HEADER AD

HEADER AD

UWT : WENYEVITI WA MITAA, VIJIJI NA VITONGOJI SIMIYU TENDENI HAKI


>> Chatanda awataka wenyeviti kuhudumia watu bila kujali itikadi za kisiasa

>>Shemsa awataka wenyeviti watambue nafasi walizopewa ni dhamana

Na Samwel Mwanga, Simiyu

MWENYEKITI wa Jumuiya ya Wanawake wa CCM (UWT) Taifa, Mary Chatanda amewataka viongozi wa serikali za mitaa,vijiji na vitongoji mkoani Simiyu kuhudumia wananchi wote kwa usawa, bila kujali itikadi za kisiasa.

Chatanda ameyasema hayo Februari 19, 2025 mjini Bariadi wakati akifungua mafunzo ya wenyeviti hao, wanawake 109 wa mkoa huo yenye lengo la kuwajengea uwezo katika kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

       Mwenyekiti wa UWT Taifa, Mary Chatanda akifungua mafunzo ya wenyeviti wa mitaa,vijiji na vitongoji wa mkoa wa Simiyu katika ukumbi wa Makuti mjini Bariadi.

Mafunzo hayo yameandaliwa na Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS) yamefanyika katika ukumbi wa Makuti.

Amesema kuwa viongozi hao wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa kufuata misingi ya sheria, kanuni, na taratibu, ili kuepuka migogoro na kuhakikisha wanawahudumia wananchi wote bila ubaguzi.

“Mmechaguliwa na wananchi katika maeneo yenu kuwaongoza katika mitaa,vijiji na vitongoji kufuatia uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika mwezi Novemba mwaka 2024.

"Sasa mkafanye kazi ya kuwahudumia wananchi kwa kutenda haki kwa kufuata misingi ya sheria,kanuni na taratibu zilizowekwa na serikali,”amesema.

Amesema kuwa jumuiya hiyo imeona upo umuhimu wa viongozi wanawake kupata mafunzo hayo na huo ni mwendelezo na utaratibu wao wa kawaida kutoa mafunzo kwa viongozi na watendaji ili kuwajengea uelewa wa pamoja kwenye kutekeleza majukumu yao.

         Baadhi ya wenyeviti wa mitaa,vijiji na vitongoji wa mkoa wa Simiyu wakiwa katika mafunzo mjini Bariadi.

“Tumewakutanisha hapa kwa pamoja ili kuwapa nyenzo muhimu kwenye kutekeleza majukumu yenu, kwani lengo la UWT ni kuhakikisha kiongozi mwanamke anatekeleza vema majukumu yake na anakuwa mfano na kimbilio la wananchi’’amesema.

Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Simiyu, Shemsa Mohamed amesema kuwa katika mkoa huo chama hicho kilipata ushindi mkubwa katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliopita na kikashinda kwa  asilimia 98.8 ya mitaa, vijiji, na vitongoji.

         Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Simiyu,Shemsa Mohamed akizungumza wakati wa mafunzo ya viongozi wanawake ambao ni wenyeviti wa mitaa,vijiji na vitongoji wa mkoa huo mjini Bariadi.

“Licha ya CCM kushinda katika uchaguzi wa serikali za mitaa nasisitiza kwamba viongozi mliochaguliwa mnapaswa kuwahudumia wananchi wote kwa usawa, bila kujali tofauti za kisiasa, ili kudumisha umoja na kuleta maendeleo endelevu katika jamii,”amesema.

Amesema viongozi hao wanapaswa kutambua kwamba nafasi walizopewa ni dhamana kutoka kwa wananchi, hivyo wana wajibu wa kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa uwazi.

Penina Nhumo ni mwenyekiti wa kitongoji cha Ichimu wilaya ya Meatu amesema kuwa amechaguliwa lakini alikuwa hajui majukumu yake hivyo kupitia mafunzo hayo yatamjengea uwezo katika kutekeleza majukumu yao.

          Baadhi ya wenyeviti wa mitaa,vijiji na vitongoji wa mkoa wa Simiyu wakiwa katika mafunzo mjini Bariadi.

“Haya ni mafunzo muhimu kwetu yanatujengea uwezo sisi viongozi  wapya tuliochaguliwa mara baada ya uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka jana binafsi nilikuwa siyajui majukumu yangu ila kupitia haya mafunzo nitakwenda kufanya kazi kwa ufanisi,”amesema.

Naye Esther Vicent ambaye ni mwenyekiti wa kitongoji cha Mahakamani wilaya ya Maswa amesema kuwa mafunzo haya yanapaswa kuwa endelevu ili kuendelea kuwajengea uwezo na kujiamini ili waweze kutoa maamuzi katika majukumu yao.

Rehema Meshack ni mwenyekiti wa kijiji cha Mwamanjili wilaya ya Busega amesema kuwa serikali inatakiwa kuweka utaratibu wa kutoa mafunzo haya kwa wenyeviti hao sambamba na kuona umuhimu wa kuwaongeze posho kwa mwezi kwani majukumu yao ni makubwa  katika jamii.

“Pamoja na mafunzo haya tuliyoyapata ni vizuri sasa serikali ione sasa umuhimu wa kutuongeza posho ya mwezi sisi wenyeviti wa vijiji maana Sh 10,000 kwa mwezi haitoshi wakati majukumu yetu ni makubwa,”amesema.

No comments