HEADER AD

HEADER AD

HATIMAYE VIROBA VYA DHAHABU VILIVYOSOTA MIEZI MITATU BILA KUUZWA BUTIAMA VYAUZWA

 

>> Ni baada ya mkuu wa mkoa wa Mara Kanali Mtambi kuingilia kati

>> Wachimbaji wampongeza RC Mara kwa kufanya maamuzi ya busara na hekima 

>>RC Mara aliwapa wachimbaji mwanasheria wa serikali awasaidie kutengeneza mikataba baina yao na mwenye leseni John Gimunta 

>> Awali DIMA Online iliibua mgogoro wa wachimbaji Butiama

Na Dinna Maningo, Butiama

HATIMAYE zaidi ya Viroba elfu kumi vya mawe yanayodhaniwa kuwa na dhahabu vya wachimbaji wadogo wa dhahabu, kikundi cha Peace Gold Mine  vilivyosota zaidi ya miezi mitatu bila kuuzwa baada ya kuibuka mgogoro wa kimaslahi baina yao na mchimbaji John Gimunta, vimeuzwa na serikali kupata mapato.

Ni baada ya mkuu wa mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi kuingilia kati mgogoro wa kikundi cha Peace Gold Mine na mchimbaji John Gimunta katika Kijiji cha Tarani, Kata ya Mirwa katika wilaya ya Butiama mkoani Mara .

    Mkuu wa mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi

RC Evans hivi karibuni mwezi Novemba, 2024 aliwakutanisha wachimbaji wa madini wilayani humo wakiwemo kikundi cha Peace Gold Mine, John Gimunta, kikundi cha Irasanilo katika ofisi yake mkoani Mara, ambapo aliweza kusikiliza malalamiko yao , kikao kilichokuwa na mvutano baina ya wachimbaji hao na mmiliki mwenye leseni John Gimunta ambaye ni Mwenyekiti wa kikundi na mwanzilishi wa kikundi cha Tarani Mining Group.

Wampongeza RC kuingilia kati mzozo

Wachimbaji wa madini ya dhahabu akiwemo Mchimbaji John Onaka, mkazi wa Kijiji cha Magunga wilayani Butiama, wamemshukuru na kumpongeza mkuu wa mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi kwa kuingilia mgogoro wa wachimbaji kikundi cha Peace Gold Mine na kuutatua, na hivyo kuweza kuuza viroba vinavyodhaniwa kuwa na dhahabu na serikali kupata kodi.

       Mkuu wa mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi akizungumza na wachimbaji wa madini ya Dhahabu kutoka wilaya ya Butiama

Pia wamekishukuru chombo cha habari cha DIMA Online kilichoibua mgogoro huo baada ya kufika kijijini na kubaini kutouzwa kwa viroba zaidi ya 10,000 na serikali kukosa mapato huku uchumi wa wachimbaji na wakazi wa wilaya hiyo, wanaojiingizia kipato kupitia shughuli za uchimbaji ikiyumba kutokana na kuwepo mzozo baina yao na mchimbaji John Gimunta.

" Tumeuza kutokana na ushauri uliotukuka kutoka kwa mkuu wa mkoa wa Mara , alionesha busara zake akatukutanisha wachimbaji wote , mwenye leseni, kikundi cha Irasanilo ,kikundi cha Peace na akatoa maelekezo ya mauzo ya hivyo viroba vilivyosota bila kuuzwa. Tumeuza kwa uhuru bila malalamiko bila kusuguana ,serikali imesimamia haki tukauza na kila mmoja akapata chake na hata sasa hivi tunaendelea kufanya kazi kwa utulivu.

" Katika viroba hivyo vilivyosota miezi mitatu bila kuuzwa Gimunta hakupata asilimia yoyote , tulilipa asilimia zilizoelekezwa na mkuu wa mkoa tu ambazo ni asilimia 0.07 za mrahaba na tozo ya huduma asilimia 0.03 .

