HEADER AD

HEADER AD

SHAIRI : KUACHA UKEKETAJI, HESHIMA KWA WASICHANA

ACHENI ukeketaji, wape watoto elimu, 

Hilo liwe ni hitaji, ambalo kwetu muhimu, 

Afya kwetu ni mtaji, huo ni ubinadamu, 

Kuacha ukeketaji, heshima kwa wasichana. 

Ni maisha ya heshima, mwana kupata elimu, 

Walakini ni tuhuma, mwili wake kudhulumu, 

Wabaki wanalalama, kwa maisha ya kudumu, 

Kuacha ukeketaji, heshima kwa wasichana. 

Waziri wetu Gwajima, kasema jambo muhimu, 

Kukeketa huko noma, watoto wape elimu, 

Mila hiyo si salama, kuelewa ni muhimu, 

Kuacha ukeketaji, heshima kwa wasichana. 

Hakika ya usalama, kwa wasichana idumu, 

Wala kusiwe dhuluma, afya zao kugharimu,

Hiyo ni yao heshima, kwa afya waweze dumu,

Kuacha ukeketaji, heshima kwa wasichana.

Kuupinga ukatili, kijinsia ni muhimu,

Hii iwe ni asili, yetu sote wanadamu,

Kwa wengine kuwajali, bila ya kuwadhulumu,

Kuacha ukeketaji, heshima kwa wasichana.

Huko mkoani Mara, ukeketaji haramu,

Kote kupingwa ni bora, kwa kupata ufahamu,

Kuyaepusha madhara, ambayo twayafahamu,

Kuacha ukeketaji, heshima kwa wasichana.

Katibu Tawala wetu, kasema jambo muhimu,

Kwa hizi juhudi zetu, za kusambaza elimu,

Ukatili kati yetu, unapungua kwa zamu,

Kuacha ukeketaji, heshima kwa wasichana.

Mara ilikuwa juu, vitendo hivi haramu,

Kwa sasa haiko juu, inavyoshuka kwa zamu,

Ni elimu iko juu, hasa muda wa msimu,

Kuacha ukeketaji, heshima kwa wasichana.

Madhara mengi kiafya, kwao hao yanadumu,

Wala si kupiga chafya, kutokwa sana na damu,

Na uzazi waogofya, wapitia hali ngumu,

Kuacha ukeketaji, heshima kwa wasichana.

Hii mila kandamizi, siyo vema ikadumu,

Watu waelezwe wazi, kuitenda wasidumu,

Watoto pia wazazi, madhara wayafahamu,

Kuacha ukeketaji, heshima kwa wasichana.

Mtunzi ni Lwaga Mwambande (KiMPAB)

lwagha@gmail.com 0767223602

No comments