SHAIRI : ANGUKA ILA USIBAKI CHINI
KUANGUKA si tatizo, hata ukifika chini,
Ni sawa sawa na nguzo, iliyokuwa angani,
Lazima vuta uwezo, kuirudisha mbinguni,
Kuanguka we anguka, ila usibaki chini.
Inuka jishikilie, sio kwako hapo chini,
Usikae utulie, unachelewa kazini,
Jinyanyue jiambie, siyo pako hapo chini.
Kuanguka we anguka, ila usibaki chini.
Wewe nguzo ya umeme, juu kwa juu safarini,
Nyaya chini ni kiwewe, ni hatari duniani,
Ziwe juu kwenye mwewe, kote ibaki amani,
Kuanguka we anguka, ila usibaki chini.
Watu wengi huanguka, wanapokuwa njiani,
Hawabaki wakadeka, kusalia pale chini,
Hutafuta cha kushika, kuinuka toka chini,
Kuanguka we anguka, ila usibaki chini.
Tena unapoanguka, iingie akilini,
Sababu ya kuanguka, isirudie njiani,
Dalili ukizinyaka, unakwepea pembeni,
Kuanguka we anguka, ila usibaki chini.
Kuanguka si habari, igusayo sikioni,
Kuinuka ni habari, sote tunaitamani,
Wachungulia kaburi, unarudi ahueni,
Kuanguka we anguka, ila usibaki chini.
Maisha ni kuinuka, hata kuanguka chini,
Hatubaki kubweteka, kuloa chozi shavuni,
Hung’ang’ana kuinuka, kupambana duniani,
Kuanguka we anguka, ila usibaki chini.
Biashara uloshika, mtaji u mavumbini,
Jipigepige inuka, uingie mzigoni,
Ya jana hayatanuka, kesho ndio i njiani,
Kuanguka we anguka, ila usibaki chini.
Wengi wanaosikika, walishuka hadi chini,
Wababe waliwachoka, wakasogea pembeni,
Hao walichangamka, hawakusalia chini,
Kuanguka we anguka, ila usibaki chini.
Bill Gate asikika, tajiri wa duniani,
Shuleni hakutukuka, kama wale kilingeni,
Sasa wasomi ateka, kawaajiri kazini,
Kuanguka we anguka, ila usibaki chini.
Shairi limetungwa na Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602
Post a Comment