HEADER AD

HEADER AD

RC KAGERA AWANYOSHEA KIDOLE WENYEVITI WANAOWARUHUSU WAHAMIAJI HARAMU KUISHI NCHINI


>> Asema baadhi ya wenyeviti wa vijiji, Vitongoji hupewa pesa na wahamiaji haramu na kuwaruhusu kuishi nchini

>>Wahamiaji haramu zaidi ya 150 hurudishwa nchi kwao

>>Mbunge Rweikiza aomba wahamiaji haramu wadhibitiwe

Na Alodia Dominick, Bukoba

MKUU wa mkoa wa Kagera Fatma Mwassa amesema kila wiki wahamiaji haramu zaidi ya 150 hurudishwa nchini mwao ambapo mkoa huo umepakana na nchi jirani ya Rwanda, Uganda na Burundi.

Takwimu hizo za kurudishwa kwa wahamiaji haramu zimetolewa Februari 19, 2025 na mkuu wa mkoa wa Kagera Fatma Mwassa katika kikao cha maendeleo ya mkoa kilichofanyika ukumbi wa mkuu wa mkoa katika manispaa ya Bukoba.

Mwassa amesema kuwa, baadhi ya viongozi wa vijiji na vitongoji wamekuwa wakipewa fedha kidogo na wahamiaji hao hivyo kuruhusiwa kuingia nchini na kuishi nchini.

        Mkuu wa mkoa wa Kagera Fatma Mwassa akizungumza 

“Namba ya wahamiaji haramu ni kubwa sana na tumeanza utaratibu wa kuwaondoa na kuwarudisha kwenye nchi zao kila wiki tunarudisha zaidi ya wahamiaji 150 kwenye nchi zao.

" Hii namba ni kubwa tunajiletea matatizo makubwa, niwaombe wadau wa kikao hiki mbariki mchakato tunaoendelea nao kwa manufaa ya kizazi kilichopo na kijacho” amesema Mwassa

Ameongeza kuwa, kama mkuu wa mkoa ameishafika eneo inapofugiwa mifugo, lakini ng’ombe walioko humo ni kutoka nchi jirani na kwamba mwanakagera hanufaiki chochote zaidi ya kukimbizwa kimbizwa hawalimi, ardhi waliyoiacha mababu wanaambiwa ni maeneo ya wafugaji.

Mwassa amewataja wanaohusika na kuwakaribisha wahamiaji haramu kuwa ni viongozi wa vitongoji na vijiji. Amewaomba wananchi na makundi mengine kuumunga mkono ili kutokomeza tatizo la wahamiaji haramu na kuongeza kuwa, kuna ukanda ng’ombe  waliopo kwenye vitalu ni kutoka nchi jirani.

Amesema watanzania wanachukua vitalu kwa gharama ya chini wanawakodisha raia kutoka nchi jirani wanaingiza ng’ombe wengi matokeo yake watanzania wanaendelea kukaa na umaskini huku wanaonufaika na vitalu ni raia wa nchi jirani wakati vilitengwa viwasaidie watanzania.

Aidha ameleza kuwa, wanapohitaji kuuza ng'ombe hao huwapeleka nchini mwao bila serikali ya Tanzania kupata kodi.

“Haya yote hayaleti afya kwa uchumi wa nchi, kwa uchumi kwa mwanakagera wala kwa uchumi wa mtu mmoja mmoja labda kwa wale wachache waliokodisha ranchi hizo”

“Madhara ya jambo hili ni pale ambapo walowezi hawa wataishi miaka mingi, watazaa wajukuu, watagombea uongozi katika ngazi mbalimbali na baada ya muda kadhaa watadai haki kama raia wa Tanzania” amesema Mwassa.

Ameongeza kusema " Mifano hiyo inaonekana siyo ya kusimuliwa, yanayoendelea Congo leo ni yale yaliyoanza kama huku kwetu tunavyoyaona na akawaomba kila mmoja asimame kidete kwamba wadhamilie kuzuia uhamiaji haramu ili kulinda mkoa huo lakini pia kulinda nchi ya Tanzania na watu wawe wazalendo.

" Maeneo ya kuingilia ni mengi hatuwezi kusubilia idara ya uhamiaji ndiyo watazuia wahamiaji haramu, kila mmoja awe askari mahili mwadilifu wa uhamiaji katika kulinda usalama wa mipaka ya nchi hii.

Mbunge wa jimbo la Bukoba vijijini Jasson Rweikiza amesema wahamiaji haramu ni lazima wadhibitiwe maana wanapokuja nchini wanafuga, wanajenga nyumba, wanalima lakini wakiwa ni wahalifu.

         Jasson Rweikiza mbunge wa Bukoba vijijini

Rweikiza amesema wahamiaji nchini mwao wanapotoka hawana amani katika nchi zao hivyo wanakimbilia Tanzania katika kisiwa cha amani na bahati mbaya wakija wanakuwa hawana amani wanaleta vurugu wanaua watu.

Aidha mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Karagwe Walles Mashanda ameeleza kuwa licha ya changamoto ya wahamiaji haramu kusababishwa na viongozi wa vijiji na vitongoji lakini pia hata ngazi za juu pia kuna watu wanachangia.

“Tukubali hata ngazi zetu kuna sehemu tunachangia uwepo wa wahamiaji haramu. Mkuu wa mkoa nakuomba tembelea wilaya yoyote yenye changamoto ya wahamiaji labda Ngara, Muleba au Karagwe ukae na wenyeviti wa vijiji na vitongoji na watendaji wa vijiji uwaulize kwa nini tatizo la wahamiaji haramu linaendelea kuwepo.

“ Na sisi kuna sehemu tunachangia kwa kutowapa ushirikiano wa kutosha kesi ziko wazi anakamatwa mhamiaji haramu anapelekwa ofisi za uhamiaji au ofisi yoyote  baada ya wiki mbili anarudi pale kijijini wakati anajulikana kwamba ni muhamiaji” amesema Mashanda.

Aidha amesema jambo hilo liliondoa imani kwa watu na lazima lifanyiwe kazi na hakuna kurudi nyuma hata wananchi wakishirikishwa kama wanaona ni njia ya ukweli watu watasaidia na kutoa ukweli.
 
          Baadhi ya wajumbe waliohudhuria kikao hicho

No comments