" Viroba tunavyoendelea kuzalisha kwa sasa tutamlipa Gimunta asilimia 15 ya uzalishaji kama mmiliki wa leseni kama tulivyokubalina kwa mkuu wa mkoa hatopata asilimia 30 kama alivyotaka mwanzo, atakuwa anapata asilimia 15 tu kwa kila mwenye duara,  na serikali itachukua mapato yake, inayobaki anachukua mwenye duara na watu wake"amesema John.

Mchimbaji huyo amesema kikao cha RC Mara kimeleta matumaini kwao " Kimeleta matumaini, binafsi sijasikia vurugu ya aina yoyote na kazi tunafanya kwa utaratibu na tunaendelea vizuri, hatujapata changamoto yoyote ambayo imeleta malalamiko . Wasimamizi wa Gimunta wanachukua asilimia zao 15 baada ya tozo ya serikali kinachobaki tunagawana sisi wenye maduara.

" Awali Gimunta alitaka apewe asilimia 30 ya viroba vya mawe yanayodhaniwa kuwa na dhahabu, wenye maduara waliona nikama ananufaika yeye wakati amepata leseni eneo ambalo alikuta watu wakilichimba na wanalipa kodi serikalini na tozo nyingine walikuwa wakilipa Irasanilo na wengine walilipa Byagunga" amesema John.

Ameongeza kusema " Wengi wameridhika na maamuzi yaliyotolewa na mkuu wa mkoa kwenye kikao, japo wapo baadhi wameng'ang'ania Peace Mine ndio ipewe leseni ya kumiliki hilo eneo na si Gimunta aliyepewa leseni kwenye eneo linalochimbwa na wachimbaji wa kikundi cha Peace ambao walikuwa kwenye mchakato wa kuomba leseni lakini akawazunguka na kuchukua leseni .

" Tunampongeza Mwandishi wa DIMA Online alifika kijijini akaandika changamoto za wachimbaji na kupitia habari zake serikali ikasikia kilio chetu. Mkuu wa mkoa akatukutanisha na kutusikiliza na akatoa maamuzi na maelekezo ambayo yamesaidia tumeweza kuuza viroba bila bughudha yoyote" amesema John.

Mwenyekiti wa kikundi cha Peace Gold Mine, Rhobi Mwita Amesema anamshukuru mkuu wa mkoa wa Mara kukaa na wachimbaji kuwasikiliza kero zao na kufanya maamuzi ambayo yamewezesha wao kuuza viroba vyao vya mawe ya dhahabu bila kutozwa asilimia 30 aliyoitaka mwenye leseni.

       Mwenyekiti wa kikundi cha Peace Gold Mine, Rhobi Mwita

" Tunashukuru sana RC , kikao chake kilisaidia sana kwasababu kilipunguza ile mihemko ambayo watu walikuwa nayo na mawazo ambayo watu walikuwa wamejiwekea kichwani. Mkuu wa mkoa alitumia sana hekima kutukutanisha na Gimunta na tulimaliza salama , wachimbaji wameuza viroba vyao vya dhahabu bila kutozwa asilimia, wamelipa tu tozo ya serikali " amesema Mwenyekiti wa Peace.

Aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa mgodi wa dhahabu wa Irasanilo unaomilikiwa na wachimbaji wadogo ambaye pia ni mwanakikundi cha Peace Gold Mine, Deogratius Marwa amesema" Tunashukuru RC amesaidia kwa kiasi chake, watu wameuza viroba vyao lakini alimwagiza afisa Madini mkoa wa Mara, kuhakikisha anatafuta eneo lingine la uchimbaji kukipatia kikundi cha Peace, tunasubiri utekelezaji wa agizo la RC. 

" Japo bado kuna baadhi ya wanakikundi  wanaona hawajatendewa haki wanaendelea na msimamo wao kwamba kikundi cha Peace ndio wanatakiwa kupewa leseni na si kikundi cha Talani. Ila wengi wameamua kusikiliza ushauri wa RC ." amesema Deogratius.

