NYAMBARI NYANGWINE KUWAPELEKA DAR ES SALAAM WAIGIZAJI WA FILAMU YA HIMAYA YA NYAKONGA
>> Lengo kuwakutanisha na wasanii wakubwa wa sanaa ya uigizaji
>> Ni vijana wazawa wa Nyakonga walioigiza filamu kijijini
>> Vijana wamtunuku Nyambari tuzo kuwaunga mkono katika sanaa ya uigizaji
>> Diwani Kata ya Nyakonga awaomba wananchi kuwaunga mkono waigizaji
Na Dinna Maningo, Tarime
MBUNGE wa zamani Jimbo la Tarime Nyambari Nyangwine ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Nyambari Nyangwine Foundation amesema kati ya mwezi Mei au Mwezi juni, 2025, atawapeleka mkoani Dar es Salaam, waigizaji wakazi wa Kata ya Nyakonga, wilaya ya Tarime mkoani Mara ili kuwakutanisha na wasanii wakubwa wa sanaa ya uigizaji.
Nyambari ametoa ahadi hiyo baada ya kufika Kijiji cha Magoto, Kata ya Nyakonga Machi, 8,2025 na kukutana na vijana wa Nyakonga walioigiza filamu iitwayo 'Himaya ya Nyakonga ' ambapo mgeni rasmi katika uzinduzi alikuwa Nyambari aliyewakilishwa na kada wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Daniel Magita .
" Mlinialika nije kuzindua filamu yenu lakini sikuweza kufika kwasababu nilikuwa nje ya nchi, nikamtuma mwakilishi akaleta Milioni 2 na wadau wengine waliniunga mkono fedha zikafika Tsh. Milioni 3.7 ikabaki Tsh. Milioni moja.
" Leo nimeona nifike niwaone niwafahamu na nikamilishe deni lililokuwa limebaki Tsh. Milioni moja , fedha hizi hapa nimetoa na hivyo bajeti yenu iliyohitaji Tsh. Milioni 4.7 imekamilika " amesema Nyambari.
Nyambari amesema kuwa alikuwa hajawahi kuonana ana kwa ana na vijana hao wa Kikundi cha Nyakonga Filamu na kwamba walimpigia simu kumuomba mchango na kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa filamu yao ya kwanza ya Himaya ya Nyakonga na hakusita kuchangia .
Nyambari Nyangwine aliyevaa kofia na suti akiwa katika picha ya pamoja na wanakikundi cha Nyakonga Filamu ,Machi, 8, 2025 katika Kijiji cha Magoto
" Mwenyekiti wa kikundi alikuwa anawasiliana na mimi kwa simu , sikuwa namfahamu wala sijawahi kuonana nae, ndio namuona hapa leo kwa mara ya kwanza . Alikuwa akinipigia simu na nimewachangia fedha nikiwa siwafahamu .
" Wanaosema Nyambari hapokei simu ni waongo . Niwaombe tushikamane ,Nyakonga ni yetu tuendelee kuiunga mkono na kushikamana , nami nitaendelea kuwaunga mkono" amesema Nyambari.
Diwani wa Kata ya Nyakonga ambaye pia ni Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Tarime , Simion Kiles , amemshukuru Nyambari kwa kuwaunga mkono vijana wa kata yake na kwamba wakienda Dar es Salaam mamabo yao yatakuwa mazuri kwakuwa watajifunza mengi.
Mwenyekiti wa kikundi cha Nyakonga Film Group Chacha Isaya kushoto na Diwani wa Kata ya Nyakonga, Simon Kiles wakiwa wameshika cheti kilichotolewa na kikundi cha Nyakonga Filamu maalum kwa Nyambari Nyangwine
" Tunamshukuru Nyambari kwa kuwaunga vijana. Tunakuomba uendelee kutusaidia . Mtu yeyote aje atuunge mkono. Filamu ya Himaya ya Nyakonga inajumuisha vijana, watoto, akina mama na wazee.
