HEADER AD

HEADER AD

RCC KAGERA YAPINGA KUGAWANYWA JIMBO LA BIHARAMULO NA NGARA

Na Alodia Dominick , Bukoba 

WAJUMBE  wa kikao cha ushauri (RCC) mkoa wa Kagera kimepinga kugawanywa kwa majimbo mawili ya uchaguzi ya Biharamlo na Ngara baada ya majimbo hayo kutokidhi vigezo vya kugawanywa huku kikao hicho kikipitisha jimbo la Nkenge kubadilishwa jina na kuwa jimbo la Misenyi.

Wajumbe wa kikao hicho kilichokaa kwa dharula Machi 17, 2025 majira ya mchana kilikuwa na agenda moja ya kubadilisha jina la jimbo la Nkenge kwenda jina la jimbo la Misenyi na kugawanywa majimbo mawili ya Biharamlo pamoja na Ngara.

Asilimia 98 wamepinga kugawanywa kwa majimbo ya Ngara na Biharamlo baada ya majimbo hayo kukosa sifa za kugawanywa ikiwemo idadi ya watu kuwa ndogo huku wakikubali kubadilishwa jina la jimbo la Nkenge na kuwa jimbo la Misenyi.

Mwenyekiti wa kikao hicho mkuu wa mkoa wa Kagera, Fatma Mwassa akizungumza na wajumbe wa kikao hicho akawataka wajumbe wanaokubali majimbo kugawanywa kupiga kura ambapo asilimia 98 wamepiga kura ya hapana kupinga kugawanywa kwa majimbo hayo huku asilimia mbili wakikubali majimbo hayo kugawanywa.

      Mkuu wa mkoa wa Kagera Fatma Mwassa akizungumza 

Mwassa alipowawataka wajumbe hao kupiga kura ya kubadilishwa jina la jimbo la Nkenge na kuwa jimbo la Misenyi wajumbe hao wamekubali na kupiga kura ya ndiyo kwa asilimia 100.

Katibu Tawala msaidizi, utawala na rasmali watu mkoa wa Kagera Bwai Biseko, akizungumzia mapendekezo yaliyotolewa na baraza la madiwani na ofisi ya mkuu wa wilaya Misenyi amesema, jimbo la Nkenge libadilishwe na kuwa jimbo la Misenyi kutokana na kwamba,  halifahamiki na limekuwa likitumiwa na muhimili mmoja wa Bunge.

Biseko akizungumzia mapendekezo ya kugawanya majimbo katika wilaya ya Biharamlo na Ngara amesema kuwa, Biharamlo inazo kata 17 ina jumla ya wakazi 457,114,  jimbo moja la Biharamlo litakuwa na kata 11 huku jimbo la Nyakanazi likiwa na kata sita.

   Katibu Tawala msaidizi, utawala na rasmali watu mkoa wa Kagera Bwai Biseko akisoma mapendekezo ya kugawanya majimbo na kubadilishwa jina la jimbo la Nkenge na kuwa jimbo la Misenyi.

"Mapendekezo katika kugawanya wilaya ya Ngara ambayo ina kata 25, wakazi 383,092, jimbo la Ngara kusini litakuwa na kata 10 na jimbo la Ngara kaskazini kata 15" ameeleza Biseko .

Aidha kutokana na majimbo hayo kutokidhi vigezo vya idadi ya watu wajumbe wamekataa majimbo hayo kugawanywa richa ya baadhi yao kueleza sababu za kisiasa za kugawanya majimbo hayo kwa maslahi ya taifa.

Mzee Pius Ngeze kutoka baraza la wazee mkoa wa Kagera amewashawishi wajumbe hao kukubali kugawanywa kwa jimbo la Ngara kwa kigezo kuwa, jimbo lina makabila mawili ya Washubi na Wahangaza na kwa masirahi ya kisiasa akaomba wajumbe wakubali  ingawa zilipopigwa kura asilimia kubwa wamekataa kugawanywa kwa jimbo hilo.

Nichoraus Basimwaki katibu wa chama cha wafanyabiashara mkoa wa Kagera ni mmoja wa wajumbe waliokataa kugawanywa kwa majimbo hayo kutokana na kutokidhi vigezo.

Mkuu wa wilaya Ngara Kanali Mathias Kahabi amesema wilaya hiyo katika kikao cha ushauri kilichofanyika wilayani humo  kimekataa mapendekezo ya kutengwa majimbo ya uchaguzi katika wilaya ya hiyo.

No comments