Mwanasheria akumbushwa mikataba 

Mchimbaji Ester Machuche Magige ameshukuru kwa mgogoro huo kumalizwa huku akiomba maelekezo yaliyotolewa na RC Mara yatekelezwe, ikiwemo kumwagiza mwanasheria wa serikali , Kitia Turuka kukaa na wachimbaji wenye mashimo (maduara) na mwenye leseni kutengeneza mikataba ambayo itanufaisha pande zote.

      Mchimbaji Ester Machuche Magige

"Changamoto iliyopo ni kutopata mikataba kama alivyoelekeza RC. Tulitengeneza mikataba yetu, kisha Mwanasheria alikuja akaichukua na kwenda nayo ili ikafanyiwe kazi baada ya hapo atuletee ili tuione tujiridhishe kwamba tuliyokubalina ndiyo hayo yaliyomo au wamebadilisha? lakini hadi sasa hatujarudishiwa mikataba.

"Wasipotuletea mikataba yetu kama tulivyokubalina hatutauza viroba tutakavyozalisha hadi pale tutakapoletewa mikataba yetu maana huyu Gimunta ni kigeugeu sana" amesema Ester.

Novemba, 04, 2024 , chombo hiki cha habari cha DIMA Online kilifika  Kijiji cha Tarani kukutana na wachimbaji ili kufahamu sababu za shughuli za uchimbaji kusimama na viroba zaidi ya 10,0000 kusota bila kuuzwa jambo lililosababisha serikali kukosa mapato.

Katika habari iliyoripotiwa November, 8, 2024  yenye kichwa cha habari ' Mgogoro kati ya Peace Gold Mine Butiama na John Gimunta waikosesha mapato Serikali. Wachimbaji wenye mashimo 27 (maduara ) ya uchimbaji katika mgodi wa dhahabu wa wachimbaji wadogo uliopo Kijiji cha Tarani, walieleza sababu za kutouza viroba vya dhahabu. Ili kupata undani wake soma habari ya Novemba, 8, 2024 na Novemba, 9, 2024 na Novemba, 10, 2024.

       Mchimbaji akishuka kuingia ndani ya shimo 

Kufuatia mgogoro huo wa wachimbaji,  Novemba, 5, 2024 na Novemba, 12, 2024 ,Mkuu wa mkoa wa Mara Kanali Evans Matambi akakutana na wachimbaji kikundi cha Peace Gold Mine, John Gimunta Mwenyekiti wa kikundi cha Tarana Mining Group , Kikundi cha Irasanilo Gold Mine katika ofisi yake mkoani Mara na kusikiliza malalamiko yao, kikao  kilichokuwa na mvutano baina ya wachimbaji hao na mmiliki wa leseni John Gimunta na hatimaye RC kutoa maelekezo na maagizo.

Serikali ya Mara ilitoa maelekezo mbalimbali ikiwemo ya wachimbaji kumpatia Mwenye leseni John Gimunta asilimia 15 badala ya asilimia 30 aliyotaka mwenye leseni,  alimwagiza Afisa Madini mkazi mkoa wa Mara, Mhandisi Amin Msuya kuhakikisha anakitafutia kikundi cha Peace Gold Mine eneo lingine la uchimbaji.

Mkuu huyo wa mkoa alimtaka Mwanasheria wa serikali, Kitia Turuka ahakikishe amekaa na wachimbaji kuwasaidia kutengeneza mikataba baina yao na mwenye leseni, Katiba ya kikundi cha Irasanilo Gold Mine ipitiwe upya kupitia wataalam na kikundi kisha wampatie katiba hiyo aipitie ambapo mkuu huyo alijitolea kuwa mlezi wa kikundi cha Irasanilo Gold Mine kama ilivyoripotiwa katika chombo hiki cha habari , Novemba, 13, 2024.

No comments