HEADER AD

HEADER AD

KUKWAMA MIUNDOMBINU YA ELIMU, AFYA KWAWANYIMA USINGIZI MADIWANI

Na Daniel Limbe, Biharamulo

KUKWAMA kwa miundombinu ya ujenzi wa vyumba vya madarasa, nyumba za walimu,zahanati na akidi ndogo ya watumishi wa umma kwenye halmashauri ya wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera, imeendelea kuumiza vichwa vya madiwani wa halmashauri hiyo.

Hatua hiyo inatokana na taarifa za kata zilizowasilishwa kwenye kikao cha robo ya pili cha Baraza hilo, ambazo zimeonyesha kila kata inakabiliwa na uhaba mkubwa wa fedha za kukamilisha miradi ya sekta ya elimu na afya.

        Madiwani halmashauri ya Biharamulo  wakijadili hoja mbalimbali.

Kadhalika uhaba wa watumishi umeendelea kuwa kilio cha kila diwani huku baadhi yao wakiwapongeza wadau wa maendeleo(sekta binafsi) ambao wekuwa wakisaidia kutatua baadhi ya changamoto za elimu ikiwemo ujenzi wa matundu ya vyoo kwenye shule za msingi. 

Wamesema kukosekana kwa fedha za ukamilishaji wa miradi hiyo umekuwa ukikwamisha jitihada za watoto kusoma kwa utulivu na usalama zaidi kutokana na baadhi ya wanafunzi kusomea chini ya miti jambo linaloshusha kiwango cha taaluma.

Uhaba wa zahanati na watumishi wa umma imetajwa kuwa sababu ya wanawake kuendelea kujifungulia majumbani na baadhi yao kujifungulia njiani kutokana na umbali wa kufika vilipo vituo vya kutolea huduma.

Miongoni mwa kata hizo ni pamoja na Rusahunga, Runazi, Nyamigogo, Nyamahanga, Kalenge pamoja na Nemba, ambao wote wamewasilisha taarifa za upungufu wa miundo mbinu katika sekta ya afya, elimu na uhaba wa watumishi.

Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Innocent Mkandara, amekiri kuwepo kwa uhaba mkubwa wa fedha za ukamilishaji wa miradi inayotajwa na madiwani hao kutokana na kuwa ni masuala ya kibajeti zaidi.

      Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Biharamulo,Innocent Mkandara akizungumza.

Hata hivyo ameendelea kutoa faraja kwa madiwani hao kuwa halmashauri hiyo itaendelea kutenga fedha kila bajeti ya mwaka kwaajili ya kutatua changamoto za miundo mbinu hiyo ili kuondoa kero zilizopo katika jamii.

Pia amewata madiwani hao kuwa na vipaumbele katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kutokana na fedha zinazotolewa na serikali kuwa kidogo ukilinganisha na mahitaji ya jamii.

"Suala la uhaba wa watumishi ni tatizo kubwa hasa kwa sekta ya elimu na siyo kwetu pekee, ispokuwa ni wilaya zote zina upungufu wa watumishi na kila serikali inapoajili huwa tunapewa idadi frani ya watumishi japo hawatoshelezi katika mahitaji" amesema Mkandara.

Mwenyekiti wa halmashauri hiyo,Leo Rushahu, amewataka madiwani hao kuendelea kusimamia ukusanyaji wa mapato ya ndani ya halmashauri ili kuiwezesha halmashauri kukamilisha maboma yaliyo kwama.

"Niwasihi sana madiwani wenzangu tujitahidi sana kusimamia makusanyo ya vyanzo vyetu vya mapato ya ndani, tukikusanya vizuri itatusaidia kupunguza changamoto nyingi tulizonazo kwenye kata zetu badala ya kutegemea fedha kutoka serikali kuu pekee" amesema Rushahu.
                     
     Katikati ni mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Biharamulo, Leo Rushahu,Kushoto ni makamu mwenyekiti, Erick Methord na kulia ni Mkurugenzi wa halmashauri, Innocent Mkandara.
     

No comments