MKE WA MBUNGE KOKA, UWT WATEMBELEA WAGONJWA WODI YA WAZAZI
Na Gustaphu Haule, Pwani
Selina Koka mke wa mbunge wa Jimbo la Kibaha Silvestry Koka amewaongoza Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)kutembelea wagonjwa na kutoa msaada katika wodi ya Wazazi katika hospitali ya Mji Kibaha iliyopo Mtaa wa Lulanzi Kata ya picha ndege.
Selina amewaongoza Wanawake hao ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya wiki ya wanawake duniani ambayo kimkoa yatafanyika wilayani Mkuranga na Kitaifa yatafanyika mkoani Arusha Machi 8,2025.
Akiwa hospitalini hapo mke wa mbunge huyo amewajulia hali wagonjwa sambamba na kutoa msaada wa sabuni katika wodi ya Wazazi huku akiahidi kuchangia Makoti 15 ya madaktari pamoja na shuka kwa ajili ya vitanda vya wagonjwa wa hospitali hiyo.
Selina Koka akimjulia hali mjamzito katika hospitali ya Kibaha Mjini ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya wiki ya wanawake duniani.
Akizungumza hosptalini hapo Selina,amemshukuru Rais wa awamu ya Sita Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya ikiwa pamoja na kuhakikisha anatoa fedha za kukamilisha ujenzi wa hospitali hiyo.
selina amesema kuwa wanawake wa Kibaha Mjini wanajivunia kupata Rais mchapakazi na kwamba lazima kama Wanawake wahakikishe wanamuunga mkono mwanamke mwenzao ili kusudi waendelee kujenga heshima hapa Nchini.
Selina Koka mke wa mbunge wa Jimbo la Kibaha Silvestry Koka akimkabidhi zawadi ya sabuni mjamzito katika hospitali ya Mji Kibaha iliyopo Mtaa wa Lulanzi Kata ya Picha ya Ndege.
"Tupo katika wiki ya maadhimisho ya Wanawake duniani, hivyo sisi Wanawake wa Kibaha Mjini tumeona ni vyema kuja hapa kuwaona wenzetu na kuwapa chochote tulichojaaliwa lakini haitakuwa mwisho kwani tutafanya mengine makubwa,"amesema Selina
Selina amesema mafanikio ya ujenzi wa hospitali hiyo yametokana pia na mchango wa Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka aliyesimamia kikamilifu ujenzi wa hospitali hiyo na hivyo kupelekea Wananchi wake kupata huduma ya matibabu kirahisi.
Amesema Mbunge yupo tayari kuendelea kushirikiana na Wananchi wake katika kuhakikisha Kibaha Mjini inapiga hatua zaidi ya kimaendeleo huku akisema atahakikisha anazifanyiakazi changamoto mbalimbali zilizopo hospitalini hapo.
Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo Bertha Makidika, amemshukuru Mke wa Mbunge huyo kwa kuona umuhimu wa kutembelea hospitalini hapo pamoja kutoa msaada kwa Wajawazito na wazazi katika wodi hiyo.
Jengo la Wazazi katika hospitali ya Mji Kibaha iliyopo Mtaa wa Lulanzi Kata ya Picha ya Ndege mkoa wa Pwani
Makidika amesema kuwa anatambua mchango wa Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka katika hospitali hiyo kwani mara kwa mara amekuwa akisaidia hospitali hiyo .
"Mara nyingi sana huwa napokea salamu za misaada mbalimbali kutoka kwa mbunge hata kama sio yeye basi anatuma mtu mwingine hivyo nakushukuru wewe mama na mbunge Koka kwa mchango wenu mkubwa katika hospitali hii," amesema Makidika.
Hatahivyo, Makidika amemuomba mke wa Mbunge huyo pamoja Mbunge wa Jimbo la Kibaha mjini kuendelea kusaidia katika changamoto zinazowakabili ili kuhakikisha huduma katika hospitali hiyo zinaboreshwa zaidi.
Post a Comment