HEADER AD

HEADER AD

RC MARA AAGIZA MADEREVA WA MABASI WANAOSHUSHA ABIRIA BUNDA NYASURA , BUNDA DDH WAKAMATWE

>> Ataka mabasi yaingie ndani ya stend ya Bunda kushusha, kupakia abiria

Na Jovina Massano, Musoma

MKUU wa mkoa wa Mara ametoa siku ishirini na moja kwa viongozi wa halmashauri,Polisi, Wilaya ya Bunda mji  kuhakikisha wanawakamata madereva wa mabasi wanaoshusha abiria na kupakia katika vituo vya vya Bunda Nyasura na Bunda DDH kuanzia March 5,2025.

Amesema kumekuwa na tabia ya madereva wa mabasi kupakia na kushusha abilia kwenye vituo hivyo badala ya kuingia ndani ya stendi kuu ya mabasi ya wilaya hiyo jambo ambalo ni kinyume  cha sheria .

Ametoa agizo hilo jana mara baada ya mkuu wa Usalama barabarani mkoani humo Adribert Ntilicha kuwasilisha taarifa ya usalama barabarani wakati wa kikao cha bodi ya barabara katika ukumbi wa uwekezaji Manispaa ya Musoma.

         Mkuu wa Mkoa wa Mara Kanali Evans Mtambi akiongea na wajumbe wa bodi ya Barabara.

"Halmashauri, LATRA, Wakala wa Barabara Tanzania (TANROAD) nawapa siku ishirini na moja vibao hivyo visiwepo na hayo mabasi yasisimame kushusha abiria hapo nawaagiza Askari wa Usalama barabarani wawakamate kwa kuvunja sheria,"amesema RC Mtambi.

Mkuu wa Usalama barabarani mkoani Mara, Adribert Ntilicha amewaambia wajumbe kwamba ,kumekuwa na ukiukwaji wa usimamaji wa mabasi ya abiria kwa kusimama barabarani na kushusha abiria kitendo ambacho kinachangia ongezeko la ajali za barabarani na kuhatarisha maisha ya watu.

        Wajumbe wa bodi ya Barabara wakimsikiliza mkuu wa usalama barabarani mkoa wa Mara

"Kwa kuwa stendi ipo ni vema ikatumika ili kupunguza ajali zisizo za lazima kwa raia. Kitengo cha usalama barabarani kimekuwa kikiwachukulia hatua lakini wamekuwa wakidai kuwa kuna alama inayowaruhusu kushusha abiria katika vituo hivyo.

"  Tunashauri alama zinazoruhusu mabasi hayo kushusha na kupakia abiria ziondolewe ili kuepusha ajali zisizo za lazima,"amesema Adribert.

Akitolea ufafanuzi wa alama hizo Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania TANROAD mkoani Mara,
Mhandisi Vedastus Maribe amesema uwepo wa alama hizo ni kwa ajili ya ushushaji wa abiria wa magari madogo (Daladala) zikiwemo bajaji na si kama inavyotumiwa na madereva wa mabasi yaendayo mikoani.

Nae Afisa Mfawidhi wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) George Robert amewaasa madereva wa mabasi kufuata utaratibu na sheria zilizowekwa ili kuepuka faini zisizo za lazima na kupunguza athari kwa jamii za ajali zinazoepukika.

      Afisa mfawidhi wa Mamlaka ya udhibiti Usafiri Ardhini LATRA mkoa wa  Mara George Robert akizungumza 
    
Hata hivyo Mwenyekiti wa halmashauri ya mji wa Bunda Michael Kweka amesema kuwa ushushaji huo wa abiria barabarani unashusha mapato ya Serikali na kukwepa kulipa ushuru wa halmashauri.

     Wakuu wa Wilaya za  mkoa wa Mara wakisikiliza hoja mbalimbali zinazotolewa kwenye kikao cha Bodi ya Barabara.

No comments