuwa ni mchawi.
Sehemu ya wakinamama wa wilaya ya Maswa waliohudhuria mafunzo ya matumizi ya nishati safi ya kupikia katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya hiyo.
“ Kwa kutumia nishati safi, sisi wanawake tunaweza kupika bila kuvuta moshi wenye sumu na hii itasaidia kuhifadhi afya zetu na wakati wengine ukitumia kupikia kuni muda mrefu ni lazima macho yako yawe mekundu na huku ukionekana hivyo unahusishwa na vitendo vya kishirikina kwa kuitwa mchawi,”amesema.
Naye Mwanahawa Mwanzalima mkazi wa mjini Maswa amesema kuwa ujio wa nishati safi kutasaidia kupunguza muda na mzigo wa kazi kwani kuni mara nyingi hupatikana kwa kutembea umbali mrefu, kazi ambayo mara nyingi wamekuwa wakiifanya kwa kusaidiaba na watoto wao,hivyo kwa kutumia nishati hiyo wataokoa muda na nguvu, na hivyo kuwekeza muda huo katika shughuli nyingine za maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
“Ni muhimu pia kwa serikali na mashirika mbalimbali ya maendeleo hapa nchini kuunga mkono juhudi hizi za matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa kuweka miundombinu inayowezesha upatikanaji rahisi na wa gharama nafuu wa makaa ya mawe kwa kaya za kipato cha chini,”amesema.
Post a Comment