MASWA YAPANDA MITI 2,700 KUKABILIANA NA MABADILIKO YA TABIANCHI
Na Samwel Mwanga, Maswa
MITI 2,700 imepandwa katika shule ya sekondari Bukigi katika kata ya Malampaka, wilaya ya Maswa kwa lengo la kuboresha mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kama ukame na ongezeko la joto.
Zoezi la upandaji wa miti hiyo limefanyika Januari 27 mwaka huu na kuongozwa na Mkuu wa wilaya ya Maswa, Aswege Kaminyoge katika eneo la shule hiyo mpya ya sekondari.
Mkuu wa wilaya ya Maswa,Aswege Kaminyoge akizungumza na wananchi mara baada ya zoezi la upandaji wa miti katika eneo la shule ya sekondari Bukigi.
Amesema kuwa wilaya hiyo imeamua kupanda miti katika eneo hilo ikiwa ni uzinduzi wa upandaji wa miti milioni moja na laki tano katika wilaya hiyo kwa mwaka huu.
Akizungumza na wananchi waliojitokeza katika zoezi hilo amesema ni mwendelezo wa agizo la serikali lililotolewa na Rais Dkt. Samia Suluhu la kuzitaka wilaya zote hapa nchini kupanda idadi hiyo ya miti.
Amesema kuwa wilaya hiyo imeanza utekelezaji wa agizo kwa kupanda miti katika eneo hilo huku akisisitiza taasisi na watu binafsi kupanda miti ambayo inatolewa na Wakala wa Misitu nchini (TFS) , halmashauri ya wilaya pamoja na mashirika yasiyo ya kiserikali.
Baadhi ya wanafunzi wa shule ya sekondari Malampaka walioshiriki zoezi la upandaji wa miti katika shule ya sekondari Bukiigi wilaya ya Maswa.
“Leo ni sehemu ya utekelezaji wa maagizo ya Rais Dkt. Samia Suluhu ya kuhakikisha wananchi wote, taasisi mbalimbali wanapanda miti kila mwaka ili kuhakiikisha miti milioni moja na laki tano inapandwa hasa kipindi hiki cha masika,”amesema.
Muhifadhi wa wakala wa huduma za misitu nchini(TFS) wilaya ya Maswa, Fabian Mosha, ameeleza umuhimu wa kuitunza miti kwa kumwagilia maji, kuzuia uharibifu wa mifugo na kupunguza matawi kwa kiwango kinachofaa ili kuepuka kuathiri ukuaji wa miti.
Mhifadhi wa TFS wilaya ya Maswa,Fabian Mosha akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) juu ya zoezi la upandaji wa miti wilayani humo.
Wakala wa huduma za misitu nchini(TFS) imeotesha na kugawa bure miche zaidi ya 200,000 kwa wilaya nzima.
Mwenyekiti wa kijiji cha Bukigi,Chingila Jilala, ameahidi usimamizi thabiti wa miti hiyo na kuendelea kupanda mingine katika taasisi, watu binafsi na eneo lililotengwa na kijiji hicho kwa ajili ya upandaji wa miti ili kufikia malengo yaliyowekwa na wilaya hiyo.
Mwenyekiti wa kijiji cha Bukigi wilaya ya Maswa,Chingila Kilala akizungumza jinsi watakavyoitunza miti iliyopanda katika shule ya sekondari Bukigi.
Naye Afisa Mazingira, halmashauri ya wilaya ya Maswa, Duttu Kafulla amesema kuwa suala la upandaji wa miti ni moja ya vipaumbele vya halmashauri hiyo ambapo shule za msingi,sekondari,zahanati na vituo vya afya wilayani humo, kila mwaka zimekuwa zikipanda miti nyakati za masika.
Amos Mishamo ni mwanafunzi wa shule ya sekondari Malampaka, ameeleza mafanikio ya upandaji miti ikiwa ni pamoja na utunzaji wa mazingira kwa ajili ya kizazi cha sasa na kijacho.
“Hatua hizi za upandaji wa miti ni muhimu kwa kushirikiana katika kulinda mazingira kwa ajili ya kizazi cha sasa na kijacho,”amesema.
Pepetua Joseph mkazi wa kijiji cha Bukigi, akisisitiza elimu kwa jamii kuhusu kutunza mazingira na kupanda miti kama njia ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi.
“Jamii inapaswa kupatiwa elimu ya mazingira, hususan juu ya utunzaji wa mazingira,mmomonyoko wa ardhi na uchafuzi wa mazingira ili kuweza kupambana na mabadiliko ya tabianchi,”amesema.
Post a Comment