DKT. MABIMBI : MSIWASHIKESHIKE MIKONO WATOTO NJITI
Na Alodia Dominick, Bukoba
JAMII hapa nchini imetahadharishwa kuacha tabia ya kwenda kuwatembelea watoto ambao wamezaliwa kabla ya wakati (watoto njiti) na kuwashika kwani kufanya hivyo kunaweza kusababisha kuwaambukiza majonjwa mbalimbali.
Tahadhari hiyo imetolewa Desemba 15,2024 na Daktari bingwa wa magonjwa ya watoto katika hospitali ya rufaa ya mkoa, Bukoba Dkt. Mike Mabimbi wakati mkuu wa mkoa wa Kagera Fatma Mwasa alipokuwa amewatembelea watoto mapacha wanne wa mwandishi wa habari wa Televishen ya Azam kutoka Kagera Benson Eustace.
Anayezungumza ni daktari bingwa wa watoto katika hospitali ya rufaa ya mkoa, Bukoba Dkt. Mike MabimbiDkt Mabimbi amesema kuwa, watoto njiti ni watoto waliozaliwa kabla ya wakati hivyo wanaporuhusiwa kutoka hospitali wakawa nyumbani wanahitaji uangalizi wa karibu wa walezi wao na hawahitaji kushikwa shikwa hadi ruhusa ya madaktari vinginevyo wanaweza kuambukizwa magonjwa.
"Tukiwaruhusu kwenda nyumbani ile jamii inaenda kuwaona watoto sisi kama madaktari huwa hatupendi, natoa wito kwa watoto wote ambao wamezaliwa kabla ya muda (njiti) tunapowaruhusu msiwe na tabia ya kwenda kuwashika shika msubili wafikishe uzito unaotakiwa ndipo tunaruhusu wachangamane na watu wengine" amesema Dkt Mabimbi.
Akizungumzia watoto wa mwandishi wa habari Benson Eustace amesema walizaliwa mapacha wanne wa kike wawili na wa kiume wawili na bado wako hospitali wako chini ya uangalizi wa madaktari na wanaendelea vizuri.
Mkuu wa mkoa wa Kagera Fatma Mwasa wa kwanza kulia akimkabidhi vitu mbalimbali Benson Eustace kwa ajili ya watoto wake mapacha wanneAmesema watoto hao walizaliwa na uzito kati ya kilo moja na nusu hadi kilo moja nukta nane na kwa Tanzania uzito wa kawaida mtoto anapozaliwa anapaswa kuanzia uzito wa kilo mbili na nusu kwenda juu.
"Mtoto anapozaliwa uzito unapungua na ndani ya wiki moja unaanza kuongezeka, kwa hiyo hawa watoto mapacha wameanza kuongezeka na wameongezeka uzito kati ya gram 20 hadi 30" amesema Dkt Mabimbi
Aidha ameeleza kwamba, mtoto anapozaliwa kabla ya muda (njiti) madaktari wanaangalia vitu vitatu ambavyo ni joto wanahakikisha anakuwa na joto linalotakiwa, usafi na unyoyeshaji au chakula.
Naye Afisa lishe wa hospitali Victoria Ngatunga amesema kuwa wanashauri mama anayenyonyesha ale zaidi ya mara tano kwa siku na vyakula anavyopaswa kutumia zaidi ni vile vyenye vimiminika kwa ajili ya kusaidia uzalishaji wa maziwa kwa wingi na viwe ni vyakula vilivyobalansiwa, matunda, wanga, ptorini, mafuta na vitamini.
Amesema, vyakula vingine ambavyo ni mbegu za mafuta kama karanga, korosho mbegu za maboga, ufuta vinapaswa kuongezwa kwenye kimiminika kwa hiyo uji utakuwa ni chakula muhimu kwa mama lakini vyakula vyenye asili ya uchachu kama limau ni vyema vikawekwa kwenye supu, pilipili manga inaongezwa kwenye uji au chakula chochote kinachofaa.
Mkuu wa mkoa wa Kagera Fatma Mwasa akiwa hospitali ya rufaa ya mkoa, Bukoba amempa pongezi baba wa watoto wanne Benson Eustace kwa kujaliwa zawadi ya mapacha hao na kutoa zawadi mbalimbali kwa watoto hao ambazo ni makopo ya maziwa, nguo, pampasi, chandarua, magodoro na blanketi za kubebea watoto (Babyshow).
Mkuu wa mkoa wa Kagera Fatma Mwasa wa kwanza kulia akikabidhi vitu mbalimbali kwa Benson Eustace kwa ajili ya watoto wake mapacha wanne"Pamoja na mchango wa serikali ambao huwa inatoa lakini tunatambua kupokea watoto wanne kwa wakati mmoja inaweza kuwa mtihani kwa familia kwamba kipato kilichopo na ugeni uliokufikia inaweza ikawa changamoto kuhudumia na haswa kwa kuwa mama ameugua muda mrefu na akalazimika kupelekwa Bugando.
"Kwa hiyo tunatambua fedha nyingi za familia zimetumika hivyo sisi tukasema ni busara tuje tukushike mkono kama serikali baba wa watoto ili kuweza kutoa msaada kidogo ikiwa ni ishara ya kufurahia ujio wa watoto hawa wanne wa kike wawili na wakiume wawili" amesema Mwasa.
Mwasa amesema alipokwenda kuangalia watoto wodini amekuta watoto zaidi ya ishirini waliozaliwa kabla ya muda na kuwa serikali imekuwa ikijitahidi kuhakikisha kwamba wanapata matunzo mazuri, uangalizi mzuri pamoja na kuwapatia maziwa.
Amewapongeza madaktari pamoja na wauguzi kwa huduma nzuri ya kangaroo wanayowapa watoto njiti kwani wana afya njema na uzito wao unaongezeka.
Baba wa mapacha wanne Benson Eustace anayeripotia Televishen ya Azam Kagera amesema, baada ya mke wake kujifungua mapacha hao alipata changamoto ya kuumwa na kukimbizwa hospitalini ya rufaa Bugando ambapo alikuwa anapatiwa matibabu ameruhusiwa na atarudi hospitali baada ya wiki moja.
Eustace ameshukuru madaktari na wauguzi kwa huduma nzuri aliyopatiwa mke wake katika hospitali ya rufaa ya mkoa, Bukoba tangu anahudhuria kliniki na hadi anajifungua mapacha hao na hadi sasa wanapoendelea kuhudumiwa hospitalini hapo.
Aidha ameishukuru jamii inayomzunguka, marafiki, ndugu, jamaa, viongozi wa serikali na wanataaluma wenzake kwa sapoti waliyompatia kwa kipindi cha wiki mbili toka watoto wamezaliwa.
Ikumbukwe kuwa Novemba 28,2024 familia ya Benson Eustace ilipata bahati ya watoto mapacha wanne ambao ni Ethan Benson, Aivan Benson, Bestina Benson pamoja na Bella Benson.
Post a Comment