HEADER AD

HEADER AD

MWALIMU ATUHUMIWA KUMBAKA MWANAFUNZI


Na Alodia Dominick, Muleba 

MWALIMU wa taaluma Lameck Jonas wa shule ya msingi Rulanda kata ya Rulanda wilaya ya Muleba, mkoani Kagera anakabiliwa na tuhuma ya kumbaka mwanafunzi wake muhitimu wa darasa la saba .

Mwanafunzi huyo ni wa umri wa miaka 13 ambapo anatuhumiwa kumpaka vitu vinavyosadikiwa kuwa ni madawa ya kulevya vilivyosababisha mtoto huyo kupoteza fahamu na kisha kufanyiwa ukatili.

Tukio hilo la ubakaji lilifanyika Oktoba 30, mwaka huu majira ya jioni baada ya mtoto huyo akiwa na wanafunzi wenzake kufika shuleni hapo majira ya mchana kwa ajili ya kuomba mwalimu huyo awaangalizie matokeo ya mtihani wa darasa la saba.

Imeelezwa kuwa mtuhumiwa alimwambia aliyefanyiwa ukatiri kuwa ameshindwa mtihani hivyo arudi baadaye ili ampe ushauri.

        Shule ya msingi Rulanda

Mwanafunzi ambaye alifanyiwa kitendo cha ukatili akisimulia mkasa huo huku akitiririka machozi asema kuwa, baada ya mwalimu Jonas kuangalia matokeo yao akiwa na wenzake watatu na kukutwa yeye ameshindwa na kupata daraja D alimwambia arudi jioni ili ampe ushauri.

“Nilirudi nyumbani nikawambia wazazi kuwa nimeambiwa na mwalimu nimeshindwa mtihani hivyo nirudi shuleni saa 10:00 jioni anishauri.

"Ulipokaribia huo muda wazazi waliniruhusu nilirudi shuleni nimsikilize mwalimu Jonas, niliporudi nilimkuta ofisini akaniambia niende darasani tulikokuwa tunasomea atanikuta”

“Nilimsubili darasani na baada ya muda alifika akaanza kufunga madirisha na mlango alipomaliza akaniambia nivue nguo nikakataa akanifungua zipu akaanza kunipaka dawa kwenye shingo, matiti, kwapani na kwenye kitovu.

" Akatoa nyingine akanipaka mgongoni alipomaliza akachukua nyingine ziko kama sukari akanipa ninywe nikakataa akaninywesha na maji kwa nguvu” alisimulia mtoto huyo.

Mtoto huyo ameongeza kuwa, mwalimu huyo baada ya kumpaka dawa sehemu hizo alivua nguo zote kama vile anaenda kuoga ndipo alitoa dawa nyingine na kuanza kumsugua sehemu za siri baada ya hapo alipoteza fahamu hakujua kilichoendelea alizinduka muda wa jioni na kumuona mwalimu huyo akichungulia dirishani mara mbili kuona kama kuna watu.

Amesema alipoona hakuna watu alimwambia aende nyumbani alipotoka nje alimuita akamwambia wazazi wake baba na mama wakimuuliza kwa nini amechelewa shuleni awadangaye alienda kwa rafiki zake.

Amesema akamwambia wakimuuliza mdomo mbona umekauka umekuaje aseme ndivyo alivyokuwa na kwa sababu alikuwa anatembea kwa kuchechemea kutokana na maumivu aliyokuwa anasikia sehemu zake za siri aliambiwa na mwalimu huyo akiulizwa aseme ndivyo anatembea au ameanguka chini.

Aidha amesema mwalimu Jonas alimwambia kuwa, akipata shida yoyote amtume mdogo wake wa miaka (11) ambaye anasoma shuleni hapo ili amfikishie taarifa mwalimu aone atafanyaje na alimsisitiza asiwaambie wazazi na mtoto huyo aliondoka akaenda nyumbani na kuwaeleza wazazi wake kilichotokea.

Kwa upande wa mama wa mtoto huyo mkazi wa kitongoji cha Kituntu kata ya Rulanda alisema kuwa, ilipofika saa 11:30 aliona mtoto anachelewa kurudi nyumbani ndipo alimfuata shuleni bila mafanikio.

