HEADER AD

HEADER AD

RC SIMIYU ASISITIZA ELIMU NA ULINZI WA HAKI KWA WANAFUNZI

Na Samwel Mwanga, Simiyu

MKUU wa Mkoa wa Simiyu, Kenani Kihongosi, ametoa wito  kwa wadau wa elimu kuhakikisha wanalinda haki za wanafunzi na  mazingira yao ya elimu yanakuwa ni salama.

Akizungumza Januari 25 mwaka huu wakati wa uzinduzi wa wiki ya sheria iliyofanyika mjini Bariadi amewahimiza walimu na wadau hao kuwa macho dhidi ya vitendo vya ukatili,unyanyasaji wa kijinsia na changamoto nyingine zinazoweza kuwazuia wanafunzi kufikia ndoto zao.

           Mkuu wa mkoa wa Simiyu,Kenani Kihongosi akizungumza siku ya uzinduzi wa Wiki ya Sheria mkoa huo mjini Bariadi.

Amesema kuwa ni muhimu sana kuhakikisha hakuna mwanafunzi wa kike anayekatiza masomo kwa sababu yoyote ile ikiwemo kuolewa katika umri mdogo na kupewa mimba katika mazingira ya shule. 

“Kila mdau wa elimu katika mkoa huu wa Simiyu kuwa jicho la serikali katika usimamizi wa wanafunzi katika ngazi zote ili kulinda haki zao ili waweze kupata elimu.”

“Toeni taarifa kwa vyombo husika pale panapojitokeza matukio yasiyo ya kawaida kwa wanafunzi ili hatua stahiki za kisheria zichukuliwe, walimu hakikisheni kuwa hakuna mwanafunzi anayekatisha masomo kwa sababu ya ndoa za utotoni au ujauzito,”amesema.

Amesema kuwa hili ni jukumu linalohitaji ushirikiano wa kila mmoja ili kuhakikisha elimu inakuwa haki inayopatikana kwa kila mtoto bila kikwazo chochote.

Naye Caroline Kiliwa ambaye ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama ya wilaya ya Bariadi amesema kuwa utawala wa sheria ni msingi wa maendeleo endelevu hivyo taasisi za haki madai zinahakikisha kwamba sheria zinatekelezwa kwa usawa bila upendeleo kwa watu wote.

   Hakimu mkazi mfawidhi , mahakama ya wilaya ya Bariadi Caroline Kiliwa akizungumza siku ya uzinduzi wa Wiki ya Sheria mkoa wa Simiyu.

Kwandu Ndambo ni mwanafunzi wa shule ya sekondari Bariadi anasema kuwa ili kutokomeza ukatili wa kijinsia katika jamii ni vizuri watu wote wanaofanya ukatili huo wanachukuliwa hatua za kisheria na kupatiwa adhabu stahiki.

“Ukatili wa kijinsia haukubaliki katika jamii huu ni wakati kwa serikali kusimamia sheria zilizopo na kuhakikisha watu wote wanaofanya ukatili wa kijinsia katika jamii wanafikishwa katika vyombo vya sheria na kupatiwa adhabu kali kwa mujibu wa sheria,”amesema.

Amesema pia serikali, asasi za kiraia, na taasisi za elimu zinapaswa kushirikiana kutoa elimu ya kijinsia kupitia shule, vyombo vya habari, na mikutano ya kijamii hii litasaidia kupunguza ukatili wa kijinsia na kujenga jamii yenye usawa na haki.

Naye Amos Mashimba ambaye ni mwanafunzi wa shule ya sekondari ya Bariadi anasema kuwa elimu ya kijinsia ni nyenzo muhimu katika kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia.

            Baadhi ya wanafunzi wa shule ya sekondari Bariadi walioshiriki uzinduzi wa wiki ya sheria mkoa wa Simiyu.

“Kwa kutoa elimu hii ya kijinsia kwa jamii, watu wataweza kuelewa masuala ya kijinsia, haki za binadamu  na umuhimu wa kuheshimiana,”amesema.

Pia amesema kuwa ni vizuri kuhamasisha mawasiliano na ulinzi wa watoto kwa wazazi na walezi kujifunza namna ya kuwasiliana na watoto wao kuhusu masuala ya kijinsia ili kuwapa uelewa wa kujilinda dhidi ya unyanyasaji.


         Mkuu wa mkoa wa Simiyu,Kenani Kihongosi(aliyekati mwenye kofia nyeupe)akiongoza maandamano ya uzinduzi wa Wiki ya sheria mkoa wa Simiyu.

     Askari wa jeshi la polisi mkoa wa Simiyu wakiwa kwenye maandamano mjini Bariadi wakati wa uzinduzi wa wiki ya sheria.

No comments