NYAMBARI NYANGWINE AWAOMBA VIONGOZI WA DINI KUKEMEA MMOMONYOKO WA MAADILI KWA VIJANA
>>Asisitiza jamii kupendana, akemea migogoro ya koo
>>Afanikisha Milioni 13 harambee kanisa la Nyabitocho SDA , yeye akichangia Milioni 5.
>> Awapatia Milioni 2 Kwaya ya kanisa la EAGT Sirari Bondeni
>>Diwani Kata ya Nyakonga awaomba waumini kuombeana mazuri
Na Dinna Maningo, Tarime
MBUNGE mstaafu Jimbo la Tarime ,Nyambari Nyangwine ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Nyambari Nyangwine Foundation amewaomba viongozi wa dini kukemea vitendo vya mmomonyoko wa maadili kwa vijana.
Pia amewaomba wanajamii na waumini kupendana kwani mambo ya dunia yatapita lakini neno la bwana litasimama imara na kwamba jamii iungane kushirikiana pamoja ili Tarime iendelee kupata maendeleo.
Mbunge mstaafu Nyambari Nyangwine akizungumza na waumini wa kanisa la Nyabitocho SDA wakati wa harambee ya ujenzi wa kibweta cha makambi
Ameyasema hayo Machi , 8, 2025 wakati wa harambee katika kanisa la Waadevestista Wasabato Nyabitocho,Kata ya Mbogi wilayani Tarime, mkoani Mara.
" Viongozi wa dini wana nafasi kubwa kukemea maovu na mmonyoko wa maadili ya vijana wetu . Tukemeeni mmonyoko wa maadili na uvunjifu wa heshima kwa vijana wetu , tuwalee vyema watoto wetu wampendeze Mungu na tuweze kupata Taifa lenye vijana wazuri.
" Vijana wengi kutwa nzima wanashinda kwenye mitandao kutukana watu sijui wanafanya kazi saa ngapi, na ukisoma wanayoandika hayana mafundisho wala maadili." Amesema Nyambari.
Ameongeza kusema " Mimi na Christopher Kangoye tuligombeaga ubunge kwenye kura za maoni za chama lakini nilisema pamoja na siasa zetu lazima tupendane na tushikamane.Kangoye alinifundisha upendo ,unyeyekevu alinisaidia sana kunijenga katika upendo" amesema.
Kiongozi wa Pathfinder kanisa la Nyabitocho SDA akimvalisha skafu Nyambari Nyangwine wakati alipowasili kanisani kwa ajili ya harambee ya ujenzi wa kibweta
" Nasisitiza upendo tupendane haya ya dunia yatapita lakini neno litasimama, tusitukanane tupendane . Mengi yanasemwa, yatasemwa lakini Nyambari ni yule yule" amesema Nyambari.
Nyambari ameiomba jamii kuepuka siasa inayochochea migogoro huku akiwaomba viongozi wa dini kukemea vitendo vya migogoro ya koo vinavyopelekea kuvunjika kwa amani na kuleta hofu kwa wananchi.
" Sasa hivi kumeibuka migogoro ya koo kwa baadhi ya koo inayopelelea kuvunjika kwa amani na wananchi kupata hofu. Niwaombe viongozi wa dini tukemee migogoro ya koo inayoibuka. Viongozi wa dini wana nafasi kubwa ya kutokomeza migogoro ya koo" amesema Nyambari.
Pia amewasisitiza vijana kujiajiri badala ya kukimbilia kuajiriwa na kusema kwamba hakuna mtu anayepata mafanikio makubwa kwa kutegemea kuajiriwa.
Waumini wa kanisa la Nyabitocho SDA wakiwa kanisani kwenye harambee ya ujenzi wa kibweta
Nyambari Nyangwine katika kuunga juhudi za kanisa ameendesha harambee katika kanisa la Nyabitocho na kufanikiwa upatikanaji wa fedha tasilimu Tsh. Milioni 13.6 na ahadi zaidi ya Tsh. Milioni 5.huku yeye akichangia Tsh. Milioni 5 ujenzi wa kibweta kanisa la Nyabitocho na ahadi sh. Milioni 5 kwa kanisa la Nyabitocho, ahadi ya Tsh. Milioni mbili Kyoruba mlimani SDA.
