HEADER AD

HEADER AD

DC CHATO AWAPONGEZA WAANDISHI WA HABARI KUIBUA TUHUMA VIGOGO WA MAJI

>>Vigogo waliohujumi maji kufikishwa Mahakamani


Na Daniel Limbe, Chato

MKUU wa wilaya ya Chato , mkoani Geita , Louis Bura amewapongeza waandishi wa habari na chombo hiki cha habari cha DIMA Online , kwa kuibua habari kwa maslahi mapana ya umma ikiwahusu vigogo wa Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Chato (CHAWASSA) kujihusisha na hujuma ya maji.

Mkuu huyo amesema hayo ikiwa ni siku moja imepita baada ya chombo hiki kuripoti habari yenye kichwa kisemacho 'VIGOGO CHAWASA WADAIWA KUIBA MAJI KUMWAGILIA MASHAMBA YAO' iliyoripotiwa Februari, 07, 2025, ikieleza Vigogo CHAWASA kuchepusha maji kwenye njia kuu na kuyaelekeza kwenye mashamba yao kinyume cha sheria.

    Mkuu wa wilaya ya Chato, Louis Peter Bura akizungumza 

Mbali na pongezi hizo amewataka Waandishi wa habari kuendelea kuihabarisha jamii kila hatua itakayo chukuliwa na serikali kwa wahusika ikiwemo kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.

"Nawapongeza sana kwa kazi nzuri mliyoifanya,naomba muendelee kuibua na mengine zaidi lakini mhakikishe mnaihabarisha jamii kila hatua zitakazo kuwa zinachukuliwa na serikali kwa watuhumiwa hao ili iwe fundisho kwa wengine"amesema Bura.

Kadhalika akichangia mijadala ya wananchi wenye kundi sogozi la watumia maji ya CHAWASSA, ambao waliojitokeza kulaani kitendo cha baadhi ya watumishi kuhujumu miundo mbinu ya maji kwa maslahi yao binafsi, Bura amewataka wananchi hao kuendelea kutoa ushirikiano kwa mamlaka mbalimbali ili kuwadhibiti watu wote wanao hujumu miundo mbinu inayogharamiwa na serikali kwa manufaa ya umma.

Amesema ni matumaini yake kuwa viongozi wa mamlaka hiyo waliobainika kuhujumu uchumi wa nchi kwa kujiunganishia maji pasipo kutumia dira ya kuhesabu kiwango cha matumizi ya maji mashambani mwao, watafikishwa mahakamani haraka.

Baadhi ya watumia maji wilayani hapa, wamelaani kitendo hicho kisicho cha kiungwana kutokana na watumishi hao kuendekeza maslahi yao binafsi badala ya umma.

"Tumekuwa tukipata maji kwa mgao halafu tunajibiwa kuwa mradi ni mdogo ukilinganisha na watumiaji, kumbe kuna mashamba yanapata maji kila siku,huu ni uhujumu uchumi" amesema Amir Madongo.

"Kumbe ndiyo maana Buzirayombo hatupati maji hata tone kumbe kuna vikwazo kwenye njia ya kufikishwa maji,hata tunayo nunua mitaani yameshapandishwa bei,mpaka natamani hao wahusika mgeweka na picha zao hapa ili tuwajue" amesema Musa Sasine.

 Ng'wana Salome (mkazi wa Itale) amesema ukanda wote wa kijiji cha Itale,Nyabilezi, Katende na Buzirayombo hawapati maji safi wala salama kutokana na kutumia njia kuu ya bomba linalochepusha maji kwenye mashamba ya vigogo wa Chawasa.

Ikumbukwe kuwa mwaka 2022 takribani wananchi 11 wa kijiji cha Majengo B kijiji cha Kahumo walilipia kiasi cha sh. 120,000 kila mmoja kwa lengo la kuunganishiwa huduma ya maji ya bomba lakini wameendelea kupigwa danadana hadi sasa pasipo kujua hatma yao huku wakiiomba serikali kuingilia kati ili haki yao ipatikane.   

No comments