HEADER AD

HEADER AD

DC CHATO AMWAGIZA MKURUGENZI KUKAMILISHA MIRADI YA WANANCHI


Na Daniel Limbe, Chato

MKUU wa wilaya ya Chato mkoani Geita, Louis Bura, ameitaka halmashauri ya wilaya hiyo kusaidia ukamilishaji wa miundo mbinu ya shule ya sekondari Mkolani kata ya Bwongera kutokana na  wananchi wa Kijiji hicho kutumia nguvu zao kujenga vyumba vitatu vya madarasa pamoja na ofisi ya walimu.

Hatua hiyo inalenga kuwanusuru watoto kutembea umbali mrefu pamoja na vishawishi wawapo njiani hali inayoweza kushusha taaluma kwa wananafunzi hao.

        Kulia ni mkuu wa wilaya ya Chato,Louis Bura,akizungumza na baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Mkolani -Bwongera

"Mkurugenzi upo hapa na umeona jitihada za wananchi hawa, kazi kubwa wamefanya kwa nguvu zao na sisi serikali kazi yetu kubwa ni kuwaunga mkono kwa jitihada zao walizofanya, niombe muone namna ya kusaidia kumalizia ujenzi huu.

"Niwashukuru sana wananchi wa Bwongera kwa kazi kubwa mliyoifanya, serikali ya awamu ya sita itaendelea kuwaunga mkono kwa kadri itakavyowezekana ili kuhakikisha watoto wote wanapata mazingira mazuri ya kusomea" amesema.

Katika hatua nyingine Bura ameonyesha kufurahishwa na jitihada za wananchi wa kata ya Muganza, kwa kujitolea zaidi ya Tsh. Milioni 10 kujenga kituo kipya cha polisi Muganza baada ya kile cha awali kuchomwa moto na wananchi wenye hasira kali 2023.

Hata hivyo ameahidi kuwasiliana na mkuu wa polisi mkoa wa Geita ili kusaidia nguvu za wananchi hao ikiwa ni pamoja na kuomba kupelekwa askari polisi kwenye kituo cha polisi nyisanzi kata ya kigongo kilichojengwa kwa nguvu za wananchi zaidi ya miaka 10 iliyopita.

Baadhi ya wananchi waliozungumza na mwandishi wetu, wameiomba serikali kusaidia ukamilishaji wa miundo mbinu ya shule za msingi,sekondari na zahanati kutokana na wao kuonyesha jitihada zao katika uchangiaji wa nguvu zao katika maendeleo ya jamii.

Ziara ya mkuu wa wilaya hiyo imelenga kukagua na kuhimiza usimamizi bora wa miradi ya maendeleo kwa Umma, Sambamba na kuihamasisha jamii kuwapeleka shule watoto wote waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza pamoja na wale wenye umri wa kuanza darasa la kwanza 2025.

     Ujenzi wa kituo cha polisi Muganza ukiendelea


Mwonekano wa vyumba vitatu vya madarasa shule ya sekondari Mkolani Bwongera



No comments