HEADER AD

HEADER AD

HAO WANAKUCHEKEA, NDIO WATAKUZOMEA

ETI gari majitaka, likipita mtaani,

Sisi wazalisha taka, tunajishika puani,

Harufu kali yanuka, tulozalisha nyumbani,

Hao wanakuchekea, ndio watakuzomea. 


Barabara ya Nyerere, siadithiwe jioni,

Lori lenye taka bure, harufu hadi moyoni,

Ni sisi tulao kware, twazalisha mitaani,

Hao wanakuchekea, ndio watakuzomea. 


Zililika zile taka, matumizi ya nyumbani,

Ni hizo zilitumika, kuzalisha viwandani,

Zikiwa ni takataka, tuzitaki asilani,

Hao wanakuchekea, ndio watakuzomea. 


Usiombe uwe taka, kama zile jalalani,

Wale waliokutaka, sasa wakumwaga chini,

Kwao ukicheka cheka, unaonekana duni,

Hao wanakuchekea, ndio watakuzomea. 


Kwa shangwe ulisikika, ulipokuwa enzini,

Kawaida kuinuka, ulipopita njiani,

Watu walitetemeka, ukiwepo kikaoni,

Hao wankuchekea, ndio watakuzomea. 


Sankara namtamka, mfano wa duniani,

Yule aliyemshika, kumsogeza kitini,

Ndiye aliyegeuka, Kwake kawa mfitini,

Hao wanakuchekea, ndio watakuzomea. 


Ni bora angemshika, amtie gerezani,

Jinsi alivyomchoka, ni risasi za mwilini,

Sankara hakuinuka, alienda kaburini,

Hao wanakuchekea, ndio watakuzomea. 


Bora unasikitika, aibu iko njiani,

Jinsi ulivyotukuka, ukitembea vichwani,

Ndivyo watavyokuzika, ukatupwe jalalani,

Hao wanakuchekea, ndio watakuzomea. 


Kile kinahitajika, ukiwapo kileleni,

Usije ukaehuka, utabakia enzini,

Kushushwa au kumshika, ni kikoa mtaani,

Hao wanakuchekea, ndio watakuzomea. 


Hili limeeleweka, ila ni gumu kichwani, 

Hatamu ukizishika, unaliweka kazumi,

Siku utapokumbuka, ni taka ya jalalani,

Hao wanakuchekea, ndio watakuzomea. 


Jua tayari wanuka, wewe uvundo hewani,

Kijaribu kuinuka, unasukumizwa chini,

Miti yote ukimshika, waishia sakafuni,

Hao wanakuchekea, ndio watakuzomea. 


Shairi limetungwa na Lwaga Mwambande (KiMPAB)

lwagha@gmail.com 0767223602

No comments