ALIYEKUWA DC MASWA AMKABIDHI OFISI DC NAANO
Na ,Samwel Mwanga, Maswa
ALIYEKUWA Mkuu wa wilaya ya Maswa mkoani Simiyu,Aswege Kaminyoge ambaye amehamishiwa katika wilaya ya Bunda mkoa wa Mara amemkabidhi ofisi,Dkt Vicent Naano Anney aliyekuwa Mkuu wa wilaya ya Bunda.
Hafla fupi ya makabidhiano hayo imefanyika leo februari 25,2025 katika ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Maswa na kushuhudiwa na Katibu Tawala wa wilaya hiyo,Athuman Kalaghe pamoja na wajumbe wa kamati ya ulinzi ya usalama.
Wengine walioshuhudia ni pamoja na Wakuu wa taasisi mbalimbali za serikali pamoja na waandishi wa habari.
Kabla ya makabidhiano, Kaminyoge amemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kumuamini na kumhamisha kituo cha kazi wadhifa huo.
“Leo namaliza miaka minne na miezi saba nikiwa Mkuu wa wilaya ya Maswa.namshukuru mwenyezi Mungu pia Rais kwa kuniamini na sasa imempendeza kunihamishia katika wilaya ya Bunda na Dkt. Vicent Naano kuhamishiwa wilaya ya Maswa,”amesema.
Amesema kuwa kwa kipindi ambacho ameongoza wilaya hiyo serikali imetoa zaidi ya Tsh. Bilioni 78 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ambapo katika halmashauri ya wilaya imepokea Tsh Bilioni 42.2, Mamlaka ya Maji Maswa na Usafi wa Mazingira(Mauwasa)Tsh Bilioni 5.5 na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira vijijini(Ruwasa) Tsh 7.3 .
Aliyekuwa Mkuu wa wilaya ya Maswa, Aswege Kaminyoge (kulia)akimkabidhi Ofisi Mkuu wa wilaya ya Maswa, Dkt Vicent Naano Anney (kushoto) aliyekuwa Mkuu wa wilaya ya Bunda,mkoa wa Mara.
Wakala ya Barabara za Mjini na Vijijini(Tarura)ilipata Tsh Bilion 9.6 na shirika la ugavi wa umeme nchini(Tanesco) Tsh Bilioni 10 .
“Fedha zote hizo nilizozitaja katika kipindi chote hicho zimekamilisha miradi na imeanza kutoa huduma na miradi mingine inaendelea kumaliziwa, tunaamini kwa kuwa umekuja miradi yote ifikapo juni 30,2025 itakuwa imekamilika kama alivyotoa maagizo waziri Mkuu,”amesema.
Pia amewaomba wananchi wa wilaya hiyo kumpatia ushirikiano Dkt. Naano kama walivyompatia yeye wakati akitekeleza majukumu yake.
Naye Dkt. Naano amesema kuwa Rais, Dkt. Samia ameonyesha imani kwake kwa kuendelea kumuamini na kutumikia wadhifa huo alionaona na kuhahidi kuendelea kusimamia shughuli za maendeleo katika wilaya hiyo.
“Ninaamini nitapata ushirikiano wa kutosha kwa watumishi wote wa serikali katika wilaya ya Maswa,mie ni msimamizi wa shughuli za maendeleo nina imani yangu kila mmoja atakeleza majukumu yake na iwapo unapata changamoto ni vizuri kutoa taarifa ili kutozua taharuki kwa wananchi wa wilaya yetu,”amesema.
Amesema kuwa huu ni mwaka wa uchaguzi hivyo atahakikisha ahadi zote zilizotolewa na serikali ya awamu ya sita katika kutekeleza miradi ya maendeleo kwa wananchi inakamilika katika wilaya hiyo.
Rais Dkt Samia Suluhu Hassan Februari 21,2025 alifanya uhamisho wa wakuu hao wa wilaya kwa mujibu wa taarifa zilizoripotiwa kwenye vyombo vya habari iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi,Balozi Dkt Moses Kusiluka.
Picha ya pamoja mara baada ya makabidhiano ya ofisi kati ya aliyekuwa Mkuu wa wilaya ya Maswa,Aswege Kaminyoge na Dkt Vicent Naano aliyekuwa Mkuu wa wilaya ya Bunda(sasa Mkuu wa wilaya ya Maswa)
Post a Comment