HEADER AD

HEADER AD

DC AAGIZA MAAFISA WA TASAF KUONDOLEWA


Na Samwel Mwanga, Maswa
 
MKUU wa Wilaya ya Maswa, Aswege Kaminyoge, ametoa agizo la kuondolewa kwa Mratibu wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) wilayani humo, Grace Tungaraza, pamoja na Afisa Ufuatiliaji wa mfuko huoJohn Wambura kwa madai ya kushindwa kusimamia miradi ya maendeleo inayoendelea kutekelezwa katika wilaya hiyo.
 
Uamuzi huo umetolewa Desemba 14 mwaka huu mara baada ya mkuu huyo wa wilaya akiambatana na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa wilaya ya Maswa  kufanya ukaguzi wa miradi inayotekelezwa na TASAF.

        Mkuu wa wilaya ya Maswa,Aswege Kaminyoge akiongea na Wataalam wa halmashauri ya wilaya  Maswa hawapo pichani baada ya kukagua ujenzi wa zahanati kijiji cha Mbaragane.

Miradi iliyotembelewa ni pamoja na ujenzi wa zahanati na nyumba ya mganga katika kijiji cha Mbaragane kwa gharama ya Tsh. 92,410,714.29  pamoja na ujenzi wa bweni la wasichana katika Shule ya Sekondari Badi kwa gharama ya Sh 160,511,505.69
 
Kwa mujibu wa Kaminyoge, fedha za ujenzi wa miradi hiyo zilitolewa na serikali kwa muda mrefu, lakini utekelezaji wake umekuwa wa kusuasua, hali inayozua maswali kuhusu usimamizi wa rasilimali na uwajibikaji wa viongozi husika.

        Mkuu wa wilaya ya Maswa,Aswege Kamiyoge(wa kwanza kulia)akizungumza na mafundi wanaojenga Zahanati ya Kijiji cha Mbaragane
 
“Fedha ya ujenzi wa zahanati na bweni la wasichana zimeingia katika akaunti yenu ya halmashauri tangu mwezi wa tano lakini hadi sasa ujenzi bado unasuasua majengo ya zahanati bado ndiyo yako hatua ya msingi na mabweni ndiyo yako usawa wa madirisha na tulipanga kufikia tarehe 30 mwezi huu yawe yamekamilika na kuanza kutumika,”
 
“Lakini hapa kuna uzembe nimekuwa nikitoa elimu kila mara ila kwa sasa nimefikia kikomo nimechoka mtanisamehe hivyo naagiza mratibu wa TASAF na afisa ufuatiliaji wote waondolewe na tupate watu wengine ambao wataweza kusimamia hii miradi,”amesema.
 
Amesema watakaochukua nafasi hizo mara baada ya maafisa hao kuondolewa ni lazima wahakikishe miradi hiyo inakamilika kwa wakati ili kuweza kuleta manufaa kwa wananchi.
 
Akizungumza mara baada ya agizo hilo,Grace Tungaraza amesema kuwa licha ya jitihada wanazozifanya kusimamia miradi hasa ya ujenzi inayotekelezwa na mfuko huo wanakumbana na changamoto ya wananchi katika kuchangia miradi hiyo nguvu zao kama ilivyoelekezwa.

          Jengo la Zahanati ya Mbaragane inayojengwa na TASAF.
 
“Katika miradi hii tunayoitekeleza ni lazima wananchi wachangie asilimia 10 ambazo ni mchanga,mawe,maji na kokoto lakini wanaotuangusha ni hawa viongozi wetu wanaowasimamia wananchi pamoja na watendaji wa Vijiji na watendaji wa Kata,”amesema

Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Shedrack Mziray akizungumza kwa njia ya simu agizo  hilo la Mkuu wa wilaya ya  Maswa, Kaminyoge amesema kuwa ni vizuri Maafisa wa Mfuko huo wakatekeleza majukumu yao ili kuweza kufikia malengo ya kuwasaidia wananchi kama ilivyokusudiwa.
 
“Uamuzi wa mkuu wa wilaya ya Maswa ni uamuzi sahihi na ninavyomfahamu kwa usimamizi huwa yuko vizuri hivyo nikuhahidi agizo lake tutalifanyia kazi lakini niwakumbushe watumishi wote wa TASAF kufanya kazi ili kufikia malengo tuliyojiwekea ya kuwahudumia wananchi,”amesema.
 
       Jengo la bweni la Wasichana katika shule ya sekondari Badi wilaya ya Maswa linalojengwa na TASAF.

No comments