HEADER AD

HEADER AD

SERIKALI KUIMARISHA USHIRIKIANO NA BENK YA CRDB

Na Daniel Limbe, Chato

SERIKALI wilayani Chato mkoani Geita imesema itaendelea kuimarisha ushirikiano na taasisi mbalimbali za kifedha ili kuchochea ustawi na maendeleo ya wananchi huku ikiipongeza benki ya CRDB kwa kusaidia jamii.

Akizungumza katika hafla ya kukabidhi madawati 40 yenye thamani ya Tsh. Milioni 3,280,000 yaliyotolewa na Benk hiyo kwenye shule ya msingi Mkuyuni, Mkuu wa wilaya ya Chato, Louis Bura, amesema msaada huo umepatikana kipindi muafaka kutokana na idadi kubwa ya wanafunzi waliosajiliwa kuanza darasa la awali na la kwanza mwaka huu.

        Kulia ni mkuu wa wilaya ya Chato,Louis Bura,akisalimiana  na mwalimu mkuu wa shule ya msingi Mkuyuni.

Amesema msaada huo utawasaidia watoto kukaa kwenye madawati na kuinua taaluma na kwamba ipo haja kwa taasisi zingine kuguswa na changamoto wa uhaba wa madawati kwenye shule za msingi na sekondari.

Aidha ameiomba benki hiyo,kuendelea kushirikiana na taasisi zingine ikiwemo wakala wa huduma za misitu nchini (TFS) wilaya ya Chato kusaidia kutatua uhaba wa madawati zaidi ya 20,000 ambayo yanahitajika katika wilaya hiyo.

Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Verena Nicholaus,amesema shule hiyo inakabiliwa na uhaba wa madawati 213 na kwamba baadhi ya wanafunzi wanalazimika kukaa chini hali inayosababisha kutofanya vizuri katika masomo yao.

Aidha ameipongeza benki ya CRDB tawi la Chato kwa kuguswa na kadhia hiyo,ambapo amesema upatikanaji wa madawati hayo utasaidia kuondoa adha iliyopo sasa ambayo imekuwa ikisababisha wanafunzi kushindwa kujiamini kutokana na uchafu wa mavazi.  

Meneja wa CRDB Kanda ya magharibi, Jumanne Wambura amesema msaada huo ni mwendelezo wa kusaidia jamii kutoka aslimia moja ya faida inayopatikana katiba benki hiyo.

      Meneja wa CRDB Kanda ya magharibi, Jumanne Wambura,akizungumza na wananchi,walimu pamoja na wanafunzi

"Msaada huu unatokana na aslimia moja ya faida tunayoipata kwa mwaka,hivyo niwasihi wazazi, walezi pamoja na walimu muendelee kutumia huduma za kifedha kutoka benki ya CRDB ili tuweze kusaidia zaidi ya hapa"amesema.

Ameahidi kutatua changamoto ya uhaba wa madawati kwenye wilaya hiyo kwa kushirikiana na taasisi nyingine kutokana na maombi yaliyowasilishwa na ofisi ya mkuu wa wilaya hiyo.

Mwakilishi wa mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Gerald Ndikumana, mbali na kuipongeza benki hiyo amesema wilaya hiyo bado inakabiliwa na upungufu wa madawati zaidi ya 20,000 .




"Jitihada mbalimbali zinahitajika ili kuondoa adha hiyo kutokana na ongezeko la watoto wanaoandikishwa kila mwaka kuanza darasa la awali na la kwanza" amesema.

Amesema shule ya msing mkuyuni ina jumla ya wanafunzi 1,683 huku darasa la awali na la kwanza likiwa limesajili watoto zaidi ya 460 katika mhula wa masomo 2025.



                        

No comments