HEADER AD

HEADER AD

TRA YAMTUNUKU CHETI MKURUGENZI KAMPUNI YA PKM KWA ULIPAJI BORA WA KODI

>> Kibiba Machage amekuwa mshindi wa kwanza kwa ulipaji bora wa kodi wilaya ya Tarime

>>Alianza na mtaji wa laki moja biashara ya rejareja, akawa dereva wa Daladala, sasa ana miliki makampuni

>> Awashauri vijana kufanya kazi kwa bidii

Na Dinna Maningo , Tarime

MAMLAKA  ya Mapato Tanzania (TRA ) imemkabidhi cheti cha ulipaji bora wa kodi mfanyabiashara Kibiba Machage, ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya PKM inayomiliki vituo vya mafuta (Sheli) , hoteli , duka la vifaa vya ujenzi, nyumba za upangaji mjini Tarime, mkoani Mara.

Kibiba Machage ameibuka kuwa mshindi wa kwanza katika wilaya ya Tarime katika ulipaji bora wa kodi ambapo ameipongeza mamalaka hiyo ya mapato kumtunuku cheti cha pongezi.

"  Tarehe 7, 2025 ,TRA ilinialika Musoma kwenye sherehe ya kuwapongeza walipa kodi . Ikafika zoezi la kutunuku vyeti vya pongezi kwa walipa kodi, nami nikapewa cheti kama mlipa kodi bora wa kwanza katika wilaya ya Tarime.

" Walikuwa wanakabidhi washindi watatu kwa kila wilaya, katika wilaya yetu tumepata watatu mimi, mmoja anaishi Sirari na mwingine Nyamongo.

" Mimi nalipa kodi ni mtanzania ninayeipenda nchi yangu nalipa inavyotakiwa. Ni mara yangu ya tatu napewa tuzo za ulipaji bora . Nina vituo vya mafuta (Sheli) , hoteli, duka la vifaa vya ujenzi , nina sambaza vifaa vya ujenzi mgodini nina nyumba za kupangisha"amesema Kibiba.

Mfanyabiashara huyo amewahimiza baadhi ya wafanyabiashara kutokwepa kulipa kodi kwani ukwepaji kodi unarudisha nyuma maendeleo ya nchi.

         Mfanyabiashara ambaye ni Mkurugenzi wa kampuni ya PKM Kibiba Machage akipokea cheti cha pongezi kwa ulipaji bora wa kodi

" Nawashauri wafanyabiashara wasikwepe kulipa kodi kwasababu nchi haiwezi kujengewa bila watanzania , na bila kulipa kodi . Ili tupate maendeleo , huduma ya maji, afya na kila kitu lazima tulipe kodi. Tusipolipa kodi tunairudisha nyuma nchi yetu.

" Tanzania ni nchi nzuri yenye utaratibu mzuri wa kikodi, hata kama una kiasi cha kodi ulichopata unaenda kwa meneja unakaa nae unamueleza unalipa kwa awamu. Mtu asiogope kulipa kodi, atatozwa mapato kulingana na biashara yake . Wafanyabiashara waombe kukadiliwa kodi walipe kodi" amesema Kibiba.

Baadhi ya wafanyabiashara ukwepa kulipa kodi kwa madai kuwa biashara zao zinawapa hasara badala ya faida. Kibiba amesema mtu akipata hasara hawezi kuendelea na biashara.

" Unapofanya biashara lazima ujue faida yake , nitatoa kiasi fulani cha kodi n.k , kama unaingia hasara usifanye biashara, au nenda umuoneshe meneja wa TRA  ulivyoingia hasara na yeye ataona unafanya kazi ya hasara naye ni binadamu atakupa makadirio kwa kile ulichokipata.

Vijana fanyeni kazi

Kibiba amewashauri vijana kutochagua kazi bali wafanye kazi yoyote kwa bidii ilimradi ni halali watafanikiwa ,kwani hata yeye alianza biashara kwa mtaji wa laki moja duka la rejareja.


" Vijana wasichague kazi, fanya kazi ilimradi ni halali . Maisha hayaji bila kufanya kazi, mtu asikudanganye kuwa kuna sehemu ya kupita makato, sehemu yoyote ile lazima ufanye kazi. Mfanyabiashara yeyote yule aliyefanikiwa ni yule anayefanya kazi , ukibaki unapiga majungu mtaani utabaki hapo hapo .

"Mimi nilianza biashara nikiwa mdogo , nilianza na mtaji wa laki moja nikaanzisha duka la rejareja , baadae nikawa dereva wa gari (Daladala). Nilifanya kazi kwa bidii mwishowe na mimi nikanunua gari langu aina ya Hiace , nikaendelea kuchapa kazi nikaongeza magari mengine.

" Sikukata tamaa leo namiliki kampuni na miradi mingine. Ukianza biashara mfuate aliyekutangulia muulize tunafanyeje , na mtu yeyote anayefanya kazi kwa bidii lazima afanikiwe " amesema Kibiba.

Aipongeza serikali ya awamu ya sita 

Kibiba amesema serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na  Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni nzuri, wafanyabiashara wanaifurahia kwa sababu wanafanya biashara kwa uhuru bila woga.

" Ni awamu ambayo kila mfanyabiashara ukimuona tangu awamu ya sita imeingia wafanyabiashara wanafanya biashara kwa kasi kwasababu kuna fursa nyingi za kufanya biashara, ni wewe mwenyewe utaona ufanye biashara gani hapa Tanzania au nje ya nchi.

" Sio kama zamani mtu ulikuwa unalazimishwa kulipa kodi mara akaunti zako zizuiwe, mara upelekwe mahakamani lakini saizi hayo mambo  hayapo mtu unalipa kodi kwa hiari bila shuruti " amesema Kibiba.

Kibiba Machage ni mfanyabiashara na mwanachama wa chama cha Mapinduzi (CCM) ambaye ujihusisha na mambo ya siasa kipindi tu cha uchaguzi na baada ya hapo uendelee na biashara zake.

Makusanyo  TRA

Meneja wa mamalaka ya mapato Tanzania, mkoa wa Mara, Nasoro Ndemo akizungumza katika maadhimisho hayo ya siku ya walipa kodi amesema kuwa mamalaka hiyo katika mkoa wa Mara imekusanya kiasi cha Tsh. Bilioni 142.98 sawa na asilimia 126 ya lengo la Tsh. Bilioni 113.52 walizokuwa wamepangiwa.

Ameongeza kuwa moja ya sababu ya makusanyo hayo kuongezeka ni mazingira mazuri yaliyowekwa na serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu na ushirikiano mzuri kutoka kwa wafanyabiashara umechangia kuvuka lengo .

Naye Naibu Kamishna wa uwekezaji biashara wa mamlaka hiyo , Wahabi Matengo amesema kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2023/2024 , mamlaka hiyo imefanikiwa kukusanya Tsh. Trilioni 28.39.

Makusanyo hayo ni ongezeko la asilimia 14.5 ikilinganishwa na makusanyo ya Trilioni 24 katika mwaka wa fedha 2022/2023 huku akiwapongeza wafanyabiashara kwa ulipaji mzuri wa kodi pamoja pamoja na waliotunukiwa vyeti vya ulipaji bora wa kodi .

         Baadhi ya wafanyabiashara waliotunukiwa vyeti vya pongezi kwa ulipaji bora wa kodi.






No comments