RC KAGERA AWAHIMIZA WATU KUWEKEZA KAGERA
Na Alodia Dominick, Bukoba
MKUU wa mkoa wa Kagera Fatma Mwassa amewataka wanakagera kuwekeza katika mkoa huo na kuwashawishi marafiki zao walioko nje ya mkoa na nje ya Tanzania kuja kuwekeza Kagera ili wainue uchumi wa mkoa wa Kagera.
Mwassa ameyasema hayo Desemba 18, 2024 katika uzinduzi wa sala na dua uliofanyika katika uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba huku viongozi mbalimbali wa madhehebu ya dini ya kikiristo na kiislamu wakiombea wananchi, mkuu wa mkoa, taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.
Maombezi hayo yamepambwa na kwaya kutoka madhehebu mbalimbali ya dini ya kikiristo pamoja na kaswida.
"Uwekezaji mbalimbali ukifanyika Kagera tutainua uchumi wa viwanda vijana wetu watapata ajira, tupate bei nzuri za mazao yetu, tukuze utalii wetu, tukuze mahusiano ya kibiashara baina ya Tanzania na nchi jirani lakini tuendelee kuchechemua uchumi wa nchi yetu na wa mtu mmoja mmoja" amesema Mwassa.
Mwassa amewashukuru viongozi wa madhehebu ya dini Jumuiya ya kikristo Tanzania (TCC), Kanisa Katoliki Tanzania (TEC), SHIA, Baraza kuu la waislamu (BAKWATA), Answar sunna Tanzania (JASUTA) na umoja wa makanisa ya Kipentekoste.
Shekhe Abdushahidu Abbas kiongozi mkuu wa Answar Sunna Tanzania (JASUTA) ambaye ni mmoja wa viongozi walioshiriki katika dua na maombezi hayo amesema kuwa, wananchi wanapaswa kutambua kuwa, utajiri na mafanikio haviwezi kuja kwa njia ya kuua watu na kuwakata viungo watu wenye ualbino bali huja kwa ushirikiano wa pamoja na kumtanguliza Mungu.
Abbas amesema pia wapo wanaodhani kupata nafasi za uongozi ni lazima atumie njia za kishirikina jambo ambalo si kweli bali wanapaswa kumtanguliza Mungu na kumuomba ili aweze kuwajalia kumudu nafasi hiyo.
Makamu wa askofu jimbo Katoliki la Bukoba Padre Samwel Mchunguzi ameliombea taifa la Tanzania na kusema kuwa, iendelee kushika amani na mataifa mengine hasa yale yanayopinga ushoga, usagaji na kubadili jinsia.
Makamu wa askofu jimbo Katoliki la Bukoba padre Samwel Mchunguzi mmoja wa viongozi wa dini walioshiriki dua na maombezi
Amepinga matumizi ya madawa ya kulevya na mambo yote yasiyofaa yanayoaibisha utu wa watu. "Mkoa wa Kagera tunaukabidhi kwa Mwenyezi Mungu Zaburi 127:1 Bwana asipoijenga nyumba waijengao wafanya kazi bure bwana asipoulinda mji waulindao wafanya kazi bure, " amesema Padre Mchunguzi.
Kauli mbiu katika tamasha hilo ni wekeza Kagera irudishe katika ubora wake.
Ikumbukwe kuwa, Mkuu wa mkoa wa Kagera Fatma Mwasa ndiye mwanzilishi wa tamasha la Ijuka Omuka na mwaka huu linafanyika tamasha la pili.
Mwaka jana lilikuwa tamasha la kwanza na uzinduzi rasmi wa tamasha hilo utafanyika kesho na mgeni rasmi ni Naibu Waziri mkuu na Waziri wa Nishati Doto Biteko.
Baadhi ya wananchi walioshiriki katika dua na maombezi
Post a Comment