ISHA MASHAUZI : UCHUMI WA MWANAMKE UNAMTEGEMEA MWANAMKE MWENYEWE
>> Awahimiza wanawake wa Tarime kujituma
>>Mkurugenzi Mwanzo Mpya Foundation, Mussa Ryoba aeleza malengo ya Taasisi
>>Wambura Mtani, Inspekta Zimbo, Kapteni Nyengedi, YAS, NBC, TWCC wasema jambo
Na Dinna Maningo, Tarime
SHIRIKA lisilo la kiserikali la Mwanzo Mpya Foundation, limewakutanisha baadhi ya wanawake na Taasisi mbalimbali kuadhimisha siku ya wanawake ( Tarime Women's Gala) huku msanii wa muziki wa Taarab, Isha Ramadhani kwa jina maarufu Isha Mashauzi akitoa burudani na kuzikosha nyonyo za wanawake.
Isha mashauzi aliyekuwa mgeni rasmi katika siku hiyo ya wanawake iliyofanyika Machi, 22, 2025 katika ukumbi wa Blue Sky Hotel mjini Tarime amewataka wanawake wa Tarime kuchapa kazi na kusema kwamba uchumi wa mwanamke unamtegemea mwanamke mwenyewe.
Msanii wa nyimbo za Taarab Isha Mashauzi akizungumza na wanawake wa Tarime wakati wa hafla ya Tarime Women's Gala iliyofanyika ukumbi wa Blue Sky Hotel , Machi, 22, 2025.
" Akina mama wa Tarime ninawaomba sana mfunguke kwenye uchumi, hizi shida ndogo ndogo zisiwepo, wanawake tunaweza . Mimi ninafanya shughuli nyingi, wanawake tujitume.
" Kila mtu apambane na familia yake usitegemee kusaidiwa na ndugu . Wanaume wapeni nafasi wanawake wafanye biashara. Mwambie mmeo wewe ukileta na mimi nikileta tunaongeza kipato" amesema Isha.
Amewaomba wanawake kutochagua kazi huku akiwasisitiza kuwafundisha watoto wao kutafuta pesa, kuwa jasiri na kuheshimu watu.
Msanii wa nyimbo za Taarab Isha Mashauzi akitumbuiza na wanawake wa Tarime wakati wa hafla ya Tarime Women's Gala
" Tujitume, mama yangu alikuwa na biashara ya kutengeneza chapati anauza Kariakoo, ameuza ubuyu shuleni nilikokuwa nasoma. Mimi nina watoto wawili nawafundisha malezi niliyofundishwa na mama yangu.
" Nakumbuka nilimkosea mama yangu nikamwambia wimbo mama nipe radhi, nampenda sana mama yangu kwasababu amenifundisha ujasiri. Tuwafundishe watoto wetu kutafuta pesa. Mtoto akijua kutafuta pesa hatopata mimba, kaeni na watoto wenu wafundishe mambo mazuri kwa maendeleo ya baadae" amesema Isha.
Isha amewaomba wanawake kujenga tabia ya kuweka pesa Benki na kwamba wanapokopa fedha ziweze kuzalisha na sio kukopa pesa ili kufanya mashindano ya mavazi na vitu .
" Usikope pesa kununua pete wakati huna biashara ya kukuwezesha kuingiza pesa, kuna wanawake wanakopa pesa kwa ajili ya kufanya mambo kuwaonesha wanawake wenzao. Na usifungue biashara ilimradi tu mwenzio anabiashara " amesema Isha.
Pia amewahimiza wanawake kujenga tabia ya kuwapa zawadi waume wao kwani kufanya hivyo ni kujenga mahusiano na upendo katika ndoa zao.
Kapteni Sharibu Nyengedi kutoka Jeshi la wananchi Tanzania (JWTZ) wilayani Tarime akiwa amemwakilisha mkuu wa wilaya ya Tarime Edward Gowele, amempongeza mkurugenzi wa mwanzo mpya kuwakutanisha wanawake na kuzungumza nao.