“Nilipofika shuleni niliona pikipiki ikiwa imepakiwa nje katika mazingira ya shule sikusikia kelele kwenye mazingira yale na sikuona mtu yeyote na nilidhani ile pikipiki ilikuwa ya mtu  ambaye alikuwa ameenda ziwani hivyo niliamua kurudi nyumbani nikawa na maswali mtoto ameenda wapi mbona siyo kawaida yake kufika huu muda hayupo nyumbani” alijiuliza mama

Mama huyo ameeleza kuwa, ilipofika saa 1:00 jioni mtoto alifika nyumbani ndipo alianza kumuhoji mtoto sehemu alipokuwa ndipo alimwambia mama yake kuwa, alikuwa shuleni mwalimu Jonas alimfungia kwenye chumba cha darasa na kumpaka dawa sehemu mbalimbali za mwili wake na kuwa alimbana midomo asipige kelele.

“Nilipomchunguza mtoto wangu nilibaini ameingiliwa kimwili kwanza alikuwa anatembea kwa kuchechemea akisema anapata maumivu sehemu za siri pia niligundua michubuko sehemu zake za siri” amesema mama

Ameongeza kuwa, baba wa mtoto alipofika nyumbani alimweleza yaliyomsibu binti yake wakaamua kwenda kituo cha polisi Muleba wakapewa fomu namba tatu (PF3) kwa ajili ya kwenda hospitali kufanyiwa vipimo ndipo walipompeleka kituo cha Afya Kaigara.

Amesema baada ya kwenda kituo cha polisi na mtuhumiwa kutoweka, baadhi ya ndugu zake waliojitambulisha kuwa ni kaka na rafiki zake walifika nyumbani kwao na kuomba walimalize jambo hili kirafiki kwa ahadi ya kuwapa kiasi cha fedha ambacho hawakukitamka.

Walilalamika kuwa, ndugu yao atapoteza kazi kwa muda ambao hajafika kazini mama akawahoji vipi kuhusu mwanangu aliyefanyiwa ukatili, hawakuwa na majibu, ndipo walipowaeleza kuwa hawahitaji fedha zao bali wanataka sheria ifuate mkondo wake.

Naye Mkurugenzi mtendaji wa halamshauri ya Muleba ambaye ni mwajiri wa mtuhumiwa Isaya Mbenje amesema, alipokea taarifa kutoka shule ya msingi Rulanda kwamba kuna tuhuma za mwalimu Lameck Jonas kufanya tendo la ukatili ambaye hajapata taarifa za umri wake.

      Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Muleba Isaya Mbenje amesema mwalimu huyo akibainika na kosa mahakamani atapelekwa tume ya maadili ili achukuliwe sheria za kinidhamu ikiwemo kusimamisha mshahara wake

Mbenje amesema, taarifa za awali zinaonyesha mwanafunzi huyo amemaliza darasa la mwezi Oktoba mwaka huu amefanyiwa ukatili na mwalimu huyo, bahati nzuri wazazi wake walipata taarifa kwa wakati na kutoa taarifa kituo cha polisi na mwalimu anaendelea kutafutwa inaonekana baada ya tukio hilo kutokea mwalimu alitoweka.

Ameongeza kuwa yeye kama mwajiri wake anamtafuta kwa ajili ya kuhakikisha anafikishwa kwenye vyombo vya dola ili sheria ichukue mkondo wake. 

“Jambo hili kwanza halikubaliki siyo maadili kwa mtu yeyote mwenye akili timamu kufanya ukatili wa namna hii kwa mtoto ambaye tunaona maisha yake ya baadaye ana nafasi ya kulitumikia taifa letu kwa njia mbalimbali.

Pia ana nafasi ya kuendelea kusoma kama mzazi na kama mwajili siwezi kukubali wala kuruhusu vitendo hivyo vifanywe na watumisi wa umma” ameeleza Mbenje.

