MFUGAJI WA NG'OMBE KIJIJI CHA MRITO ACHINJWA
>>Imedaiwa kabla ya kuuawa ilionekana gari nyeusi yenye vioo vyeusi ikimfuatilia
>> Mauaji yahusishwa na fitina, visasi
>>Matukio ya watu kujichukulia sheria mkononi yawatia hofu wananchi Nyamongo
Na Dinna Maningo, Tarime
HOFU imetanda katika mji wa Nyamongo, wilaya ya Tarime, mkoani Mara kufuatia kuibuka matukio ya watu kujichukulia sheria mkononi na kufanya mauaji.
Wananchi Nyamongo wameiomba serikali kuingilia kati kuchukua hatua za haraka kuwabaini watu wote waliohusika kujichukulia sheria mkononi na kufanya matukio ya kuua watu ili kukomesha vitendo vya uhalifu.
Wakizungumza na DIMA Online, kwa nyakati tofauti, Mwenyekiti wa Kijiji cha Mrito, Joseph Manga amesema kuwa siku ya jumanne , Februari, 18, 2025 saa moja usiku mfugaji wa ng'ombe, Marwa Masiaga mwenye umri wa miaka 70 mkazi wa Kitongoji cha Miliminsi akiwa nyumbani kwake aliuawa kwa kuchinjwa kwa mapanga na watu ambao hawajafahamika.
"Tukio hili limenisikitisha sana , limetokea siku ya jumanne saa moja usiku . Mimi na OCCID Nyamwaga tulifika nyumbani kwa marehemu, tulimwita mwenyekiti wa Kitongoji, tukafanya mahojiano na wanafamilia, mchungaji wa ng'ombe na majirani .
" Mke wa marehemu amesema mmewe alikuwa nje ya geti akitoa ndama waliokuwa zizini ambalo lipo nje ya uzio wa nyumba, wakati anazitoa ili kuziingiza ndani ya nyumba ndipo alivamiwa.
"Amesema alisikia mmewe akipiga yowe alipofika nje ya geti aliona mtu mmoja akikimbia akiwa amevaa shati nyeupe huku mmewe akiwa kalala chini. Alimwita binti yake akaleta tochi, walivyomulika wakakuta tayari mmewe kaishakata roho" amesema Mwenyekiti wa kijiji.
Mwenyekiti huyo wa Kijiji ameongeza " Walimchinja kama kuku wakamkata koromeo, wakamkata kichwani ,ukiangalia walivyomkata nikama walitokea kwa nyuma yake na kumfanyia ukatili huo.
" Marehemu alikuwa anakunywa soda kwenye baa moja ya senta hapa Mrito, yeye si mlevi ,alipoondoka na kufika nyumbani watu wasiofahamika walimvamia na kumchinja, tukio lilifanyika kwa muda mfupi.
" Wapo wananchi wamesema kabla ya Marehemu kuuawa kuna gari nyeusi yenye vioo vyeusi ilikuwa imepaki barabarani jirani karibu na nyumbani kwake maana mji wa marehemu upo jirani na barabara mita 100 " amesema Joseph.
Mwenyekiti huyo wa kijiji amesema kwamba kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi wanaendelea na uchunguzi ili kuwabaini waliohusika na mauaji.
Mkazi wa Kijiji cha Mrito ambaye hakutaka jina litajwe amesema " Marehemu alikuwa senta ya Mabera, kuna gari nyeusi yenye vioo vyeusi aina ya Succeed iliyokuwa imetokea barabara ya Kerende - Murito ilikuwa imepaki senta na hakuna mtu aliyeshuka ndani ya gari hilo.
" Baada ya Marehemu kuondoka mida ya saa moja kasoro gari hilo lilimfuata kwa nyuma hadi karibu na nyumbani kwa marehemu likapaki baadae likaondoka ,hatukujua chochote kwahiyo hatukulifuatilia tulijua ni mtu ana mambo yake.
