HEADER AD

HEADER AD

MAUWASA MASWA WATOA MSAADA WODI YA WAZAZI

Na Samwel Mwanga, Maswa

KATIKA kuadhimisha kilele cha wiki ya maji,Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Mjini Maswa (MAUWASA) kwa kushirikiana na Wenyeviti wa vitongoji wa mamlaka ya mji mdogo wa Maswa wametembelea Hospitali ya wilaya ya Maswa na kutoa misaada mbalimbali kwa wagonjwa katika wodi ya Wazazi.

Akizungumza Machi 22, 2025 wakati akikabidhi msaada huo,Leonard Mnyeti ambaye alikuwa akimwakilisha mkurugenzi Mtendaji wa MAUWASA amesema kuwa lengo la ziara yao katika hospitali hiyo ni kuwafariji na kuwashika mkono wagonjwa hasa katika wodi ya kinamama waliojifungua.


       Kaimu Mkurugenzi MAUWASA, Leonard Mnyeti(kushoto)akimkabidhi,Joyce John sabuni na mafuta ambaye ni mmoja wa wagonjwa waliolazwa katika wodi ya wazazi hospitali ya wilaya ya Maswa ikiwa ni sehemu ya kilele cha wiki ya maji mwaka 2025.

Amesema kuwa MAUWASA katika  maadhimisho ya wiki ya maji moja ya mipango waliyoipanga ni pamoja na kuungana na Wajumbe wa Mamlaka ya Mji mdogo wa Maswa ambao ni wenyeviti wa vitongoji katika eneo linalohudumiwa na mamlaka hiyo kwa kutembelea chanzo cha maji ambalo ni bwawa la New Sola na hospitali hiyo.

“Mmetuona tumeungana na wajumbe wa mamlaka ya mji mdogo wetu wa Maswa hili jambo tulilipanga ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya wiki ya maji ambapo leo yamefikia kilele.

“Tuliona ni vyema tuwe nao kwa kuwa maeneo yao ya utawala sisi MAUWASAasa ndiyo tunayahudumia hivyo kabla ya kufika hapa hospitalini tumewatembeza kwenye bwawa letu na kuona jinsi maji yanavyotibiwa na kuchujwa na kisha kusukumwa kwa wananchi,” ”amesema.

Ametoa pongezi kwa madaktari, wauguzi na watumishi wengine wa hospitali hiyo kwa kuwathamini na kujitoa kwao kuwahudumia wagonjwa waliopo hospitalini hapo.

      Mwakilishi wa Mganga Mfawidhi wa hospitali ya wilaya ya Maswa(aliyeko kushoto)akipokea vifaa vya usafi kutoka MAUWASA ikiwa ni sehemu ya kilele cha wiki ya Maji 2025.

Mnyeti aliukabidhi uongozi wa hospitali hiyo bidhaa zenye thamani ya Sh Milioni Moja zikijumuisha sabuni za kufulia na kuogea,mafuta ya kujipaka pamoja na dawa kufanyia usafi na vifaa vya usafi katika wodi.

Akipokea msaada huo ,Matroni wa hospitali hiyo,anastela Selestine ameishukuru Mauwasa kwa kuwakumbuka wahitaji hao ambao wamelazwa katika hospitali ya wilaya ya Maswa.

“Msaada huu ni wa muhimu sana na utasaidia kutatua baadhi ya changamoto zilizopo kwa wagonjwa wetu hawa tulionao na wanaendelea kupata matibabu,”amesema.

Pia ametoa wito kwa taasisi nyingine za serikali na zile za binafsi kuiga mfano huo ili kuwezesha hospitali hiyo kuwahudumia kikamilifu wagonjwa,ambapo baadhi yao wametelekezwa na familia zao.

Mwenyekiti wa mamlaka ya mji mdogo wa Maswa,Carolina Shayo amesema kuwa hiyo ni hatua nzuri ya MAUWASA kushirikiana na viongozi wa vitongoji na kusaidia jamii kwa vitendo.

     Angela Masunga mtumishi wa MAUWASA (kulia) akimkabidhi Agata Wiliam (kulia) sabuni na mafuta katika wodi ya wazazi katika hospitali ya wilaya ya Maswa ikiwa ni kilele cha wiki ya maji.

“Maadhimisho ya kilele cha wiki ya Maji kwa mtindo huu yanaonyesha dhamira ya taasisi hiyo ambayo ni MAUWASA katika kuwajali wananchi sambamba na kuboresha huduma za maji na kujali ustawi wa wananchi,”amesema.

Naye Joyce John ambaye ni miongoni mwa waliopatiwa msaada huo amesema kuwa hii inathibitisha ukaribu wa MAUWASA kushirikiana na wananchi katika changamoto wanazozipata.

“Huu ni uthibitisho dhahiri wa ukaribu wa MAUWASA na sisi wananchi maana ni nadra sana kuona taasisi za serikali kutembelea wagonjwa na kuwafariji kwa kuwapatia misaada mbalimbali kama hii tuliyopatiwa binafsi nashukuru sana,”amesema.

Agata Wiliamu aliyelazwa katika hospitali hiyo anasema kuwa MAUWASA imeonyesha umuhimu wa kuwajali wagonjwa kwa njia ya misaada ya faraja nah ii inaimarisha mshikamano kwa jamii.

“Jambo hili linasaidia kujenga mshikamano kati ya taasisi na jamii kwa ujumla kutokana na kutoa hii misaada kwetu sisi ambao bado wodini tukiendelea na matibabu mbalimbali,”amesema.


No comments