WAZIRI GWAJIMA ATAKA MIDAHALO, MAKONGAMANO YA KUPINGA UKATILI YAFANYIKE VIJIJINI
>>Lengo wananchi wapate fursa ya kuuliza maswali
>> Asisitiza elimu iendelee kutolewa
Na Dinna Maningo, Tarime
WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na wenye mahitaji maalumu, Dkt. Doroth Gwajima ameyataka mashirika, taasisi na wadau mbalimbali kupeleka elimu vijijini ikiwemo midahalo na makongamano kwakuwa kufanya hivyo jamii itaweza kuuliza maswali yanayohusu masuala ya ukeketaji.
Ameyasema hayo wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia, yaliyofanyika Nyamongo- Tarime na kuwashirikisha watu mbalimbali wakiwemo viongozi wa serikali ya mkoa wa Mara, wilaya ya Tarime, askari wa jeshi la Polisi kutoka mikoa mbalimbali nchini, mashirika yasiyo ya kiserikali, viongozi wa dini na wananchi.
Waziri wa maendeleo ya jamii, jinsia, wanawake na wenye mahitaji maalumu, Dkt. Doroth Gwajima akiburudika na viongozi, wadau wa kupinga ukatili wa kijinsia
Waziri Dorothy amesema endapo makongamano na midahalo yakifanyika na jamii ikapewa nafasi ya kuuliza maswali na yakajibiwa itasaidia watu kuweza kibadilika kwani maeneo ya mijini yamebadilika ikilinganishwa na vijijini.
" Naupongeza mgodi wa Barrick North Mara kwa kunialika niwapongeze pia mashirika , Taasisi wanaopinga vitendo vya ukatili kwa kutoa elimu. Tuelimishane kama ndugu sisi kwa sisi , najua inahitaji muda kuweza kuyafikia mabadiliko na kuyamiliki, kwasababu tusipoyamiliki watayafanya kwa kufichaficha.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Kewanja akisalimiana na Waziri wa maendeleo ya jamii, jinsia, wanawake na wenye mahitaji maalumu, Dkt. Doroth Gwajima aliyejifunga kitambaa kichwani, kulia ni Meneja mkuu wa mgodi wa Barrick North Mara, Apolinary Lyambiko wakati akipokea hundi ya serikali ya Kijiji.
"Uwepo wa shule nyingi za kata umesaidia sana. Naomba kuwepo nyongeza ya makongamano, midahalo mbalimbali huko vijijini ili ile jamii iweze kuzungumza na sisi , iweze kutuuliza maswali na tukatoa mifano watabadilika" amesema Dkt. Dorothy.
Ameongeza kusema " Mwakani tukijaliwa tutakuja Tarime tukae tuwaulize tuanzie kijiji gani hadi kijiji gani, tukae tupeleke huko elimu . Kiwango cha ukeketaji kinaongezeka sehemu za vijijini ikilinganishwa na mijini, tuwaelimishe wenzetu watabadilika " amesema.
Waziri huyo ameupongeza mkoa wa Mara kwa juhudi za kupunguza vitendo vya ukatili wa kijinsia ambao umetoka nafasi ya kwanza hadi nafasi ya tatu huku akiipongeza serikali ya mkoa huo, mashirika, viongozi wa dini, wazee wa mila na jamii kwa ujumla kwa ushirikiano ambao umesaidia kupunguza vitendo vya ukatili.
"Tafiti za kitaifa za idadi ya watu na afya za mwaka 2022 kiwango cha ukatili wa kijinsia kimepungua kwa asilimia mbili , na kwa upande wa baadhi ya maeneo mkoa wa Arusha unaongoza kwa asilimia 43, Myanyara asilimia 43 na Mara ni mkoa wa tatu ukiwa na asilimia 28.
" Singida ni asilimia 20, Tanga asilimia 19 na Dodoma asilimia 18. Asilimia 8.3 wenye umri kati ya miaka 15-49 wamekeketwa ikilinganishwa na asilimia 10 ya mwaka 2016" amesema Dkt. Dorothy.
Ameongeza kuwa serikali itaendelea kushirikiana na mashirika mbalimbali na wadau kuhakikisha jamii inaendelea kupata elimu na kuimarisha utekelezaji wa sheria zinazopiga marufuku ukeketaji.
Waziri wa maendeleo ya jamii, jinsia, wanawake na wenye mahitaji maalumu, Dkt. Doroth Gwajima akisalimiana na Wazee wa Mila koo 12 ya jamii ya kabila la Wakurya wilayani Tarime.
" Sheria hizo tuzitunge tuwapeleke wananchi wakae wao wenyewe watoe maoni vifungu gani vinaweza kumaliza tatizo. Nafurahi kuwaona wazee wa kimila wa koo 12 . Ukiuliza wanasema kuna koo 12 , haya hizi hapa ziko hapa zinatupa ushirikiano, twende tukajiulize sisi tunakwama wapi mbona wanatupa ushirikiano? ".
Katibu Tawala wa mkoa wa Mara, Erasto Kusaya ameiomba jamii yote ya mkoa wa Mara kuungana na kuitumia siku ya uhuru kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia huku akiwahakikishia wananchi kwamba viongozi wote wa mkoa watakuwa bega kwa bega na wananchi wa mkoa huo kuhakikisha ukatili unatokomezwa.
