HEADER AD

HEADER AD

FISI 16 WAUAWA SIMIYU


>> Ni kutokana na kukithiri matukio ya fisi kushambulia na kuua watu 

Na Samwel Mwanga, Simiyu

OPERESHENI maalum ya kudhibiti fisi wakali na waharibifu mkoani Simiyu imewezesha fisi wapatao 16 wauawa ili kurejesha usalama na utulivu kwa wananchi.

Hayo yameelezwa jana februari 19, 2025 na Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Kenani Kihongosi alipokuwa akiongea na waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari ofisini kwake.

Amesema kuwa hatua hiyo imechukuliwa na serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii baada ya matukio kadhaa ya fisi kushambulia na kuua watu katika wilaya za Itilima na Maswa mkoani humo.

Amesema kufuatia changamoto hiyo, serikali ilichukua jukumu kubwa la kuhakikisha inalinda wananchi wake ikiwemo kuanzisha oparesheni hiyo mwezi januari,25 mwaka huu iliyohusisha Jeshi la Uhifadhi kwa taasisi za  Mamlaka za Usimamizi wa Wanyama Pori Tanzania(TAWA), Mamlaka za Hifadhi za  Taifa (TANAPA)na Wakala wa Misitu(TFS), kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi pamoja na wananchi.

“Kama mtakumbuka mwezi Desemba 20,2024  baada ya fisi kuvamia makazi ya watu na kusababisha vifo vya watoto, serikali ilichukua hatua kubwa ya kushirikisha vyombo vyake TAWA na Jeshi la Polisi na kuanza oparesheni.

" Ilipofika mwezi januari 25, 2025 oparesheni ya mkoa mzima ilifanyika kwa ukubwa, kuhakikisha inakabiliana na fisi wote waliokuwa wanasumbua wananchi"

“Na kwa taarifa njema ni kwamba tangu kuanza kwa oparesheni hii, vyombo vyetu vimeweza kudhibiti na kuua fisi 16 na ndio maana kwa sasa mnaweza kuona hali imetulia" amesema.

Kihongosi ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama mkoa huo, amewatoa hofu wananchi na akisisitiza kuwa hali ni shwari na kuwataka waendelee na shughuli zao kama kawaida.

Amekemea vikali imani za kishirikina kuhusiana na mnyamapori aina ya fisi kwa baadhi ya wakazi wa mkoa wa Simiyu na kuwataka wote wanaofuga wanyamapori hao kuacha mara moja kwani ni kosa kisheria kumiliki nyara za serikali bila kibali.

Afisa Habari wa TAWA, Beatus Maganja amewaomba wananchi wa mkoa huo hususani wilaya ya Itilima kuacha tabia ya kutembea  nyakati za usiku na alfajiri kwani ni nyakati ambazo wanyama fisi huwa katika mawindo yao.

Pia amewasisitiza wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa maofisa wa Jeshi la Uhifadhi waliopo uwandani humo ili kuongeza ufanisi wa zoezi hilo huku akiwahakikishia kuwa serikali imedhamiria kulinda wananchi wake na kwamba askari wapo uwandani wanafanya kazi usiku na mchana kuwahakikishia usalama wao.

Nao baadhi ya wananchi wa mkoa huo wameishukuru kwa juhudi zinazofanywa naserikali katika kukabiliana na changamoto hiyo kwani  imeweza kuwarejeshea matumaini, utulivu na amani.

"Kwa kweli tulikuwa tunasumbuliwa sana na hawa fisi ambao walikuwa wanauwa watu hasa watoto, baada ya serikali kusikia ikaweka ulinzi, kwakweli imetufanyia vizuri sana mpaka leo hatujawasikia tena matukio ya namna hiyo,”amesema Mozo Mabula  mkazi wa mijiji cha Mwamunhu wilaya ya Itilima.

Naye Baya Shinhu mkazi wa kijiji cha Ilalambasa amesema kuwa ni muhimu kwa serikali kuweka mikakati ya kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu ili kulinda maisha ya watu na mali zao.

Jumla ya watu 9 wameuawa mkoani humo kwa kushambuliwa na wanyama hao wakiwemo watoto watatu katika wilaya za Itilima na Maswa kwa mwezi Novemba 2024 hadi Januari 2025.


No comments