TRA YAMTUNUKU AFISA MADINI MARA TUZO YA URAHISISHAJI UKUSANYAJI KODI
>> Urahisishaji wa ukusanyaji kodi umeiwezesha ofisi ya Madini Mara kukusanya Mabilioni ya fedha
Na Dinna Maningo, Musoma
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) mkoa wa Mara, imemtunuku tuzo na cheti cha pongezi afisa Madini mkazi, mkoa wa Mara kwa urahisishaji wa ukusanyaji wa kodi katika sekta ya madini.
Mamlaka hiyo ya Mapato Februari, 7,2025 mjini Musoma iliwakutanisha wafanyabiashara na taasisi mbalimbali katika mkoa huo kuwapongeza kwa ulipaji bora wa kodi kwa kipindi cha mwaka 2023 na kuwatunuku tuzo.
Akizungumza na DIMA ONLINE ofisi ya madini mkoa wa Mara, Afisa Madini mkazi, mkoa wa Mara ,Amin Msuya ameipongeza TRA kwa kuipatia ofisi ya madini tuzo na kusema kuwa tuzo hiyo ni ya kwanza kutolewa ofisi ya madini Mara.
Afisa Madini mkazi, mkoa wa Mara ,Amin Msuya aliyetunukiwa tuzo ya urahisishaji wa ukusanyaji wa kodi sekta ya madini mkoa wa Mara.
Akieleza sababu ya kutunukiwa tuzo na cheti cha pongezi amesema " Mfumo thabiti wa ukusanyaji wa maduhuri ya Serikali ikiwemo kodi kutoka kwa wachimbaji umewekwa katika masoko ya madini na kurahisisha wachimbaji hao kutekeleza takwa hilo la kisheria" Amesema Amin.
Akieleza ni kwa namna gani ofisi ya madini mkoa wa Mara imekuwa ikirahisisha ukusanyaji wa kodi amesema " Kwa sasa masoko yetu yanahakikisha mali zote zinazofanyiwa biashara zinachangia mapato ya serikali kwa mujibu wa sheria.
" Kwa upande wa kodi ya TRA mchimbaji akileta dhahabu kuuza katika masoko anafahamu kuwa anapaswa kulipia asilimia 2 ya thamani ya dhahabu yake. Hii ilitokana na maboresho ya sheria ya fedha yaliyofanywa mapema mwanzoni mwa mwaka 2023/2024" amesema Amin.
Amesema katika masoko hayo maafisa mbalimbali wa serikali wamekuwa wakihudumu ili kuendelea kuhakikisha utekelezaji wa sheria unakuwa kwa kiwango cha juu.
Ameeleza kuwa katika mkoa wa Mara pamoja na kuwa na soko kuu Wilayani Musoma lakini pia kuna vituo vya ununuzi mbalimbali katika maeneo ambayo pamekuwa na uchimbaji wa madini.
Amevitaja vituo hivyo vya ununuzi ni pamoja na Tarime, Nyamongo, Serengeti, Butiama na Bunda. Pamoja na vituo hivyo amevitaja pia vituo vidogo (collection centres) vya Kedeli, Kinyambwiga, Suguti na pia kituo kipya kinaanzishwa katika eneo la Ekungu ambapo uchimbaji umekuwa na mwamko mkubwa kwa muda wa hivi karibuni.
Msuya ameeleza kuwa ofisi ya madini mkoa wa Mara imepewa lengo la kukusanya Tsh. Bilioni 176.3 kwa mwaka huu 2024/2025 na mpaka kufikia tarehe 7 Februari tayari wameshafanikiwa kukusanya Tsh. Bilioni 134.7 ambayo ni asilimia 74.7 ya lengo hilo la mwaka.
Ameongeza kuwa elimu ya ufuataji wa sheria katika sekta ya madini imeendelea kutolewa kwa wadau na kuleta uelewa wa kutosha na kufanikisha makusanyo TRA.
Amewahimiza wafanyabiashara kuhakikisha wanafanya biashara kwa kutumia masoko yaliyowekwa ili kuulinda mnyororo wa biashara madini.
Msuya ametoa wito kwa wadau na wafanyabiashara wote wa madini katika mkoa wa Mara kuhakikisha wanafuata sheria, miongozo na kanuni kama ambavyo wanaelekezwa.
Pia amewaasa wafanyabiashara kutumia bei elekezi ambazo zinatolewa na ofisi kila siku na kubandikwa katika mbao za matangazo katika masoko na katika makundi ya mitandao ya kijamii.
Amewapongeza wadau wote wa sekta ya madini mkoani Mara kwa kulipa kodi na kuwaomba waendelee kutoa ushirikiano ili kuendelea kuikuza sekta ya madini.
Cheti cha pongezi kilichotolewa na mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa afisa madini mkazi mkoa wa Mara, Amin Msuya .
Makusanyo ya TRA
Meneja wa mamalaka ya mapato Tanzania, mkoa wa Mara, Nasoro Ndemo akizungumza katika maadhimisho ya siku ya walipa kodi yaliyofanyika Februari , 07 , 2025 mjini Musoma, amesema kuwa mamalaka hiyo katika mkoa wa Mara imekusanya kiasi cha Tsh. Bilioni 142.98 sawa na asilimia 126 ya lengo la Tsh. Bilioni 113.52 walizokuwa wamepangiwa.
Ameongeza kuwa moja ya sababu ya makusanyo hayo kuongezeka ni mazingira mazuri yaliyowekwa na serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu na ushirikiano mzuri kutoka kwa wafanyabiashara umechangia kuvuka lengo .
Naye Naibu Kamishna wa uwekezaji biashara wa mamlaka hiyo , Wahabi Matengo amesema kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2023/2024 , mamlaka hiyo imefanikiwa kukusanya Tsh. Trilioni 28.39.
Makusanyo hayo ni ongezeko la asilimia 14.5 ikilinganishwa na makusanyo ya Trilioni 24 katika mwaka wa fedha 2022/2023 huku akiwapongeza wafanyabiashara kwa ulipaji mzuri wa kodi pamoja pamoja na waliotunukiwa vyeti vya ulipaji bora wa kodi .
Tuzo iliyotolewa na mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa afisa madini mkazi mkoa wa Mara, Amin Msuya.
Post a Comment