" Tunadhani ile gari ndo ilikuwa imebeba watu waliokuja kumuua Marwa maana baada ya kufika karibu na nyumba ya marehemu ilisimama kisha muda mfupi ikaondoka, ilipoondoka zilipita dakika 25 au 30 tukasikia kilio nyumbani kwa marehemu" amesema.
Mwananchi mwingine ameongeza kusema "Yawezekana kifo chake kimetokana na kisasi au alikuwa na ugomvi na mtu, maana hata marehemu na familia yake walikuwa hawana mahusiano mazuri, walikuwa hawaelewani , hawapendani maana mme ana wake zaidi ya watano na ni tajiri wa ng'ombe ana mifugo mingi hivyo kulikuwa kukitokea kutoelewana ndani ya familia yake" amesema .
Mwananchi mwingine amesema" Marehemu alikuwa na vyesi vyesi na kuna kesi moja alishinda ambayo mahakama ilitoa hukumu kwamba marehemu alipwe Tsh. Milioni 200 , sasa yawezekana hilo likachangia yeye kuuawa maana mtu aambiwe alipe milioni 200 na huwenda hana hizo pesa za kumlipa unategemea nini" amesema.
Mwenyekiti mstaafu Kijiji cha Murito, Joseph Mangure amesema mbali na tukio hilo pia mwezi Januari, 2024 kijana wa marehemu aliuawa kwa kukatwakatwa mapanga.
" Marwa Masiaga ni tajiri wa ng'ombe ana ng'ombe zaidi ya 300, mida ya mchana alikuwa senta akinywa soda kwenye Bar. Mida ya saa moja kasoro tano hivi aliondoka na pikipiki yake akaenda nyumbani alipofika baada ya dakika 30 tulisikia yowe . Inasemekana waliomvamia walikuwa watu wanne.
" Matukio ya watu kujichukulia sheria mkononi yamezidi sana Nyamongo. Mwezi wa kumi mwaka jana kijana wa marehemu aliuawa kwa kukatwa mapanga huko Kijiji jirani cha Nyansurura wilaya ya Serengeti. Inasemekana kaka wa marehemu alikuwa na uhasama na watu wa kule Bukira -Serengeti kwamba alimuua mtu huko na wale wakawa wanamfuatilia kaka yake.
" Baada ya kuona kaka yake hatokezi haendi huko Masurura ndipo wakadili na mdogo wake ambaye alikuwa anaenda huko. Siku moja akiwa anakunywa pombe wakati anarudi nyumbani akavamiwa njiani na kukatwakatwa mapanga akafa. Tunaomba serikali iingilie kati kukomesha watu wanaojichukulia sheria mkononi" amesema Joseph.
Wiki mbili zilizopita katika Kijiji cha Kewanja- Nyamongo ,kulitokea mauaji ya mwanaume mmoja ambaye mwili wake ulikutwa umetupwa karibu na nyumbani kwake Kitongoji cha Kegonche akiwa amechomwa kisu na utumbo kutoka nje.
Imeelezwa kwamba huwenda tukio hilo linahusishwa na visasi, ama wivu wa kimapenzi pamoja na imani za kishirikiana.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Kewanja Joshua Chacha (Chia) amesema hadi sasa hakuna aliyebainika kuhusika na mauaji na kwamba kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi wanaendelea na uchunguzi kubaini waliohusika na tukio hilo.
" Musa aliuawa na watu ambao hawajafahamika kisha wakaupeleka mwili wake nyumbani kwake Kegonche. Nilitoa taarifa polisi ,wanaendelea na uchunguzi. Hakutolewa figo kama watu wanavyodhani , mwili ulichekiwa alikuwa na viungo vyote. Alichomwa kisu tumboni ,utumbo ukatoka nje wakadhani ametolewa viungo vya ndani.
" Huwenda ni visasi maana sio kwamba ni mtu mwenye uwezo wa kimaisha kwamba ana pesa hapana ni mtu wa maisha ya kawaida" amesema Mwenyekiti.
Post a Comment