Nyambari akiwa Sirari alichangia Tsh. Milioni 2 Kwaya ya kanisa la Evangelistc Assembles of God Sirari Bondeni (E.A.G.T).
Pia madiwani wanane katika halmashauri ya wilaya ya Tarime walimuunga mkono Nyambari kwa kuchanga jumla ya Tsh. 900,000 ujenzi wa kibweta kanisa la Nyabitocho na kumpongeza kwa juhudi zake za kuchangia makanisa.
Diwani wa Kata ya Nyakonga ambaye pia ni Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Tarime Simion Kilesi amewataka waumini kutoombeana mabaya badala yake waombeane mema huku akichangia harambee Tsh. Milioni moja ujenzi wa kibweta.
" Tunamshukuru Nyambari kushiriki harambee , washiriki wa Nyabitocho walipoambiwa unakuja kuwachangia walifurahi na wakasema kibweta kitakamilika .Mungu kwanza ndio mengine yafuate .Nimekuwa nikichangia harambee nyingi na sijawahi kupungukiwa ,unapotoa unabarikiwa.
Diwani wa Kata ya Nyakonga ambaye pia ni Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Tarime Simion Kilesi.
" . Duniani kuna mambo mengi , unapomjua Mungu unapata neema nyingi. Tuombeane mema, tusiombeane mabaya, tusisemane vibaya tusemane vizuri ili watu wa Mungu Waziri kuokolewa kupitia kazi ya Mungu inayofanyika" amesema Diwani Simion.
Mshiriki wa kanisa la Nyabitocho Selonga Paul amesema kata ya Mbogi ilisaulika hivyo amefurahi baada ya yeye kumuomba Nyambari kushiriki kwenye harambee na amefika na kuchangia fedha huku naye akichangia Tsh. 600,000 na ahadi ya Tsh. 400,000.
Mkurugenzi wa Mara Online ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa habari mkoa wa Mara, Jacob Mugini amechangia Tsh. 200,000 na Christopher Kangoye akichangia Tsh. 200,000 .
Mwenyekiti wa Chama cha wanaandika wa habari mkoa wa Mara na mmiliki wa Mara Online akizungumza wakati wa harambee Nyabitocho SDA
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Mbogi Chacha Matiko aliahidi mifuko mitano ya saruji atakayoitoa jumamosi ya wiki ijayo.
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Mbogi Chacha Matiko akizungumza wakati wa harambee SDA
Akisoma taarifa ya kanisa la Nyabitocho, mzee wa kanisa hilo Lukius Chacha Kirigiti amesema mtaa wa Nyabitocho ulipokea injili mwaka 1946 kutoka kanisa la Magoto na kwamba mtaa huo una makanisa matano.
Mzee wa kanisa la Nyabitocho SDA Lukius Chacha Kirigiti akisoma risala wakati wa harambee kanisa la Nyabitocho
Amesema kanisa lilijengwa kwa michango ya washiriki na wadau wa maendeleo na kwamba linahitaji kujenga kibweta cha kufanyia makambi na vivuli vya kuketi waumini wakati wa makambi.
Amesema kiasi cha Tsh. Milioni 60 kinahitajika ambapo wao kanisa wamefanikiwa kuchanga zaidi ya Tsh. Milioni 5 na lengo kufikia makambi ya mwezi wa saba kibweta kiwe kimekamilika.
Mchungaji wa mtaa wa Nyabitocho Kumba Kihiri amempongeza Nyambari, Madiwani, wadau wa maendeleo pamoja na washiriki kwa kuchanga fedha kwa ajili ya ujenzi wa kibweta na kuwaomba wasiishie hapo na badala yake waendelee kuyasaidia makanisa.
Post a Comment