HEADER AD

HEADER AD

RAS PWANI AWATAKA WATAALAM WA SHERIA KUWASAIDIA WANANCHI WENYE HALI DUNI

Na Gustaphu Haule, Pwani


KATIBU Tawala wa mkoa wa Pwani ambaye pia ni Skauti Mkuu wa Tanzania Rashid Mchatta amewataka wataalam wa masuala ya sheria waliopo mkoani Pwani kujikita katika kuwasaidia Wananchi wenye hali duni ambao hawana uwezo wa kusimamia kesi zao pindi zinapofika Mahakamani.

Mchatta ametoa wito huo Februari 23 ,2025 mjini Kibaha wakati akifungua mafunzo kwa wataalam kwa ajili ya utekelezaji wa kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia (Mama Samia Legal Aid Campaign) unaosimamiwa na Wizara ya Katiba na Sheria.

         Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani ambaye pia ni Skauti Mkuu wa Tanzania Rashid Mchatta akifungua mafunzo ya wataalam wa kisheria wanaokwenda kutoa huduma katika kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia itakayoanza kutekelezwa Mkoa wa Pwani Februari 25 hadi Machi 9 mwaka huu.

Amesema kuwa wapo wananchi wengi wanaokabiliwa na kesi mbalimbali lakini wanashindwa kupata haki zao kutokana na kukosa uelewa wa masuala ya Kisheria na hata hali duni za kimaisha.

Mchatta amesema kuwa kutokana na kuwepo kwa changamoto hiyo katika jamii serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan imeona ianzishe kampeni maalum ya kuwasaidia Wananchi inayoitwa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia, ( Mama Samia Legal Aid Campaign).

Amesema kuwa,kampeni hiyo ilizinduliwa Februari 27, 2023 mjini Dodoma na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa lakini kwa mkoa wa Pwani inazinduliwa Februari 24,2025 na itaanza kufanyakazi Februari 25, 2025 hadi Machi 5 mwaka huu ikiwa ni muda wa siku tisa.

       Wataalam wa masuala ya kisheria wakiwa katika mafunzo maalum kwa ajili ya utekelezaji wa kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia,(Mama Samia Legal Aid Campaign) yaliyofanyika Februari 23,2025  Mjini Kibaha

Mchatta ameongeza katika kuelekea kwenye utekelezaji wa kampeni hiyo Serikali imeona itumie fursa hiyo kuwapa mafunzo wataalam wa kisheria ambao watakwenda kusimamia na kutekeleza mpango huo katika maeneo yao.

Mchatta amesema kuwa mkoa wa Pwani ni mkoa ambao umekuwa na changamoto nyingi hususani migogoro ya ardhi, mirathi na ndoa kwahiyo kupitia kampeni hiyo itakuwa sehemu ya kufungua fursa ya utatuzi wa migogoro kwa wananchi.

"Natarajia kuona baada ya kampeni hii ,ninyi wataalam wa masuala ya kisheria mnaendelea kuwa mstari wa mbele katika kuwasaidia wananchi ambao mara nyingi wamekuwa wakikosa na kupoteza haki zao kutokana na kukosa uelewa wa kisheria,"amesema Mchatta.

Ametoa wito kwa wataalam hao kufanyakazi kwa ueledi katika kuratibu zoezi hilo vizuri ikiwa pamoja na kuhakikisha wanawafuata Wananchi katika maeneo ya mikusanyiko ikiwemo sokoni ili kuwasaidia katika masuala yote ya kisheria.

      Mmoja wa wataalam wa masuala ya kisheria Simon Lendita akizungumza katika mafunzo hayo Februari 23 Mjini Kibaha

"Wataalam wa kisheria mnapewa mafunzo haya leo lakini napenda kuona mnawasaidia Wananchi na Jamii kiujumla na ikiwezekana changamoto zao zinakuja na majibu sahihi na zile ambazo mnaona ni kubwa basi mnazichukua na kuzipeleka juu kwa ajili ya kuzifanyiakazi," ameongeza Mchatta .

Katika hatua nyingine amemshukuru Rais wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuruhusu kampeni ya msaada wa kisheria ibebe jina lake pamoja na Wizara ya Katiba na Sheria kwa kubeba jukumu hilo na  kushirikisha Mkoa wa Pwani katika utekelezaji wake.

Mkurugenzi wa Huduma za Kisheria kutoka Wizara ya Katiba na sheria Anjellah Anatory, amesema kuwa serikali inatekeleza kampeni ya huduma za kisheria Tanzania Bara na Visiwani ambapo mpaka sasa tayari wamemaliza Mikoa 19 na Mkoa wa Pwani ni mkoa wa 20.

       Mkurugenzi wa Huduma za Kisheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria Anjellah Anatory, akizungumza katika mafunzo ya wataalam kwa ajili ya utekelezaji wa kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia yaliyofanyika Februari 23,2025 Mjini Kibaha Pwani.

Amesema kuwa wananchi wengi wamekuwa na uhitaji wa msaada wa kisheria kutokana na changamoto wanazopitia ambapo lengo la kampeni hiyo ni kutoa elimu lakini pale kwenye matatizo wanatoa ufumbuzi na yale ambayo yanakuwa magumu wanasheria wanayachukua na kwenda kuyafanyiakazi.

Amesema kuwa kwa mkoa wa Pwani mafunzo hayo yamewakutanisha wataalam mbalimbali wa kisheria kutoka katika halmashauri zote za mkoa wa Pwani wakiwa 45 wakiwemo wanasheria wa Halmashauri,maafisa msaada wa kisheria ,polisi,wanasheria mbalimbali,maafisa ustawi wa jamii na makundi mengine muhimu ya kisheria.

Hata hivyo baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo akiwemo Simon Lendita Mwanasheria kutoka Wilaya ya mafia na Yasmin makanya kutoka halmashauri ya Kibaha Vijijini wameeleza umuhimu wa mafunzo hayo huku wakisema wanakwenda kuyatumia mafunzo hayo katika kuwasaidia wananchi katika maeneo yao.


Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani na Skauti Mkuu wa Tanzania Rashid Mchatta aliyeketi mbele  (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wataalam wa masuala ya kisheria walioshiriki mafunzo kwa ajili ya utekelezaji wa kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia.

No comments