MJUMBE WA MKUTANO MKUU CCM TAIFA HAJULIKANI ALIPO
>> Polisi Mwanza yasema inaendelea na uchunguzi
MJUMBE wa mkutano mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa , Daniel Chonchori maarufu Chox , mkazi wa mtaa wa Temeke, wilaya ya Nyamagana, mkoani Mwanza ambaye ni mfanyabiashara na aliyekuwa amedhamilia kutiania kugombea ubunge Jimbo la Tarime mjini hajulikani alipo.
Katika mitandaoni ya kijamii ikiwemo makundi ya WhatsApp na mtandao wa X zimesambaa taarifa za kutojulikana mahali alipo huku wanafamilia, ndugu, jamaa na marafiki wakiliomba Jeshi la Polisi kusaidia aweze kupatikana .
Mjumbe wa mkutano mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa , Daniel Chonchori maarufu Chox hajulikani alipo.
Hata hivyo Jeshi la polisi mkoa wa Mwanza limetoa taarifa ya kupotea kwa Daniel Chonchori mwenye umri wa miaka 46, kwamba mnamo tarehe 23.03.2025 majira ya 20:00hrs katika kituo cha polisi Nyamagana zilipokelewa taarifa kutoka kwa familia ya Daniel Chonchorio ambao ni wakazi wa mtaa wa Temeke kata ya Nyakato.
Ndugu hao walieleza kuwa Daniel majira ya 08:00hrs aliondoka nyumbani kwake akiwa emevaa nguo za mazoezi na simu yake ya mkononi na kuaga kuwa anakwenda kufanya mazoezi ya viungo na angerudi nyumbani mara baada ya mazoezi hayo.
Kwa mujibu wa SACP Majaliwa amesema ndugu hao wamedai kuwa, ilipofika majira ya 11:00hrs ndugu Daniel hakurejea nyumbani hali iliyoifanya familia yake kuingiwa na wasiwasi, hivyo kulazimika kutoa taarifa kwa Jeshi la polisi.
Taarifa hizo zilipokelewa na uchunguzi kuanza mara moja, huku Jeshi la polisi likishirikiana kwa karibu na familia, ndugu, jamaa na marafiki. Hata hivyo Daniel Chonchorio hadi sasa hajapatikana.
Ameongeza kuwa Daniel Chonchori ambaye pia ni mjumbe wa halmashauri kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) makazi yake mengine ni pamoja na Tarime mkoa wa Mara na Dar es Salaam.
Amesema uchunguzi kuhusiana na tukio hilo unaendelea kufanyika na Jeshi la polisi mkoa wa Mwanza linawaomba wananchi au mtu yeyote atakaye kuwa na taarifa kumuhusu Daniel Chonchorio, atoe taarifa kwenye kituo cha polisi kilicho karibu naye au kwenye mamlaka nyingine za Serikali.
Post a Comment