Kapteni Sharibu Nyengedi kutoka Jeshi la wananchi Tanzania (JWTZ) wilayani Tarime ( aliyesomama akizungumza
" Ni wasomi wachache sana wanarudi nyumbani kuja kusaidia, anaishi mbali anafanya kazi mbali angeweza kufanya vitu huko lakini akaona arudi nyumbani . Wasomi wote wa Tarime tungerudi kuisaidia Tarime leo Tarime ingekuwa mbali" amesema Nyengedi.
Amewashukuru wanawake kushiriki katika halfa hiyo huku akiwahimiza kujishughulisha ili kupata vipato vyao wasitegemee kila kitu kufanyiwa na mwanaume kwani wakifanya kazi watakuwa huru hawatonyanyaswa na wanaume.
Mkurugenzi wa Mwanzo Mpya Foundation wa tatu kushoto akiwa katika picha ya pamoja na maafisa wa Jeshi la Polisi, wa pili kushoto ni Kapteni Sharibu Nyengedi kutoka Jeshi la wananchi Tanzania (JWTZ) wilayani Tarime.
" Kitu pekee kinachoweza kumfanya mwanamke awe huru ni kipato chake , tutahangaika sana kusema wanaume tusiwanyanyase wanawake lakini kitu pekee kitakachokufanya wewe uwe huru ni kipato chako.
" Ukiwa na kipato chako sisi wanaume waga hatukusumbui yaani wewe ndio utakuwa unatusumbua sisi na tutaishi kwa amani na wewe. Kila kitu ukimtegemea mwanaume mtaishi kwenye hii dunia kwa kunyanyasika , ili msinyanyasike lazima muwe na vipato vyenu, huwezi mtegemea mwanaume kila kitu alafu umkontroo anayekulisha ndio anakukontroo" amesema.
Mkurugenzi wa Shirika la Mwanzo Mpya Foundation, Mussa Ryoba mzawa wa Tarime, mkazi wa mkoani Shinyanga amesema kuwa shirika limejikita katika masuala ya elimu, afya, maji safi na salama na udhibiti wa madawa ya kulevya.
Mkurugenzi wa Shirika la Mwanzo Mpya Foundation, Mussa Ryoba akizungumza wakati wa hafla ya wanawake Tarime
" Tunamshukuru Rais Samia kwa kutusaidia nyenzo mbalimbali kuanzia vijijini, ngazi ya kata kuhakikisha watoto wanapata elimu . Shirika letu linajihusisha pia na udhibiti wa madawa ya kulevya.
"Mimi natoka mtaa wa Tagota kuna vijana pale wanafyatua tofari, baadhi yao wanavuta madawa ya kulevya. Pia tunatamani kila tawi lipate maji safi na salama . Tuna haja ya kumsaidia Rais Samia katika maendeleo . Vilevile naahidi kukisaidia kikundi cha Tarime Women's Gala " amesema Mussa.
Mada mbalimbali zatolewa
Katika siku hiyo ya mwanamke zikatolewa mada mbalimbali kutoka Taasisi binafsi, huku Jeshi la Polisi likikemea vitendo vya matumizi ya dawa za kulevya.
Afisa habari wa Shirika la Mwanzo Mpya Foundation, Wambura Mtani akatoa elimu ya malezi na makuzi akiwasisitiza wanawake kuwalea watoto wao katika maadili mema.
" Akina mama jitahidini sana kubadilika waleeni watoto katika malezi bora. Watoto wetu wanatokana na maisha yetu wazazi, ili mtoto awe na malezi bora inatokana na nyie wazazi" amesema.
Afisa jamii Jeshi la Polisi Tarime, Rorya Inspekta Zimbo Omary ametoa elimu ya madhara ya madawa ya kulevya huku akisema mtu muhimu katika ukuaji kwenye jamii ni mwanamke na kwamba ili jamii iendelee lazima kumwinua mwanamke.
