HEADER AD

HEADER AD

BITEKO MGENI RASMI TAMASHA LA IJUKA OMUKA KAGERA

Na Alodia Dominick, Bukoba

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati hapa nchini Doto Biteko anatarajia kuwa mgeni rasmi katika tamasha la Ijuka Omuka likiwa na lengo la kuonyesha fursa mbalimbali za kibiashara zinazopatikana mkoani Kagera.

Tamasha hilo linalotarajiwa kuzinduliwa Desemba 19, 2024.  Ijuka Omuka ni lugha ya kihaya kwa kiswahili maana yake ni kumbuka nyumbani, ni tamasha linalowashirikisha wanakagera wanaoishi ndani na nje ya mkoa wa Kagera na wadau mbalimbali wa maendeleo. 

Mkuu wa mkoa wa Kagera Fatma Mwasa ndiye mwanzilishi wa tamasha la Ijuka Omuka na mwaka huu linafanyika tamasha la pili, mwaka jana lilikuwa tamasha la kwanza.

Mwasa akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari ofisini kwake Desemba 14, 2024 amesema uzinduzi utafanyika Desemba 19,2024 na mgeni rasmi atakuwa ni Naibu Waziri mkuu na Waziri wa Nishati nchini Doto Biteko.

     Waandishi wa habari wakizungumza na mkuu wa mkoa wa Kagera Fatma Mwasa

Amesema Ijuka omuka ya mwaka jana haikuhusisha wadau wengi na kuwa ya mwaka huu itahusisha matukio manne ambayo Desemba 18,2024 dua ya kuombea mkoa, taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, yatazinduliwa maonyesho ya biashara ambayo yatadumu kwa siku 10.

"Siku ya tarehe 19,2024 ni siku maalumu kwetu tutaanza na kongamano la biashara na hili litakuwa maalumu kwa wafanyabiashara pamoja na watendaji wa serikali ili kuondoa changamoto zote za kibiashara zinazowakabili wafanyabiashara" amesema Mwasa 

Amesema kuwa, Desemba 19 mchana litakuwepo tamasha la utamaduni wa mtu wa Kagera, Desemba 20,2024 yatakuwepo mashindano ya pikipiki, jioni yatakuwepo maonyesho ya mavazi na milindimo ya pwani na watakuwepo wasanii mbalimbali.

Desemba 21,2024 mchana yatakuwepo mashindano ya mpira wa miguu kati ya timu ya Simba na Kagera sugar na jioni watakuwepo wasanii mbalimbali wa kizazi kipya.

     Mkuu wa mkoa wa Kagera Fatma Mwasa akizungumza na waandishi wa habari ofisini

Aidha ameeleza kuwa, Desemba 22, 2024 itakuwepo ibada na matukio mengine yataendelea na kuwa maonyesho ya biashara yataendelea hadi Desemba 26,2024.

Hata hivyo, tamasha la Ijuka Omuka limeanza mwaka jana na mwaka huu itakuwa ni mara ya pili kufanyika na mwaka jana mkuu wa mkoa Mwasa alitambulisha tamasha hilo kwa wadau wakachangia michango mbalimbali kwa ajili ya ujenzi wa uzio wa bweni la wasichana Sekondari ya Omumwani pamoja na sekondari ya Bukoba.


No comments