Amesema hicho ni kitendo cha aibu kwa mwalimu aliyeaminiwa na kutegemewa kuwafundisha watoto kuwaelekeza na kuwafunza maadili mema sasa kitendo cha kubadilika na kuwa mnyama hiki kitendo hakikubaliki.

Diwani wa kata ya Rulanda Evart Ernest amesema kuwa, alipokea taarifa za mtoto kubakwa Oktoba 31, mwaka huu majira ya saa 12:30 asubuhi kutoka kwa afisa elimu kata aliyempigia simu juu ya tukio hilo na kumjulisha kuwa tayari hati ya kumkamata mtuhumiwa kutoka jeshi la polisi imetolewa.

      Diwani wa kata ya Rulanda Evert Ernest akizungumza juu ya tukio hilo

Ernest amesikitishwa wakati anafuatilia swala hilo asubuhi alipomtafuta mzazi akasema ameenda kwa mtendaji wa kijiji kwa ajili ya kwenda kumkamata mtuhumiwa saa 11:00 alfajiri hakufunguliwa mlango hadi alipompigia yeye saa 2:00 asubuhi na kumuhoji kulikoni ndipo mtendaji alimjibu alikuwa anaoga.

“Ukiangalia muda huo unaona kama kuna tatizo maana haiwezekani mtu umwamshe tangu saa 11:00 alfajiri hadi saa 2:00 asubuhi adai alikuwa anaoga, uzembe huo ndiyo ulisababisha mtuhumiwa kutoroka kabla hajakamatwa” amesema Ernest.

Aidha amewashauri wazazi kurudi kituo cha polisi, wakiwa polisi walimweleza diwani kuwa polisi wamenyimwa ushirikiano wanawarusharusha na wanapewa kauli za kukatisha tamaa, ndipo naye alienda kituoni na kumpigia mkuu wa polisi wilaya (OCD) akatoa maelekezo wakamuone mkuu wa kituo (OCS).

Ernest baada ya kuzungumza na OCS alimwambia kuwa, mtuhumiwa huyo lazima akamatwe na kudai kuwa kuna matukio mengi kulingana na mtoto alivyoeleza yakiwemo madawa anayodaiwa kumpaka mtoto huyo.

Alipohojiwa kama kuna matukio mengine ya ubakaji katika kata yake alisema hilo ni tukio la kwanza labda matukio mengine ya ukatili yapo kama vile wazazi kutelekeza familia, vipigo vilivyopitiliza na watoto kutumikishwa chini ya umri.

Wilmina Projestus mkazi wa kijiji cha Rulanda amesema, vitendo hivi vya ukatili vimekuwa kama mazoea na wao wazazi wameanza kuogopa imekuwa ni changamoto kubwa, enzi zao walikuwa wakisoma shule hakukuwa na vitendo hivyo walikuwa wakivisikia mikoa ya mbali sasa hivi vimeingia kila mkoa.

“Tunaiomba serikali iwe na mpango maalumu wa kudhibiti vitendo hivi katika jamii kwa kuanza kutoa elimu kwa wanafunzi kuhusu masuala ya ukatili kwa sababu ukatili ni mwingi watoto wetu tuwalinde ili waweze kujitambua na kukwepa kuingia katika mitego ya wabakaji” amesema Wilmina.

Yusto Bakuju mkazi wa kitongoji Kituntu alisema, kitendo cha ukatili alichofanyiwa mtoto huyo ni unyama unaolenga kumkatisha tamaa mtoto katika maisha yake sababu bado ni mdogo na ana ndoto nyingi, unyama aliofanyiwa ni mbaya unaweza kumuathiri akili yake.

        Yusto Bakuju mkazi wa kitongoji cha Kituntu kata ya Rulanda amekemea kitendo hicho.

Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Kagera Blasius Chatanda alipohojiwa kwa njia ya simu amesema, yupo safarini kuelekea wilayani Misenyi na kuwa atafuatilia na kutoa taarifa Novemba saba, mwaka huu.

Hata hivyo, tukio hilo limeibuliwa na Chama cha waandishi wa habari wanawake mkoa wa Kagera chenye lengo la kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia na kujenga usawa wa kijinsia.

No comments