" Tuko tayari kumlinda mtoto wa kitanzania kwa gharama zozote . Ni imani yangu tukitoka hapa tutakuwa sehemu ya walimu kwenda kufundisha wenzetu yale tutakayoyapata.
" Naamini ukatili Mara utapungua na baadae kutokomeza, kikubwa nj ushirikiano na kutoa elimu kwa jamii ili kila mmoja aweze kufahamu madhara yanayotokana na ukatili wa kijinsia ndani ya jamii yetu. Nia ya serikali ni kuhakikisha tunatokomeza vitendo vyote vya ukatili wa kijinsia" amesema Erasto.
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Polisi Tarime Rorya, SACP Mark Njera amesema mkoa huo wa polisi umefanya kampeni maalum ya kutoa elimu kwa jamii juu ya ukatili wa kijinsia iliyolenga kuyafikia makundi yote yaliyo hatarini kufanyiwa ukatili wa kijinsia.
Askari wa Jeshi la Polisi kutoka mikoa mbalimbali nchini wakiwa kwenye maandamano ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia Nyamongo.
" Kampeni hii hadi sasa imewanufaisha zaidi ya wanafunzi wa shule za sekondari 34000, shule za msingi 41000 na watu wazima wasiopungua 102000 katika kata zote 60 za mkoa wa polisi Tarime Rorya." amesema RPC Mark.
Ameongeza kuwa jumla ya makosa 1099 yameriporiwa mwaka 2024 ikilinganishwa na makosa 1163 yaliyoripotiwa kipindi cha 2023, ikiwa ni pungufu ya makosa 64 sawa na asilimia 5.8.
Msanii kutoka Jeshi la Polisi mkoa wa Simiyu mwenye kipaza sauti akiimba wakati wa maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia
" Makosa ya shambulio la aibu, kujeruhi, kutishia kuua, ukeketaji na kutekeleza familia yameriportwa kwa kiasi kikubwa mwaka huu ikilinganishwa na mwaka Jana. Hii inachangiwa na wananchi kupata uelewa na kutosha juu ya makosa ya ukatili wa kijinsia na unyanyasaji hivyo kupata makosa hayo kwa wingi kwenye vituo vya polisi" amesema.
Amezitaja changamoto zinazozikumba Jeshi hilo katika kukabiliana na ukatili wa kijinsia kuwa ni pamoja na kutowepo kwa sheria yenye meno inayoweza kushughulikia kosa la ukeketaji.
" Kwasababu sheri inayotumika kuwaadhibu wakosaji wa kosa la ukeketaji ni kifungu cha 168 A cha kanuni ya adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022 ambacho kinataja ukeketaji kuwa ni ukatili dhidhi ya mtoto na kutoa adhabu ya kifungo kisichopungua miaka mitano na kisichozidi miaka 15 au faini ya Tsh. Milioni moja au vyote.
" Kifungu hiki cha sheria hakitoshi kushughulikia kosa hilo na adhabu inayotolewa ni ndogo mno kwa mtu anayemsababishia binadamu ulemavu wa kudumu kwa makusudi" amesema .
Amesema changamoto nyingine ni baadhi ya Asasi zinazoshughulikia ukatili wa kijinsia hasa ukeketaji kuwekeza nguvu kubwa katika kutangaza tatizo badala ya kutafuta njia ya pamoja katika kutatua changamoto ya ukeketaji.
Pia wananchi kuendelea kukumbatia mila na desturi zinazokinzana na sheria ikiwa ni pamoja na kufanya suluhu ya makosa ya jinai hasa ya ukatili pamoja na mmomonyoko wa maadili unaotokana na kukosekana kwa maelezo sahihi kwa watoto.
Meneja mkuu wa mgodi wa Barrick North Mara, Apolinary Lyambiko amesema mgodi huo ulianza mwaka 2002 ni mdau mkubwa wa maendeleo na katika masuala ya jinsia.
Meneja mkuu wa mgodi wa Barrick North Mara, Apolinary Lyambiko kushoto) , Waziri wa maendeleo ya jamii, jinsia, wanawake na wenye mahitaji maalumu, Dkt. Doroth Gwajima mwenye kitambaa kichwani, wakikabidhi hundi kwa kiongozi wa serikali ya Kijiji.
Amesema kuwa mgodi umeweza kuajiri wafanyakazi wa kampuni mama ya Barrick wapatao 3613 , kati ya hao wanawake ni 461 sawa na asilimia 12.8.
" Tumeboresha mazingira ya wanawake kuweza kutumia haki zao za uzazi, mafunzo ya uzazi , lakini pia kuna jengo maalum kwa ajili ya wanawake waliojifungua lengi ni kuondoa changamoto kwa wanawake" amesema Apolinary.
Ameongeza kuwa mgodi umetekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ya afya, maji, elimu , miundombinu ambayo imesaidia kukuza usawa wa kijinsia na kwamba tangu mwaka 2020 hadi sasa mgodi wa North Mara umewekeza katika miradi 253 yenye jumla ya Tsh. Bilioni 22.
Meneja mkuu wa mgodi wa Barrick North Mara, Apolinary Lyambiko akizungumza
Post a Comment