" Wanawake ndio mwalimu wa kwanza kwenye familia,mama anapojifungua mtoto anakuwa wa kwanza kuwasiliana na mtoto kuliko baba, mama ndio mwalimu wa kwanza kwa malezi ya mtoto" amesema.
Amewaomba wanawake kuwachunga watoto wao wasiweze kutumia madawa ya kulevya kwani watoto wana mtindo wa kuiga tabia na kwamba madawa ya kulevya yanaathiri afya ya mwili na utendaji kazi kushuka na kusema kwamba katika mkoa wa Mara jumla ya watu 25769 wamepata tiba.
Meneja Biashara Benki ya NBC Michael Christopher, amesema wanawake wanachangia pato kubwa kwenye biashara na kwamba kupitia biashara zao wameweza kuajiri watu wengi wanaume na wanawake.
"Akaunti ya Johari ni akaunti inayoongozea faida hivyo wanawake mnakaribishwa kujiunga na Benk ya NBC kwani wanawake wanachangia pato kubwa kwenye biashara" amesema Michael.
Meneja wa kampuni ya YAS ambayo awali ilikuwa ikiitwa kampuni ya Tigo mkoa wa Mara, Abdillahi Luhorela amesema kampuni hiyo ina huduma nyingi zikiwemo zinazogusa wanawake.
Meneja wa kampuni ya YAS ambayo awali ilikuwa ikiitwa kampuni ya Tigo mkoa wa Mara, Abdillahi Luhorela akizungumza.
" Kampuni ya YAS ni kampuni ya mawasiliano inayopatikana kwa teknolojia ya 4G , mwanamke yeyote alipo atapata mawasiliano kupitia teknolojia hii. Sisi kampuni tuna huduma ya lipa kwa simu, inamwezesha mfanyabiashara mdogo kupata huduma hii, simu za mkopo unalipa kidogokidogo" amesema Meneja.
Katibu wa Chemba ya Wanawake wafanyabiashara Tanzania, mkoa wa Mara (TWCC) Annastazia Maximilian amesema Chemba hiyo imekuwa ikiwatafutia fursa wanawake Wajasiriamali ndani na nje ya nchi.
Katibu wa Chemba ya Wanawake wafanyabiashara Tanzania, mkoa wa Mara (TWCC) Annastazia Maximilian, akieleza shughuli zinazofanywa na Chemba
" Inawajengea uwezo wanawake hasa kwenye suala la elimu ya fedha na imekuwa ikisisitiza sana wanawake kuwa na nidhamu ya fedha ili kulinda uchumi wa familia na taifa Kwa ujumla.
Regina Mwera mkazi wa mjini Tarime amelipongeza shirika la Mwanzo Mpya Foundation kwa kuwakutanisha wanawake ambapo wameweza kujifunza mada mbalimbali.
Regina Mwera mkazi wa mjini Tarime miongoni mwa waliotunukiwa cheti baada ya kupata elimu iliyotolewa wakati wa hafla ya Tarime Women's Gala.
" Hii siku imekuwa nzuri tumejifunza malezi ya watoto, wanawake tutafute pesa. Niwaombe wanawake wenzangu tulee watoto wetu kwenye maadili, tusiwe bize kwenye shughuli zetu na kusahau kuongea na watoto wetu" amesema Regina.
Wakili wa kujitegemea aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Tarime na Diwani wa Kata ya Nyamwaga, Yomam Misiwa , amempongeza Rais Samia kwa kazi kubwa anayoifanya kuhakikisha wananchi wanapata msaada wa kisheria katika masuala mbalimbali yakiwemo ya ardhi, mirathi, utawala bora.
Wakili wa kujitegemea aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Tarime na Diwani wa Kata ya Nyamwaga, Yomam Misiwa, akielezea yaliyofanywa kwenye uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan .
Picha za matukio katika hafla ya Tarime Women's Gala
Post a Comment