" Tuwaunge vijana maana sanaa ni ajira tunaiona kila mahali hata Rais akienda kwenye shughuli zake anawatumia wasanii. Ipo siku na nyie mnaweza mkatumiwa na Rais. Tunampongeza Rais Samia kwa kuwajali wasanii na tuna muunga mkono" amesema Simion.
Vjana wa Nyakonga wakamkabidhi Nyambari Nyangwine cheti cha pongezi kutokana na mchango wake katika kuunga juhudi za vijana katika sanaa ya uigizaji.
Mwenyekiti wa kikundi cha Nyakonga Film Group Chacha Isaya akimkabidhi cheti cha shukrani Nyambari Nyangwine
Mwenyekiti wa kikundi cha Nyakonga Film Group Chacha Isaya amempongeza Nyambari kwa mchango wake wa kuunga juhudi zao katika sanaa ya uigizaji.
" Wanaosema Nyambari hapokei simu wapuuzeni. Mimi nimekuwa nikiwasiliana na Nyambari kwa simu wakati wote, hata kama ni usiku wa manane anapokea simu yangu.
" Tunakushukuru Nyambari umekuwa mstari wa mbele kutuunga juhudi . Fedha ulizotupatia tumenunua vifaa kama vile Kompyuta, Camera , Standi, tumeweza kupata ofisi. Lengo letu ni kufika mbali kama wasanii wengine wakubwa " amesema Chacha.
Nyambari Nyangwine akionesha cheti alichokabidhiwa na kikundi cha Nyakonga Filamu
>>>Rejea
Awali katika uzinduzi wa filamu ya Himaya ya Nyakonga, Februari, 24, 2025, Daniel Magita akimwakilisha Nyambari alitoa fedha Tsh. Milion 2 fedha za Nyambari, ambapo awali Nyambari alitoa Tsh. Milioni 1.4 kwa ajili ya maandalizi ya uzinduzi na kwamba Nyambari nakusema kwamba Nyambari ataendelea kuunga juhudi za wasanii hao wa uigizaji.
Kada wa CCM Danie Magita hivi karibuni akikabidhi fedha zilizotolewa na Nyambari Nyangwine kwa kikundi cha Nyakonga Filamu
" Nyambari Nyangwine amesema kuwa ataendelea kuwachangia kadri mtakavyohitaji msaada, na hata sasa amewaleta waandishi wa habari hapa ili kuripoti tukio lenu watu wawaone wajue kumbe hata vijijini kuna watu wana vipaji.
" Nyambari Nyangwine hana mambo ya koo yeye ni Mwirege lakini amesaidia vijana wa koo ya Nyabasi , yeye anaangalia uwezo wa mtu katika kupambana katika maendeleo" alisema Daniel.
Diwani wa Kata ya Nyakonga, Simon Kilesi nae hakuwa nyuma alichangia Tsh. Milioni 1.1 huku wananchi nao wakimuunga fedha ambapo jumla ya kiasi cha Tsh. Milioni 3.7 zilichangwa ambapo hitaji ni pesa Tsh. Milioni 4.7 na hivyo kubaki zikihitajika Milioni 1 kukamilisha hitaji la fedha kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya kurekodia kazi ya sanaa katika uigizaji , fedha ambazo Leo Nyambari amezikamilisha.
Nyambari Nyangwine akitazama baadhi ya vifaa vilivyonunuliwa na kikundi cha Nyakonga Filamu kwa fedha za Nyambari Nyangwine na wadau wengine wa maendeleo akiwemo Diwani wa Kata ya Nyakonga Simon Kilesi
Katibu wa umoja wa vijana wa chama cha mapinduzi (UVCCM) kata ya Nyakonga, Mwita Francis aliwaomba vijana kusonga mbele " Hiki kinachofanyika hapa kinatokana na umoja wa vijana , haya ni matunda ya jumuiya ya vijana . Kuna wakati walikata tamaa lakini niliwashauri tusonge mbele na leo wamezindua filamu" amesema.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyakonga Makomo Magabe aliwapongeza vijana kwa kujihusisha na sanaa ambao ni wa kwanza kuibuka katika Kijiji chake huku akiwahimiza kuchapa kazi ili wajekuwa wasanii wakubwa.
Post a Comment