HEADER AD

HEADER AD

WAZALISHAJI WA BIDHAA VIWANDANI WATAKIWA KUZINGATIA UBORA

Na Samwel Mwanga, Simiyu

NAIBU Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe ametoa wito kwa wazalishaji wa bidhaa mbalimbali za viwandani hapa nchini kuzingatia ubora ili ziweze kushindana katika soko.

Hayo yameelezwa Februari 23, 2025 alipotembelea kiwanda cha kutengeneza Chaki kilichoko wilaya ya Maswa mkoani hapa na kujionea uzalishaji wa bidhaa hiyo kiwandani hapo.

Waziri Kigahe amefurahishwa na shughuli zinazofanywa na kiwanda hicho kinachomilikiwa na halmashauri ya wilaya hiyo na kusema kuwa ni kiwanda kikubwa ambacho serikali imeamua kuwekeza kwa gharama ya Tsh. Bilioni 10.


       Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara,Exaud Kigahe(wa pili kulia mwenye kofia nyeupe) akiangalia maboksi ya chaki zilizozalishwa katika kiwanda cha Chaki cha Maswa.

“Bilioni 10 zimewekezwa katika kiwanda hiki ili uwekezaji uwe na tija ni vizuri kuzalisha bidhaa zenye ubora ambazo zitashindana na bidhaa nyingine kwenye soko la nje.

“Shirika la viwango nchini (TBS) wasaidieni halmashauri ya wilaya ya Maswa ambao ndiyo wamiliki wa kiwanda hiki kuhakikisha wanazalisha bidhaa bora,”amesema.

Amesema kuwa dhamira ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania sio kufanya biashara bali kuendelea kuweka mazingira rafiki na wezeshi kwa wawekezaji na wafanyabiashara ndani na nje ya nchi na ndiyo maana halmashauri ya wilaya hii imeamua kuanzisha  kampuni ya Nghami Industries Company Ltd ili iweze kusimamia kiwanda.

‘Serikali yetu haifanyi biashara ila lengo lake ni kuweka mazingira rafiki na wezeshi kwa wawekezaji na wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi,ila tukipata miradi ya kujenga viwanda kama hiki cha Maswa ni lazima serikali ianzishe kampuni tanzu kwa ajili ya kukiendesha kibishara kama hii kampuni ya Nghami Industries Company Ltd,”amesema.

Pia amewataka wafanyakazi wa kiwanda hicho kuwa mstari wa mbele katika kukisemea vyema pamoja na kufanya kazi kwa bidii ili kujenga ufanisi lakini wakati huo huo ametaka kuboreshwa kwa vitendea kazi kwa wafanyakazi hao.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo,Maisha Mtipa amesema kuwa kuanzia mwezi Mei 2024 hadi januari 31,2025 uzalishaji wa chaki vipande 2,529,147 vimeweza kutoa katoni 843.05 na katoni 250 zimeuzwa.

    Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Maswa,Maisha Mtipa(wa kwanza kulia)akitoa maelezo ya jinsi kiwanda cha chaki kinavyofanya kazi kwa Naibu Waziri,Viwanda na biashara,Exaud Kighae(aliye kati).

Amesema kuwa mapato baada ya kutoa gharama za uendeshaji yanatarajia kufikia Tsh. Bilioni 16.3 kwa miaka kumi na tano na kwa mwezi ni Sh 3 bilioni.

“Mapato ya kiwanda hiki yatatusaidia kutekeleza miradi yetu ya maendeleo katika halmashauri yetu kupitia mapato ya ndani kwani tulikuwa tukitegemea sana zao la pamba kama ndicho chanzo kikuu cha mapato yetu ya ndani,”amesema.

  Sehemu ya mitambo ya kiwanda cha kutengeneza Chaki kinachomilikiwa na halmashauri ya wilaya ya Maswa.

      Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe (mwenye Kizibao rangi ya njano) akiangalia chaki zilizozalishwa na kiwanda cha Maswa.

No comments